JAJI WARIOBA ASEMA TUMSAIDIE RAIS MAGUFULI KUSHINDA VITA HII YA RASILIMALI ZA NCHI
Hivi karibuni Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt John
Pombe Magufuli alipokea ripoti ya Kamati ya kwanza na ya pili ya
uchunguzi wa makontena 277 ya mchanga wa madini (makinikia) yaliyokuwa
njiani kusafirishwa nje ya nchi na uchunguzi ulifanyika na kulibaini
ndani ya mchanga huo kuna dhahabu na madini mengine kwa asilimia kubwa.
Aidha, Mhe Rais amechukua hatua mbalimbali kulingana na ushauri wa kamati husika, pamoja na maamuzi yake kama Rais.
Kutokana na sakata la hilo, Idara ya Habari-MAELEZO imepata fursa ya
kufanya mahojiano na Waziri Mkuu na Makamu wa Kwanza wa Rais wa Jamhuri
ya Muungano wa Tanzania Mstaafu Mheshimiwa, Jaji Joseph Sinde Warioba
katika ofisi zake zilizopo Osterbay Jijini Dar-es-salaam.
SWALI: Ninanukuu maneno ya Baba wa Tafa, Hayati Mwl Julius Kambarage
Nyerere kuhusu raslimali za nchi na hususan madini alisema: “Madini yetu
tuliyonayo ni vema kuyaacha mpaka Watanzania watakapokuwa na ufahamu wa
kutosha wataamua kuyachimba” mwisho wa kunukuu nini maana yake?
JIBU: Mara baada ya Uhuru wa Tanganyika mwaka 1961 Hayati, Mwalimu
Julius Kambarage Nyerere alipokea nchi kama Waziri Mkuu wa kwanza wa
Tanganyika huru akiwa hana wataalamu zaidi ya madaktari 2 na yeye
mwenyewe ambaye alikuwa msomi kutoka chuo Kikuu cha Edinburg Uingereza.
Kwa hali hiyo, Mwalimu alikuwa sahihi usingeweza kuruhusu rasilimali za
nchi mfano madini kuchibwa na wageni kutoka nje maana yake Watanganyika
wangekuwa watazamaji tu bila kufaidika na lolote.
Mwalimu alihakikisha anawekeza katika elimu ambayo ilikuwa bure kuanzia
msingi hadi chuo kikuu elimu ndio msingi wa kuondoa Ujinga Umasikini na
Maradhi. Alitambua Watanganyika wakielimika na kupata utaalamu wa madini
ikiwani pamoja na uchimbaji watakuja kuyachimba na kufaidika.
SWALI:Tanzania ni kati ya nchi zilizobarikiwa kuwa na raslimali nyingi
za kila aina kuanzia madini, gesi, wanyamapori na hifadhi, misitu,
milima, maporomoko ya maji, mabonde maziwa makubwa kwa madogo, bahari ya
hindi na raslimali za mazao ya uvuvi, nchi yenye ardhi ya kutosha
watanzania wenye uwezo wa kufanyakazi kwa ufanisi . Unadhani nini tatizo
letu, nini cha kufanya?
JIBU: Sioni kama kuna tatizo la msingi lakini, ni suala la uelewa mara
nyingi kuna watu ambao huamini viongozi wao kwa kila kitu wanachosema.
Lazima wananchi wawe makini kwa sababu tatizo la watanzania ni maendeleo
kila mwananchi ana kiu ya kutaka tufikie mahala pazuri kama Taifa na
mimi nakubaliana nao kabisa.
Tuna rasilimali nyingi, ambazo kimsingi tukiweza kuzishughulikia kwa
makini kama lilivyoshughulikiwa suala la mchanga wa madini tutakuwa
mbali sana kiuchumi.
Mosi, tuangalie rasilimali ya madini kwa mapana yake na kushughulikia
wawekezaji wa ndani na wale wa nje, Barick na Acaccia ni sehemu ndogo
sana ya madini, tuangalie wachimaji wa ndani mfano Tanzanite ni aibu
madini yanachimbwa Manyara biashara hii inatokaje Mererani na kufanyika
Nairobi na New Delhi tujiulize kwa nini sio Arusha na Dar-Es-Salam.
Pili, upande wa rasilimali za maziwa makubwa tuliyonayo Victoria,
Tanganyika na Nyasa, Bahari ya Hindi kuanzia Moa mpaka Tanga kwa kiasi
gani tumeweza kutumia rasilimali za bahari maharamia wanakuja na meli
zao wanavuna tu na kuwatajirisha watu wengine. Mfano ziwa Victoria
linategemewa na wananchi wengi na sasa samaki hamna wamekwisha kwa
sababu hatusimamii rasilimali zetu ipasavyo. Maana suala sio kuvuna tu
tunalindaje hizi rasilimali zetu ili ziwepo leo kesho na vizazi vijavyo.
Tatu, Maliasili zetu za wanayamapori, mbuga za wanyama, vitalu vya
utalii unampaje mfanyabiashara kibali cha kuwinda miaka 99 yaani atumie
yeye, wanawe na wajukuu zake, watanzania watatumia lini, haya ni masuala
ya msingi kabisa ya kuangalia upya.
Nne, Ardhi Mwalimu alisema ili tuendelee tunahitaji vitu vine Watu,
Ardhi Siasa Safi na Uongozi Bora. Mwalimu Nyerere aliona ardhi ndio
kilakitu hivyo vyote tulivyovitaja vipo ardhini pamoja na sisi wanadamu
tunaitegemea kwa kila kitu. Maeneo mengi yaliyotumiwa na watu kwa
shughuli za ufugaji aidha , yana matumizi mengine kama nyumba, kilimo
cha mashamba makubwa, na idadi ya watu inaongezeka ardhi ni ileile hii
imesababisha migogoro ya watumiaji wa asili wa maeneo hayo na wenye
matumizi mengine tunatatuaje changamoto hii.
SWALI: Kwa kuwa umebobea katika masuala ya mikataba na sheria, ushauri
gani unautoa katika masuala yote ya raslimali za Tanzania? Nani
anatakiwa kusimamia raslimali hizi kwa ufanisi?
JIBU: Hii sio suala la mjua sheria au asiyejua, Mwanasheria lazima
anazijua sheria ndio maana amepewa dhamana. Linalojitokeza ni ukosefu wa
maadili ya uongozi, imani, utiii, uwazi na kutopenda nchi yako na
Watanzania ambao wamekupa dhamana ya kusimamia jambo.
Ndio maana Mwalimu Nyerere aliweka miiko ya uongozi, maadili ya uongozi
kwenye Azimio la Arusha. Kila mwananchi alikuwa anaweza kujua kiongozi
huyu muadilifu au sio muadilifu na anachukuliwa hatua kabla mambo
hayajaharibika.
Lakini sio vema kumhukumu mtu kwa jambo lolote lile, ni vema busara
itumike kujua kilichotokea mfano hili suala la mchanga wa madini ya
makinikia.
Jambo la msingi ni kutafuta suluhu itakayotupeleka mbele, tuone sera
zetu zikoje na zinatusaidiaje kulinda rasilimali za Taifa, tunarekebisha
vipi kuondoa tatizo, sheria na utendaji kwa ujumla. Naomba watanzania
tutoe maoni na mawazo yatakayoboresha sera, sheria na utendaji au
usimamizi wa rasilimali husika. Tunaweza kurudisha miiko na maadili ya
uongozi katika kusimamia rasilimali za nchi, kila Mtanzania ajue sio
mali yake ni ya Watanzania wote lazima aitunze vinginevyo atahukumiwa
kwa hilo.
SWALI: Ni ukweli usiopingika kuwa kosa limeshafanyika kwa hili
tuliloliona la mchanga wenye madini ya dhahabu, ambapo mhusika ambaye ni
mmiliki wa Kampuni inayobeba mchanga huo tangu 1998 hadi 2017 amewasili
nchini kuonana na viongozi wakuu wa serikali, nini maoni yako kuhusu
hili?
JIBU Sisi hatukushughulika na uchimbaji wa madini, lakini utafiti
tulifanya na kujua madini yapo na kuna maeneo mengi ambayo tumeweza
kufanya vizuri tunapata mapato, lakini hatukupata mapato yote.
Lakini hili la mchanga sitaki kulizungumzia sana nadhani watu
wanalichukulia kwa mihemko sioni faida kuzungumzia matukio badala ya
kuona tafsiri nzima nini cha kufanya.
Ninachokiona na cha muhimu sana, Watanzania wamepata faida kwa mara ya
kwanza tumeweza kujua mikataba ya madini ikipitiwa na Kamati zote mbili
zimetueleza maeneo yote ya mikataba waliyopitia na kuja na mapendekezo.
Tumetambua serikali ilikuwa na hisa au la mrahaba asilimia ngapi, kodi
kiasi gani, na mambo kama hayo.
Naomba jambo hili lisibague, tunasema hatupati mapato ya kutosha ni
lazima tujue kwa wachimbaji wa nje na wa ndani mfano nani anajua
wachimbaji wadogo wadogo wamechimba madini kiasi gani tangu 1998 hadi
2017 na kodi kiasi gani imeimngia. Tumepata nafasi sasa ya kuangalia
sera za kulinda rasilimali ya madini na nyingine zote katika nchi, kama
maliasili ya bahari tunaitumiaje, gesi, makaa ya mawe, chuma, wanyama
pori na mambo kama hayo.
Hii imetufungua macho sera ya aina gani sheria za aina gani, jinsi gani
ya kutunza na kutumia rasilimali hizi tulizopewa na mungu.
SWALI: Kwa kuwa wananchi tulio wengi tunaenda kwa mihemko bila
kupambanua hoja husika na kutoa mapendekezo au maoni yatakayo isaidia
serikali kuboresha sera sheria na utendaji wa rasilimali zetu unadhani
tatizo ni nini?
JIBU: Hatujaona uongozi wa Kitaifa katika hili suala la mchanga wa
makinikia ninachokiona mimi ni uongozi wa chama na siasa nyingi, sio
sahihi kabisa wanafanya makosa hili ni suala la rasilimali za nchi ni la
kila Mtanzania.
Viongozi hawawatendei haki wananchi wanaowakilisha, wanakuwa na mihemko
wanasema kamata, shitaki, wafunge. masuala ya kitaifa hayaendi hivyo
sisi sio Polisi wala Mahakama waachieni wenye kazi yao.
Uongozi wa kulalamika hautusaidii, wananchi wanataka kuona rasilimali
zetu zinanufaisha na kuboresha huduma za jamii ambazo wanalalamika kila
leo hakuna dawa, elimu isiyowajenga vijana na mambo kama hayo.
SWALI: Mhe. Kutokana na sakata la mchanga wa dhahabu uliokuwa
unasafirishwa nje ya nchi na matokeo yake watanzania tunajifunza nini
kwa maoni yako?
JIBU: Kabla ya tuona funzo tulilopata nadhani ni vema nikazungumzia
jambo hili, nimeona mjadala katika mitandao ya kijamii ambayo inafanywa
kwa mihemko. Ukiangalia vyombo vya habari au viongozi tumejikita katika
majina ya watu, nilikuwa nnaangalia Bunge wote wanakwenda kwa wale
waliotajwa unakuta kuna wanaochangia na wanaolaumu ama unsahangilia au
unalalamika kuhusu watu.
Kubwa ni utaratibu tulionao haitasaidia kulalamika juu ya watu
waliofanya kazi huko nyuma, tunaweza kuwauliza wahusika nini kilitokea
mpaka kufanya hivyo, lakini hilo sio kubwa, muhimu ni kutafuta ufumbuzi.
Mjadala huu umenikumbusha Awamu ya kwanza ya Mwalimu Nyerere viongozi
wote na wananchi walikuwa wanalalamika kila kitu wanachokikosa ni kwa
sababu ya wakoloni. Mwalimu akasema namnukuu: “Ni kweli wakoloni
wametuleta matatizo mengi sana lakini haitoshi kulaumu wakoloni bila
kuondoa mateso ya wananchi”. Mwalimu akaja na Waraka ambao ulikuwa
unaitwa “Act dont Argue” nadhani bado upo.
Waziri wa Katiba na Sheria Profesa Palamagamba Kabudi nanukuu amesema.
“Napenda kupata maoni tufanye nini kuhusu suala hili la mchanga wa
dhahabu (makinikia).” Namuunga mkono, sasa tumepata nafasi ya kutoa
maoni, mawazo ambayo ni muhimu sana maoni ya wadau katika uundaji wa
sera na sheria
Sasa hivi siamini kama hatuna utaalamu, nina hakika tunao wa kutosha
tatizo ni maadili na hilo lazima kutafuta ufumbuzi wake, pia tuunge
mkono serikali inachofanya kupambana na rushwa na ufisadi.
“Lakini tusijidanganye bishara ya madini, mafuta ina changamoto kubwa
sana duniani hususan Afrika, maana unapambana na watu wenye fedha
biashara hii popote utakapo kwenda, ambapo uchumi unategemea mafuta na
madini utaona jinsi wakubwa wanavyooneemeka na rasilimali hizo na
kuwaaacha wananchi wakiwa masikini mfano mzuri Nigeria”.
Pamoja na kuangalia maadili na nidhamu lazima kuwe na uwazi katika mikataba ni muhimu sana.
SWALI: Una maoni na mapendekezo yako kwa viongozi wote na Mhe Rais katika kumuunga mkono?
JIBU: Kwanza naliona hili la malumbano yatatugawa, waache tofauti zao
hii lawama ya madini ingekuwa ni mwanzo kwa kuleta mawazo na maoni ya
kutengeneza nchi yetu katika kulinda na kuzitumia rasilimali zote kwa
maendeleo ya taifa letu.
Viongozi msaidieni Rais kulishughulikia kwa pamoja hili si jambo la
chama wala Taasisi. Hakuna haja ya kupeana lawama ukishasema tumekosea
unatakiwa ueleze tufanye nini, sio kusema serikali ichukue hatua kwani
serikali ni nani si mimi na wewe sasa kwa nini hutaki wewe kulitolea
maoni?
Tujiamini nimeona katika malumbano hayo, wengine wanaonekana kama
hatujiami kama tukifanya hivi tunaweza kushitakiwa, mabadiliko yoyote
yana machungu yake. Tusije tukapoteza imani tuliyonayo maana tunaweza
tukapoteza mapato yetu lakini ni lazima tufanye kwa kujenga afya ya
rasilimali zetu.
Rais amekutana na mmiliki wa Barick na kila upande una msimamo wake,
tuiachie serikali na nina imani kabisa serikali itafanikiwa.
Kinachonishangaza ni mazungumzo ya baadhi ya viongozi kuwa serikali
ihakikishe tunapata hizo fedha walizo taja kwenye taarifa.
Nadhani hii sio sahihi, tuna imani na Viongozi wet wakuu haswa Rais,
lolote litakaloafikiwa tulipokee na kulikubali tusije kuanza kulumbana
ripoti imesema trilioni 108 ziko wapi? Pia nilisemee hili la dalili za
kupoteza imani, eti tukifanya hivyo tutashitakiwa, sababu ya mikataba na
wawekezaji hawatakuja mimi naamini watakuja tu rasilimali zipo kwetu
hawana jinsi.
SWALI: Msaada wako binafsi kwa Rais au maoni yako kwa Rais
JIBU: Sisi tupo, Uongozi ni suala la kupeana vijiti mimi natoka Mara
nimepitia utamaduni wa kabila langu kwa utamaduni wetu unafika mahali
unangatuka watu wanadhani kungatuka ni kustaafu hapana sio sahihi.
Ukitoka jandoni mzee wako lazima angatuke maana umekuwa sehemu ya jeshi
la kabila na yeyote ambaye kijana wake yuko kwenye jeshi yeye anatoka.
Wazee hawaingii katika mambo ya vijana na sisi tupo lakini hatutaki
kuingilia utendaji wao kama sisi tulivyoachiwa kuendesha nchi, ila Rais
akituhitaji tupo tayari kwa ajili ya ushauri anaweza kuukubali au
kuukataa. Nataka nimhakikishie kwa hili tupo pamoja na tutatoa maoni ya
kurutubisha Sera, Sheria na Utendaji katika rasilimali za nchi hii.
Comments
Post a Comment