HISTORIA YA MUUZA MADAWA YA KULEVYA NGULI DUNIANI PABO ESCOBAR
Katika
milima inayotazamana na mji wa Medellín nchini Colombia, yapo majengo ya
kifahari kabisa ndani ya milima hiyo ambayo kwa sasa majengo haya
yanatumika kama nyumba ya watawa wa Kanisa Katoliki lakini kabla ya
watawa hawa kupewa majengo haya mwaka 2007, majengo haya yalikuwa ni
gereza ambalo lilijengwa mwaka 1991 kumuhifadhi mfungwa maalumu raia wa
Colombia.Gereza hili lilikuwa ni tofauti kabisa na magereza yote ambayo
umewahi kuyasikia kwani gereza hili licha ya kuwa mali ya serikali
lakini michoro yake ilichorwa na kubuniwa na mfungwa mwenyewe.
Si hivyo
tu, bali hata maaskari magereza ambao walikuwa wanalinda gereza hili
walichaguliwa na mfungwa mwenyewe na hata polisi wa nchi ya Colombia
walikuwa hawaruhusiwi kusogolea gereza hilo hata umbali wa maili 12.
Kama hiyo haitoshi gereza hili lilikuwa na uwanja wa mpira wa miguu,
lilikuwa na bafu lenye Jaccuzi, lilikuwa na bar, lilikuwa na maporomoko
ya maji (water falls) yaliyobuniwa kiustadi, na pia chumba (selo)
alicholala mfungwa huyu kilikuwa na kitanda kikubwa cha duara chenye
kuzunguka pamoja na televisheni kubwa.
Kama hii
haitoshi kwenye gereza hilo pia kulikuwa na chumba maalumu cha michezo
ya watoto maalumu kwa ajili ya watoto wa mfungwa huyo pindi akitembelewa
na familia yake. Na pia ndani ya gereza kuliwekwa darubini kali
(Telescope) ya kumuwezesha mfungwa huyo kuangalia katika mji wa Medellín
ambako familia ya mfungwa huyu iliishi na kila siku jioni walitoka nje
kibarazani kuongea naye kwenye simu huku akiwatazama kwa darubini.
Gereza
hili lilijulikana kama La Catedral (the cathedral) na lilimuhifadhi
mfungwa muhimu zaidi duniani na binadamu aliyeifinyanga na kuifanya
biashara ya mihadarati iwe jinsi ilivyo hivi leo. Marafiki zake wa
karibu walipenda kumuita El Patrón (The Boss) au El Zar de la Cocaína
(The Tsar of Cocaine) lakini alipozaliwa wazazi wake walimuita Pablo
Emilio Escober Gaviria au kwa kifupi Pablo Escobar kama ulimwengu wote
ulivyomtambua.
The Boss
Akiwa
mtoto wa tatu kwenye familia ya watoto saba ambapo baba yake alikuwa ni
mkulima na mama yeke mwalimu wa shule ya chekechea, Pablo Escobar
alikuwa ni mwenye kutamani mambo mazito na mwenye maono makubwa tangu
angali mtoto.
Akiwa
bado kwenye umri wa makumi (teenage) Pablo mara kwa mara aliwaambia
ndugu zake na marafiki zake kuwa anataka awe na utajiri wa kiasi cha
Peso Milioni 1 za Colombia (COL$ 1 Million) atakapofikisha umri wa miaka
22.
Ndoto
hizi zilimfanya ashindwe kumaliza Chuo kikuu alipokuwa anasoma
(Universidad Autónoma LatinoAmericana of Madellín) na kujiingiza katika
biashara za halali na haramu na hatimaye aliacha masomo chuoni. Moja ya
biashara zake haramu za kwanza kabisa akiwa kijana chini ya miaka 21
ilikuwa ni kutengeneza vyeti bandia vya stashahada vya chuo alichokuwa
anasoma na kuwauzia watu waliohitaji kwa ajili ya kwenda kupata ajira.
Pamoja na
biashara hiyo pia Pablo alijihusisha na kusambaza mizigo ya sigara
zilizokuwa haziruhusiwi nchini Colombia (Marlboro), pia alifanya kazi
kama mlinzi binafsi (bodyguard) pamoja na wizi wa magari.
Moja ya
matukio muhimu ya ujana wa Pablo yaliyochangia kuamsha ari ndani yake na
kumfanya atamani kuwa moja wa manguli wa biashara haramu lilikuwa ni
tukio ambalo alipofikisha miaka 26 alifanikiwa kuweka benki (Cash
Deposit) kiasi cha Peso Millioni 100 za Colombia (COL$ 100 Million).
Mafanikio
haya yaliwasha taa ndani yake na kuamsha ari ya kutaka kuwa 'Papa'
katika 'Dunia' ya siri ya ulimwengu wa biashara haramu.
Katika
miaka ya 1970 mamlaka ya kupambana na matumizi mabaya ya madawa nchini
marekani (US Drug Enforcement Agency) waliwahi kutangaza kuwa wamewekeza
zaidi rasilimali zao kupambana na matumizi na uingizaji wa dawa aina ya
Heroin nchini marekani na kwa maoni yao walisema kuwa wanadhani madawa
aina ya Cocaine hayakuwa na uwezo wa kuleta uteja (addiction) au kufanya
mtumiaji kuwa muhalifu tofauti na dawa aina ya Heroin. Hivyo basi
walielekeza nguvu zao zote na rasilimali kupambana na biashara ya
usafirishaji wa Heroin kama kipaumbele cha kazi zao.
Hili
lilikuwa ni kosa kubwa sana kwa upande wao. Kwani kijana Pablo aliona
mwanya huu na udhaifu huu upande wa DEA au pengine tusema kwamba Pablo
alifahamu zaidi kuhusu ulimwengu wa mihadarati kuliko DEA.
Kitu
kikubwa ambacho Pablo alikiona na watu wakiwemo DEA hawakukiona ilikuwa
ni uwezekano (potential) ya kuifanya Cocaine kuwa moja ya madawa yenye
soko zaidi Amerika ya Kaskazini. Katika kipindi hiki kulikuwa na
watumiaji wachache sana wa Cocaine nchini marekani lakini Pablo aliona
fursa ya kuifanya mihadarati hiyo kuwa moja ya madawa yenye kuhitajika
sana nchini marekani na ulimwenguni kiujumla.
Kutokana
na uzoefu wake wa ulimwengu wa kihalifu, Pablo aligundua kuwa zao la
Coca linalimwa nchini Bolivia ambalo linatumika kutengeneza Cocaine ni
bora zaidi kuliko Coca inayolimwa nchini kwake Colombia. Hivyo basi
Pablo akadhamiria kuwa kama anaingia kwenye biashara hii ya kusafirisha
Cocaine ni lazima mihadarati yake iwe tofauti na bora zaidi kuliko
Cocaine nyingine watu waliyozoea kutumia. Akadhamiria kufanya Cocaine
yake iwe daraja la kwanza ili kuvutia watumiaji na kufanya soko likue
kwa haraka.
Kama
sehemu ya mkakati wake wa kuingia rasmi kwenye biashara ya kusafirisha
mihadarati aina ya Cocaine, mwaka 1975 kijana Pablo alisafiri mpaka
nchini Bolivia kukutana na Roberto Suaréz Goméz ambaye marafiki zake
walipenda kumuita El Padrino (The Godfather) kiongozi wa Genge
lililoitwa La Corparacíon (The Corporation). Suaréz alikuwa ndiye mtu
pekee anayeendesha na kuratibu uzalishaji wa zao la Coca katika nchi ya
Bolivia na Peru. Kipindi hiki Suaréz tayari alikuwa na mtandao mkubwa
katika America ya kusini na alikuwa na jina kubwa, ushawishi na nguvu ya
kijeshi hivyo haikuwa kazi rahisi kwa kijana Pablo kumshawishi Suaréz
akubali kufanya naye biashara.
Huyu
bwana Suaréz alikuwa na nguvu kiasi kwamba alikuwa na jeshi lake binafsi
la anga (Air force) na wanajeshi wa miguu 1,500 ambao walipatiwa
mafunzo nchini libya.
Pablo
alitumia uwezo wake wa kujieleza na uzoefu wake wa ulimwengu wa kihalifu
kumshawishi Suaréz na kumueleza kuhusu mkakati wake wa kuiteka biashara
ya mihadarati ya Cocaine nchini marekani na akamdadavulia jinsi ambavyo
yeye Suaréz atapata utajiri wa kupindukia kama atakubali kufanya nae
biashara.
Pia Pablo
alimpa wazo Suaréz kuwa atumie ushawishi wake alionao serikalini
(Suaréz alikuwa amefanikiwa kumpenyeza Mdogo wake serikalini na kuwa
Waziri wa mambo ya ndani) ahakikishe wanakutana na kiongozi wa Cuba
Fidel Castro ili wamuombe kuwa mshirika wao katika mambo kadhaa.
Suala
hili lilifanikiwa kwani Pablo na Suaréz walipata fursa adhimu na
wakakutana na Fidel Castro na ombi lao kubwa kwake lilikuwa ni
kuwaruhusu kupitisha mizigo yao nchini kwake Cuba na nchi za jirani
pasipo bugudha. Pia walimuomba aruhusu ndege zao za mizigo zitue kwenye
viwanja vya ndege vya Cuba na kujaza mafuta pale inapobidi kufanya
hivyo.
Castro
akawakubalia kwa masharti mawili, moja ni kwamba atakuwa anawachaji
mamilioni ya dola za marekani kwa huduma hizo na pili mihadarati hiyo
isiuzwe ndani ya Amerika ya Kusini bali isafirishwe na kuuzwa Marekani
ambapo Fidel Castro alisisitiza kuwa atafurahi akiona vijana wa Mabepari
wakiharibika na mihadarati.
Masharti
yote mawili haya yakakubaliwa na Pablo na Suaréz kisha wakarejea
Bolivia. Baada ya kufanya mazungumzo juu ya namna watakavyo fanya
biashara hatimae Pablo na Suaréz walifikia muafaka na kwa mzigo wake wa
kwanza alioununua nchini Bolivia kutoka kwa Suaréz ulikuwa ni kilo 14 za
unga gafi za Cocaine.
Baada ya
unga gafi kufikishwa nchini Colombia kwenye mji wa Medellín, Pablo
alikuwa ameandaa jengo maalum la ghorofa mbili ambalo alilitengeneza
kuwa maabara maalumu ambapo Cocaine gafi kutoka Bolivia ilichanganywa na
maligafi nyingine na kuboreshwa zaidi kikemia na hatimaye kupata
Cocaine daraja la kwanza aliyoihitaji tayari kusafirishwa nchini
Marekani kwa 'walaji'.
Baada ya
Cocaine kutoka kwa Pablo kuingia kwenye soko la Marekani uhitaji na
biashara ya mihadarati ya Cocaine ilipaa kwa kasi ya ajabu na Pablo
Escobar akaanzisha rasmi genge lake la biashara ya mihadarati na
akaliita Medellíne Cartel.
Pablo
akatengeneza mtandao madhubuti wa wasambazaji wa mihadarati yake katika
miji ya Florida na California pamoja na majimbo mengine ya Marekani.
Pia
akabuni njia mpya ya kupitisha mihadarati kupitia Bahamasi katika kisiwa
cha Norman's Cay takribani kilomita 350 kusini mashariki mwa pwani ya
Florida.
Ili
kufanikisha zaidi azma yake Pablo Escobar alinunua nusu ya ardhi ya
kisiwa cha Norman's Cay na nusu nyingine ikanunuliwa na swahiba wake wa
kimarekani aliyeitwa Robert Vesco ambaye pia alikuwa ndiye
anashughulikia masuala yake ya kibenki na uhasibu.
Katika
Kisiwa hiki Pablo alitengeneza uwanja wa ndege, bandari, hoteli, nyumba
za kuishi pamoja na ghala kubwa la jokofu maalumu kwa ajili ya kuhifadhi
mizigo ya Cocaine kabla ya kuisafirisha kwenda marekani. Kwa kifupi
hapa ndipo kilikuwa kitovu cha kibiashara cha Genge lake la Medellíne
Cartel.
Pablo
Escobar alikuwa amepania haswa kuliteka soko la Cocaine Amerika ya
Kaskazini na hii ilijidhihirisha kutokana na juhudi zake alizozifanya
kibiashara ili mda wote awe hatua kadhaa mbele tofauti na washindani
wenzake kibiashara.
Pablo
Escobar alikuwa amepania haswa kuliteka soko la Cocaine Amerika ya
Kaskazini na hii ilijidhihirisha kutokana na juhudi zake alizozifanya
kibiashara ili mda wote awe hatua kadhaa mbele tofauti na washindani
wenzake kibiashara.
Ili
kufanikisha usafirishaji wa mizigo yake kwa ufasaha na uhakika Pablo
alinunua ndege za mizigo 15 za ukubwa wa kati na helikopta 6. Pia
alinunua Nyambizi ndogo mbili (submarines) kwa ajili ya kusafirisha
mizigo mikubwa ya mihadarati.
Hadi
kufikia mwaka 1985 Pablo alikuwa anasafirisha takribani tani 70 mpaka 80
za Cocaine kwa mwezi na alikuwa ameshikilia asilimia 80 (80%) ya soko
la mihadarati la Marekani.
Na katika
kipindi hiki Genge lake la Medellíne Cartel lilikuwa linaingiza kipato
cha cha Dola Milioni 70 kwa siku (Shilingi Bilioni 140 za Kitanzania) na
mapato yao kwa mwaka mzima yalifikia Dola Bilioni 21.9. (Shilingi
Trilioni 46 za Kitanzania).
Katika
miaka ya 1990 utajiri wake binafsi ulifikia kiasi cha Dola za kimarekani
Bilioni 30 ambazo ni sawa na Dola Bilioni 54 kwa hesabu za sasa
(Shilingi Trilioni 110 za kitanzania)
Ni katika
kipindi hiki ambacho Jarida maarufu la Forbes lilimuorodhesha Pablo
Escobar kama mtu namba 5 tajiri zaidi ulimwenguni na muhalifu tajiri
zaidi katika historia ya Ulimwengu.
Kutokana
na nguvu na ushawishi alionao, Pablo aliteuliwa na serikali kama mjumbe
wa baraza la wawakilishi la Colombia (Chamber of Representatives of
Colombia) kupitia chama cha Kiliberali Cha Colombia (Colombia Liberal
Party).
Moja ya
majukumu muhimu aliyoyafanya akiwa kama Mjumbe wa Baraza la Wawakilishi
kilikuwa ni kwenda kuiwakilisha Serikali ya Colombia katika sherehe za
kuapishwa kwa Waziri Mkuu mpya wa Uhispania Bw. Felipe González mwaka
1982 ambapo Pablo alitumia nafasi hii ya Safari ya kiserikali nchini
Uhispania kuanzisha tawi jipya la Genge lake la Medellíne Cartel katika
nchi ya Uhispania.
Hacienda Nápoles: Pepo Juu ya Uso wa Dunia
Kutokana
na utajiri uliopitiliza wa Pablo Escobar alithubutu kutengeneza makazi
ya kuishi ambayo namna pekee ya kuyaelezea ni kana kwamba
alijitengenezea 'pepo' akiwa duniani.
Katika
mji mdogo wa Puerto Triunfo, takribani kilomita 150 kutoka katika mji wa
Medellín, Pablo alinunua eneo lenye ukubwa wa Kilomita za mraba 20 na
kujenga makazi yake na familia yake na akayaita makazi haya Hacienda
Nápoles (Naples Estate).
Licha ya
majengo ya kifahari ya kuishi yeye na familia yake pia makazi haya
yaliwekwa anasa lukuki zisizomothirika. Ndani ya makazi haya kulikuwa na
Uwanja wa ndege binafsi (private airport), bustani maalumu ya sanamu za
kuchonga na kufinyanga (Sculpture Park), kulikuwa na sehemu maalumu ya
kuhifadhi magari ya kifahari na pikipiki za kifahari kwa ajili ya
kutazama tu (collection), kulikuwa na uwanja wa mbio za magari magogo
(kart racing track), kulikuwa na uwanja wa mapigano ya ng'ombe
(Bullring), na pia ndani ya makazi haya kulikuwa na mbuga ya wanyama ya
kutengeneza (Zoo) ambapo Pablo alikusanya aina mbali mbali za wanyama
kutoka kila kona ya dunia na kuwaweka humo.
Katika
geti la kuingia kwenye 'pepo' ya Pablo sehemu ya juu ya geti
ilininginizwa ndege (ndege halisi) kama urembo. Ndege hii aina ya Piper
PA-18 Super Cub yenye namba ya mkia HK-617-P hii ndio ilikuwa ndege ya
kwanza aliyoitumia Pablo kuingiza mzigo wake wa kwanza wa Cocaine nchini
Marekani.
Hapa katika 'pepo' hii ndipo ambapo Pablo Escobar aliishi yeye na familia yake.
Plata o Plomo
Moja ya
vitu muhimu vya kihalifu alivyovifanya Pablo na kufanikiwa kuibuka kama
kinara wa uhalifu Amerika ya kusini ilikuwa ni kutekeleza sera yake
aliyoianzisha yeye mwenyewe ili kuidhibiti serikali na vyombo vya ulinzi
ambapo sera hii aliita "Plata o Plomo" (silver of lead (fedha au
risasi)). Akiwa na maana kwamba kama wewe ni mtu wa serikali na ikitokea
mmesigana basi atakupa fedha (rushwa) kama ukikataa kupokea fedha basi
anakupiga risasi.
Sera hii
ilimfanya Pablo aogopwe na watendaji wa serikali pamoja na vyombo vya
usalama na ikapelekea wengi kukubali 'Plata' (silver (fedha)) wakihofia
kupoteza maisha endapo wangekataa fedha kutoka kwa Pablo. Hii ilimsaidia
Pablo Escobar kuwa na vibaraka wengi katika serikali na vyombo vya
ulinzi na usalama.
Lakini
sera hii iligharimu maisha ya watu wengi sana wale ambao walikataa
kupokea fedha kutoka kwa Pablo na mojawapo ya matukio mawili
yanayokumbukwa sana ya utekelezaji wa sera ya 'Plata o Plomo' ni haya:-
Mosi; Uvamizi wa Mahakama Kuu ya Colombia 1985.
Mwaka
1985 baada ya mabishano ya muda mrefu bungeni kuhusu vifungu vya
kikatiba vinavyokataza raia wa nchi ya Colombia kukabidhiwa kwa nchi ya
kigeni akiwa kama muhalifu hatimae serikali ikafungua kesi ya kikatiba
mahakama kuu ya Colombia ikitaka ruhusu ya kukabidhi baadhi ya wahalifu
kwa serikali ya Marekani ikitokea wakikamatwa.
Suala
hili lilikuwa linamlenga moja kwa moja Pablo Escobar kwani serikali ya
Colombia ilikuwa inapewa shinikizo kubwa na Marekani kuwa wafanye
marekebisho ya katiba ili iruhusu raia wa nchi hiyo ambaye ni muhalifu
kukabidhiwa kwa nchi ya kigeni. Haya yalikuwa ni maandalizi endapo
ikitokea Pablo Escobar akikamatwa.
Pablo
akajitahidi kwa juhudi zake zote kuhonga serikalini na hata kutoa onyo
kuwa mabadiliko hayo ya kikatiba yasifanyike lakini serikali iliendelea
na mchakato kutokana na shinikizo walikuwa wanapata kutoka kwa marekani.
Inajulikana
kwamba Pablo mara kwa mara alikuwa akiapa mbele za watu wake wa karibu
kuwa kamwe hatokubali kufungwa katika nchi ya marekani na alikuwa na
msemo anaoupenda kuusema kwamba "ni heri kuwa kaburini Colombia kuliko
kuwa hai kwenye gereza la Marekani".
Baada ya
juhudi zake zote za kuionya serikali kutobadili katiba kushindikana
hatimaye Pablo akakodi kikundi cha wapiganaji wa msituni kilichoitwa
M-19 ili wasaidie kumaliza tatizo lake.
Siku ya
Novemba 6, 1985 majaji 25 wa mahakama kuu walikuwa katika vikao vya
mwisho kujadili na hatimae waweze kuridhia mabadiliko hayo ya katiba
lakini kabla ya kumaliza vikao vyao na kuridhia mabadiliko hayo
walivamiwa na wapiganaji wa kikundi cha M-19.
Wapiganaji
hawa walivamia na kuteka mahakama kuu kwa muda wa siku mbili na zaidi
ya nusu ya majaji waliuwawa na waliosalia walichukuliwa mateka.
Majaji
hawa waliochukuliwa mateka walikuja kutumiaka kama sharti muhimu la
kuibana serikali waache kurekebisha katiba ili waweze kuachiwa. Baada ya
serikali kukubali kuacha kubadili katiba hasa kipengele cha kukabidhi
wahalifu kwa nchi ya kigeni, majaji wote waliotekwa wakaachiwa.
Pili; Mauaji Mgombea Urais Luis Carlos Galán
Tukio la
pili linalokumbukwa sana la utekelezaji wa sera ya 'Plata o Plomo'
lilikuwa ni mauaji ya mgombea Urais wa Colombia aliyeitwa Luis Carlos
Galán. Galán alikuwa anaongoza kwenye kura za maoni nchi nzima na
alikuwa anatarajiwa kushinda kwenye uchaguzi mkuu wa urais wa Colombia
wa mwaka 1990.
Moja ya
sera kubwa aliyokuwa anaihubiri kila kona ya nchi ilikuwa ni kupambaa na
Magenge ya Mihadarati hasa hasa akililenga Genge la Medellíne Cartel na
kiongozi wake Pablo Escobar.
Pablo
alimtumia barua kadhaa ambazo ziliwekwa nje ya nyumba yake kwenye
kisanduku cha barua akimuonya na kumtaka aachane na sera hiyo ya
kumsakama yeye pamoja na washirika wake wa Medellíne Cartel lakini Bwana
Galán alionekana dhahiri amezamilia kutekeleza sera hiyo endapo
angechaguliwa kuwa rais wa Colombia.
Akiwa
katika kampeni Bwana Galán alifanikiwa kufika kwenye mji wa Madellín
ambapo Pablo alikuwa na ushawishi mkubwa na wapo wananchi waliojaribu
kumuua Galán kwa kumrushia guruneti la kutupa kwa roketi (Rocket
Propelled grenade) lakini kwa bahati nzuri Bwana Galán akisalimika.
Baada ya
hapo Pablo akakodi wadunguaji maalumu kufatilia nyendo za Galán na
akawapa amri ya kumpiga risasi mara tu wakipata upenyo wa kufanya hivyo.
Wiki
kadhaa baadae akiwa kwenye kampeni katika mji wa Saocho Kiranga
alipokwenda kuhutubia wafuasi wake wapatao 10,000 waliokusanyika
wakisubiri kumsikia na mara baada ya kuwasili na kupanda jukwaani
kuhutubia kabla hajatoa hata salamu kwa wafuasi wake alidunguliwa na
risasi na kupoteza maisha papo hapo.
Tukio
hili lilizua taharuki nchi nzima na imekuwa skendali yenye utata mpaka
leo hii nchini Colombia kwani kuna tetesi kuwa viongozi wa serikali,
polisi, pamoja na mashushushu walishirikiana na Pablo Escobar kutekeleza
mauaji haya.
Licha ya
Pablo kuonekana kama adui namba moja nchini marekani na baadhi wa
watendaji wa serikali ya Colombia hali ili kuwa tofauti kwa raia
masikini wa Colombia ambao wengi wao walimuona kama shujaa wao na katika
mji aliozaliwa na kushi wa Medellín anaonekana zaidi ya shujaa kwani
mpaka leo hii wanamuona kama ni aina fulani hivi ya masihi walipewa.
Hii inatokana na umahiri wa Pablo Escobar katika mahusiano na jamii iliyokuwa inamzunguka.
Pablo alikuwa ni mtu mwenye kusaidia masikini nchini Colombia pengine kuliko hata serikali yenyewe.
Pablo
alijitolea kweli kweli katika kuboresha huduma za jamii kama vile
kujenga mahospitali, shule, nyumba za wazee, nyumba za kuishi kwa ajili
ya masikini na akawekeza fedha nyungi kujenga miundo mbinu ya Kanisa
Katoliki na nyumba za kuabudia. Pia Pablo alijenga vya kuendeleza watoto
katika mpira wa miguu, alifadhili klabu mbali mbali za wakubwa za mpira
wa miguu na alijenga viwanja vya kisasa kabisa vya mpira na michezo
mingine.
Ilifikia hatua mpaka Pablo alikuwa anawapa fedha taslimu wananchi wa Madellíne ili waweze kujikimu kimaisha.
Mambo haya yote yalifanya wananchi wampende na kufumbia macho uhalifu wote aliokuwa anaufanya.
Kwa mfano
katika mji wa Madellín ilifikia hatua kana kwamba wananchi wote
walikuwa ni walinzi wake binafsi kwani walikuwa wakimtonya kila
walipoona polisi wageni wakiingia hata kwa siri kwenye mji huo. Au
wakati mwingine walikuwa wakitoa taarifa za uongo au kukataa kusema
chochote pindi wakiulizwa na vyombo vya ulinzi kuhusu nyendo za Pablo.
Hii
ilimfanya Pablo azidi kujizatiti na kuongeza mahaba kwa wakazi wa
Medellín na raia wa Colombia kwa ujumla.Pablo ataendelea kua na
mahusuano mazuri na wananchi.
VITA KUU YA KWANZA YA MAGENGE YA MIHADARATI.
Kuna msemo wanasema 'adui wa adui yako ni rafiki yako'! Swali: je, inakuwaje pale adui wa adui yako akitishia maslahi yako??
Adui wa Adui yako (Kikao cha Kwanza)
Hapo
baadae nitaeleza kwa kifupi kuhusu kuibuka kwa genge lingine ambalo nalo
lilishamiri katika biashara ya Cocaine lililoitwa Cali Cartel hivyo
kufanya kuwe na uwepo wa magenge mawili yanayoshindana kibiashara yaani
Medellín Cartel chini ya Pablo Escobar na Cali Cartel.
Licha ya
ushindani wao wa kibiashara mwaka 1983 iliwabidi washirikiane kwa sababu
za msingi kabisa. kuliibuka kikundi cha wahuni waliokuwa wanateka watu
na kudai fedha kutoka kwa ndugu ili wawaachie. Baada ya kuteka ndugu
kadhaa wa viongozi wa serikali wahuni hawa wakaanza kuteka ndugu wa
mabosi wa Cartels na kudai pesa.
Moja ya
watu muhimu waliowateka alikuwa ni Marta Nieves Ochoa dada wa moja ya
mabosi wa Cali Cartel na watekaji walikuwa wanataka wapewe dila milioni
10 ili wamuachie. Hii ndio ilikuwa sababu kubwa ya mabosi wa Cali Cartel
na Medellín Cartel kukutana ili kuweka mkakati maalumu ambao utapeleka
ujumbe kwa wahuni na watekaji wote kuwa familia za mabosi wa Magenge ya
mihadarati ni mwiko kuzigusa.
Katika
kikao hiki cha kwanza Medellín Cartel na Cali Cartel waliunda kikosi
kazi maalumu walichokiita Muerte a Secuestradores (Death to kidnappers
(Kifo kwa Watekaji)) au kama kilivyojulikana kwa kifupi MAS.
Kila Genge lilichangia fedha, vifaa (silaha), na askari kwa ajili ya kikosi kazi cha MAS.
Kesho
yake baada ya kikundi hiki kuundwa ndege ilipita juu ya uwanja wa mpira
wa miguu kuliko kuwa na mechi kubwa ikifanyika na kumwaga vipeperushi
kuhusu kutangaza zawadi nono kwa yeyeto atakayetoa taarifa kuhusu
kufahamu lolote juu ya wahuni wanaoteka watu na kushinikiza wapewe hela.
Jioni ya siku hiyo taarifa muhimu kutoka kwa wananchi zikaanza kuletwa
na kikosi kazi cha MAS mara moja kikaanza kukamata wahuni wa vikundi vya
utekaji na kuwatesa huku wakiwarekodi na kuwatumia wenzao wanaoshikilia
dada wa bosi wa Cali Cartel.
Ndani ya
siku tatu Marta Naives dada wa bosi wa Cali Cartel aliachiwa akiwa
salama salimini na huo ndio ukawa mwisho wa magenge ya wahuni kuteka
wanafamilia wa mabosi wa magenge ya mihadarati.
Kama ni rafiki yako, anaweza kuwa mshirika wako: Kikao cha Pili
Licha ya
ushindani wa kibiashara kuendelea kuwepo kati ya Medellin Cartel ya
Pablo Escobar na Cali Cartel lakini kufanikiwa kwa mkakati wa MAS
kuliwapa moyo kuwa yako maeneo mengine mengi wanayoweza kufanya kwa
kushirikiana na yakawa na faida kwa pande zote mbili.
Sehemu ya
kwanza ambayo waliona inaweza kuwa na faida kwa pande zote mbili
ilikuwa ni Cali Cartel kukubali Pablo Escobar aweze kupitisha fedha zake
haramu katika benki ya First InterAmericans Bank ambayo ilikuwa
inamilikiwa na maswahiba wa mabosi wa Cali Cartel. Hii ilikuwa na faida
kwa kubwa kwa Pablo kwani ilikuwa ni njia rahisi na salama kwake kuweza
kusafisha fedha zake haramu lakini pia ilikuwa na faida upande wa
wamiliki wa benki maswahiba wa mabosi wa Cali Cartel kwani nao wangepata
faida kwa kutoa huduma hiyo kwa Pablo kutokana mabilioni ya dola ya
dola ambayo atakuwa anayapitisha kwenye benki yao.
Sehemu ya
pili waliyokubaliana kushirikiana ilikuwa ni namna ya kuratibu bei ya
Cocaine mtaani, kuratibu viwango vya ubora wa uzalishaji na njia salama
za kusafirisha mizigo.
Sehemu ya
tatu walikubaliana kuhusu kugawana soko. Cali Cartel wakakubaliwa
kuendesha biashara kwenye jiji la New York na Medellín Cartel ya Pablo
Escobar wakapewa Florida na Miami. Jiji la Los Angels likaachwa kama
sehemu huru ambayo yeyote anaweza kufanya biashara.
Kwa pamoja wakasonga na biashara ikashamiri.
Rafiki yako anapotishia maslahi yako: Vita Kuu ya Kwanza (Pablo Escobar VS Cali Cartel).
Biashara
ya madawa ya kulevya katika America ya Kusini na duniani kote kwa miaka
yote imetawaliwa na vita kati ya magenge yanayopambana ili kumiliki na
kujipatia ushawishi zaidi katika soko. Lakini katika historia hakuna
vita ya magenge ya mihadarati iliyotisha na kuitikisa Marekani na
Amerika ya Kusini kama vita kati Medellín Cartel ya Pablo Escobar dhidi
ya Cali Cartel.
Vita hii ilitishia hata usalama wa uwepo wa Taifa la Colombia na kuleta aibu kubwa kwa serikali za Colombia na Marekani.
Lakini kabla sijaeleza chochote kuhusu vita hii, nieleze kwa ufupi tu kuhusu Cali Cartel.
The Cali Cartel
Cali
Catel ilianzishwa mwishoni mwa miaka ya 1970 kikiwa kama kikundi maalumu
cha wapiganaji kilichokuwa kinatumiwa na Pablo Escobar na kilijulikana
kama Las Chemas.
Moja wapo
ya kazi walizozifanya kwa mafanikio ilikuwa ni utekaji wa raia wawili
wa nchi wa uswisi na wakalipwa kiasi cha dola laki saba.
Baada ya
malipo haya washirika wa kikundi cha Las Chemas wakajitenga na Pablo
Escobar na kukimbilia kusini mwa nchi ya Colombia katika mji wa Cali na
wakatumia fedha hiyo kuanzisha biashara yao ya mihadarati na
wakafahamika kama The Cali Cartel.
Baada ya
biashara yao kuanza kukua wakafanikiwa kuwashawishi wanajeshi kadhaa
waasi na kujiunga nao katika biashara na wakafanikiwa kuwapata wengi.
Uwepo wa
wanajeshi katika Cali Cartel unadhihirishwa na mfumo wao wa kibiashara
pamoja na uwezo wao wa kufanya upelelezi na ushushushu
(counterintelligence).
Kwa mfano
mfumo wao wa kibiashara ulikuwa tofauti na Medellín Cartel ya Pablo
Escobar ambayo yenyewe ilikuwa ni genge linalomilikiwa na mtu mmoja
(Pablo) ambapo Cali Cartel wenyewe walikuwa ni muunganiko wa
wafanyabiashara wanaojitegemea wanaounda genge/mtandao mmoja wa
mihadarati (Cali Cartel).
Kwa
upande wa ushushushu na upelelezi walikuwa mahili kiasi kwamba katika
baadhi ya ripoti za CIA walikuwa wanawaita kwa jina la utani "Cali the
KGB", wakiwafananisha na shirika la upelelezi la Urusi ya kipindi hicho.
Turejee kwenye...'Vita Kuu'
Ushindani
mkubwa wa kibiashara kati ya magenge haya mawili unaweza kuwa sababu
kubwa ya wao kuingia vitani lakini hii iliepushwa kutokana na vikao vya
makubaliano walivyokaa awalinkuhusu kugawana soko.
Sababu
kubwa zaidi na ya msingi iliyochochea vita hii ilikuwa ni Pablo kuamua
kuacha kuheshimu makubaliano akiyoingia na Cali Cartel kutokana na genge
hili kujihusisha na vitendo ambavyo Pablo alivipinga kwa nguvu zote.
Haijulikani
ni kichaa gani kiliwapata viongozi wa ngazi za juu wa Cali Cartel
lakini ilipofika miaka ya kati kati ya 1980 Cali Carteli wakaanza
kujihusisha na imani zenye utata za "Kusafisha Kizazi/jamii" (Social
Cleansing). Cali Cartel walisimamia mauaji ya mamia ya watu kwenye mji
wa Cali pasipo sababu ya msingi wakidai kuwa watu hao wanaichafua Cali.
Mauaji
yao yaliwalenga walemavu, machangudoa, watu wanajihusisha na mapenzi ya
jinsia moja, watoto wa mitaani, na watu wasio kuwa na makazi.
Baada ya
kuwaua waliwaandika maandishi kifuania "Cali limpia, Cali linda" (Clean
Cali, beautiful Cali (Cali nadhifu, Cali inayopendeza)
Vitendo
hivi vilimkera Pablo na ikampa sababu ya kutokuheshimu makubaliano yake
na Cali Cartel kuhusu kugawana soko na akaamuru watu wake wafanye
biashara nchini marekani katika mji wowote ule wanaojisikia.
Kitu hiki
kikiwakera viongozi wa Cali Cartel na ili kumuonyesha kuwa wamechukizwa
wakaanza kutoa ufadhili kwa kikundi cha wapiganaji kilichokuwa
kinajiita Los Pepes amacho ni kifupi cha Los Perseguidos por Pablo
Escobar (People Persecuted by Pablo Escobar (watu walioumizwa na Pablo
Escobar)).
Kikundi
hiki kilikuwa kinaundwa na ndugu za watu waliouawa na Pablo au Wapambe
wake na walikuwa wamejiapiza kumsaka na kumuua Pablo popote alipo.
Kitendo cha mabosi wa Cali Cartel kuanza kukipa ufadhili kikundi hiki
kilichochea moto wa vita ya magenge amabao haukuwahi kuonekana hapo
kabla.
Katika
kipindi hiki Colombia ilishuhudia mauaji ya kutisha ambapo wafuasi wa
magenge yote mawili walikuwa wakitafutana usiku na mchana. Mauaji haya
yaliwahusu mpaka marafiki, ndugu na wanafamilia wa makundi yote mawili.
Katika mwaka 1988 pekee idadi ya vifo ilifikia zaidi ya watu 21,000 na
mwaka 1989 idadi iliongezeka mpaka vifo zaidi ya 28,000.
Hiki
kilikuwa ni moja ya vipindi vigumu zaidi kiusalama kwa Pablo kwani
alikuwa na lundo la maadui waliokuwa wakimtafuta. Kulikuwa na serikali
ya marekani inamtafuta, serikali ya Colombia inamtafuta, Kikundi cha Los
Pepes kinamtafuta, na genge la Cali Cartel linamtafuta. Kutokana na
suala la usalama kuwa tete mno ilimlazimu aame kutoka katika 'pepo' yake
ya Hacienda Napolés na kwenda kujificha katika nyumba za maficho juu ya
milima ya mji wa Madellín.
Ilikuwa
inambidi abadili makazi mpaka mara nne kwa siku moja. Nyumba zake nyingi
hizi za juu ya milima alikuwa anazitumia kuhifadhi pesa na silaha na
ilitokea siku walienda kwenye nyumba yake iliyopo karibia kabisa na
kilele cha mlima na ilikuwa iko ndani ya msitu mnene.
Siku hii
kulikuwa na baridi lisilomithirika na kutokana na nyumba hii kujengwa
maalumu kwa ajili ya kuhifadhi fedha na silaha haikuwa na mfumo wa joto
wala umeme. Ilifikia kipindi cha usiku baridi lilizidi na kupitiliza
kiwangi cha kawaida mpaka ikaanza kutishia afya ya mtoto wake wa kike
aliyekuwa naye pamoja na familia yake.
Kutokana
na kutokuwepo na namna nyingine yeyote ya kupasha moto nyumba hiyo ili
kupunguza baridi, ili mbidi Pablo achome moto maburungutu ya fedha usiku
kucha ili kuipatia joto familia yake na hasa mtoto wake wa kike ambaye
alionekana kuathiriwa zaidi na baridi. Mpaka asubuhi kunakucha na baridi
kupungua kufikia kiwango cha kawaida Pablo alikuwa ameteketeza
maburungutu ya hela ya kiasi cha dola milioni mbili za kimarekani.
Baada ya
Juhudi za Cali Cartel kumpata Pablo kutozaa matunda, walitoa kandarasi
kwa Jorge Selcado ambaye alikuwa ni muhandisi na Mwanajeshi. Jorge
alikuwa maarufu kwa kuandaa timu maalumu za mauaji ya kuratibiwa
kiumakini (assassination teams) na mara zote mipango yake inakuwa ya
mafanikio.
Baada ya
Jorge kupewa 'ofa' hii na mabosi wa Cali Cartel aliwasiliana na watu
wake ambao walikuwa ni wanajeshi wa kukodi (mercenaries) kutoka nchini
uingereza ambao walikuwa wamewahi kutumikia katika jeshi la Uingereza
kitengo maalumu cha Anga (SAS - Special Air Services).
Timu hii
ilikuwa na watu kumi mbili na iliwasili Colombia na kufanya mazoezi kwa
miezi kadhaa ili kujiandaa na zoezi lililopo mbele yao. Walifahamu kuwa
kwa kipindi hicho Pablo alikuwa amejificha mahali kusiko julikana kwenye
milima, hivyo walisubiri wapate taarifa kuwa amerejea kwenye 'pepo'
yake ya Hacienda ili wafanye shambulio la kushitukiza.
Siku hiyo
haikuchelewa sana kwani timu ya Mpira ambayo Pablo alikuwa anaishabikia
na kuifadhili ilifanikiwa kuchukua ubingwa wa ligi kuu ya Colombia.
Hivyo Pablo alirejea jijini Medellín ili ajumuike kusherehekea ushindi
huo.
Kikosi
hiki kilichotumwa kumuua Pablo walijiandaa na Chopa mbili za kivita
zilizobeba silaha nzito na mpango wao ulikuwa wamshitukize Pablo nyakati
za asubuhi na kufanya shambulizi nyumbani kwake Hacienda Napolés.
Ili
mpango huu uwe na ufanisi walikubaliana kuwa washambulie kutokea nyuma
ya milima na chopa ziruke katika mfumo maalumu wa kijeshi wa usawa wa
chini chini kabisa (nap-to-earth) ili wasiweze kuonekana kutokea mbali.
Keshi
yake chopa ziliruka kuelekea Hacienda Napolés kama walivyopanga wapitie
nyuma ya milima huku zikiruka chini chini, lakini wakiwa kwenye milima
hiyo kwa bahati mbaya chopa moja ilimshinda rubani kutokana na kuruka
chini chini na ikagonga kwenye mlima na kudondoka.
Zoezi
ambalo kilipangwa kuwa la kwenda kushambulia na kumuua Pablo likageka
kuwa ni zoezi la uokoaji na mpango huu ukaishia hapo hapo.
Zoezi
ambalo kilipangwa kuwa la kwenda kushambulia na kumuua Pablo likageka
kuwa ni zoezi la uokoaji na mpango huu ukaishia hapo hapo.
Baada ya kufeli kwa zoezi hili serikali ya Colombia iliwasiliana na Pablo kujaribu kumuomba ajisalimishe.
Waliharibu
kumbembeleza kwa kila namna ambayo waliweza na kumuahidi watakubaliana
na masharti yoyote atakayoyasema. Serikali ilifikia kipindi walikuwa
'desperate' kutokana na aibu waliyokuwa wanaipata kimataifa kwa
kushindwa kumdhibiti muhalifu mmoja aliyeifanya nchi yao ya Colombia
mpaka kubatizwa jina la 'Capital of death' (mji wa kifo). Hivyo
matamanio yao ilikuwa tu kuutangazia ulimwengu kuwa wamemkamata Pablo.
Baada ya
Pablo kutafakari kwa kina na kuona jinsi usalama wake na familia yake
kuwa ni mdogo kutokana na maadui wanaomzunguka kila kona akakubali ombi
la serikali kujisalimisha lakini akawapa masharti matatu.
Moja,
kipindi hicho serikali ilikuwa imefanya mchakato na kubadili kifungu cha
katiba kuruhusu kukabithi raia wake kwa nchi za kigeni (extradition).
Pablo akawaeleza waitishe kikao maalumu cha Bunge na kurudisha kifungu
cha zamani kinachokataza raia wa nchi hiyo kukabidhiwa kwa nchi za
kigeni. Serikali ikakubaliana na sharti hili. Kikaitishwa kikao maalumu
cha bunge na kifungu hicho cha katiba kikarejebishwa.
Pili,
Pablo aliwapa sharti kuwa anataka atengenezewe gereza maalumu katika
sehemu atakayoichagua yeye na yeye na wahandisi wake ndio watakaochora
michoro ya namna gereza hilo anavyotaka liwe. Serikali wakakubaliana na
sharti hili na gereza kikajengwa kama ambavyo Pablo aliamuru.
(Tafadhali
rejea aya ya kwanza ya makala hii kuhusu namna ambavyo gereza hili
likikuwa tofauti na gereza lingine lolote duniani).
Gereza
hili lilipo malizika Pablo mwenyewe alilipa jina La Catedral (The
Cathedral) lakini watu wengi walilipa jina la utani 'Club Escobar' na
wengine waliliita 'Hotel Cathedral'.
Sharti la tatu aliwaambia serikali yeye ndiye atakaye chagua askari wa kumlinda. Serikali ikakubali pia sharti hili.
Baada ya
masharti yote kukamilika yakafanyika makubakiano maalumu ya kisheria
ambapo Pablo Escobar licha ya uhalifu wa kutisha alioufanya kwa miaka
karibia ishirini alipewa adhabu ya kifungo cha miaka mitano pekee.
Baada ya makubaliano. Pablo alijisalimisha na kupelekwa kwenye makazi yake mapya, gereza la La Catedral.
Baada ya
Pablo kujisalimisha mwaka 1991 serikali ilitangazia ulimwengu kwa
mbwembwe zote kuwa wamemkamata Pablo Escobar na amehifadhiwa katiba
gereza la siri.
Ikikuwa
ni kweli kuwa Pablo alikuwa gerezani lakini ulimwengu mzima walifichwa
ukweli halisi kwani katika gereza hilo Pablo aliishi kama mfalme na
aliendelea kutoa maagizo kwa wafuasi wake na kuendesha biashara yake ya
miahadarati akiwa ndani ya La Catedral. Tena kwa sasa Pablo inawezekana
alifurahi zaidi kwani alikuwa uhakika wa usalama wake kutokana na
kulindwa na jeshi la serikali ambao wao walimuona kama mfungwa huku yeye
akiwaona kama walinzi wake binafsi.
Kitendo
hiki kiliwaumiza sana Cali Cartel ambao walihangaika usiku na mchana
wafahamu hili gereza lilipo. Baada ya mwaka mkoja wakapata taarifa
kuhusu mahala ambapo gereza anahifadhiwa Pablo. Kutokana na ulinzi mkali
wa kijeshi waling'amua fika kuwa hawataweza kuvamia gereza hilo na
kumuua Pablo hivyo mshauri wao wa masuala ya kijeshi akawashauri Jorge
Selcado akawashauri kuwa namna pekee ya kumuua Pablo ndani ya La
Cathedral ni kulipua gereza hilo kwa mabomu mazito kwa kutumia ndege
maalumu ya kivita.
Cali
Cartel wakanunua ndege ya kivita aina ya A-37 Dragonfly na wakaweza
kupata dili la magendo kuuziwa mabomu mazito ya kivita ya uzito wa
paundi 500 kutoka kwa generali wa jeshi ka El Salvador.
Hivyo Jorge akarusha ndege na kuelekea El Salvador katika uwanja wa ndege wa kiraia asubuhi alfajiri ili kuchukua mabomu.
Kwa
bahati mbaya mabomu hayo yalikuwa kwenye maboksi makubwa manne na ndege
aliyoenda nayo Jorge ilikuwa ndogo isingeweza kubeba maboksi yote hayo.
Wakahangaika kunga'aniza maboksi yaenee ndani ya ndege lakini maboksi
matatu pekee ndiyo yalienea. Zoezi hilo la magendo lililopaswa kuchukua
dakika chache tu likatumia zaidi ya dakika ishirini ambapo palianza
kupambazuka na watu kufika uwanjani hivyo ikambidi Jorge aruke na
maboksi matatu na kulitelekeza boksi moja uwanjani hapo.
Baada ya
raia kushikwa na butwaa kuhusu walichokiona hatimae polisi walifika na
baada ya masaa machache walipewa taarifa za siri kuhusu mpango huo wa
Cali Cartel kununua mabomu hayo ili kulipua La Catedral. Skandali hii
iliteka vyombo vya habari siku hiyo na ikapekekea Cali Cartel kuachana
na mpango huo wa kulipua La Catedral waliamini kuwa taarifa hiyo itakuwa
imemfikia Escobar na ameshachukua tahadhali.
KIFO CHA PABLO El Mágico
Licha ya
serikali kufahamu kuwa Pablo alikuwa anaendelea na biashara zake licha
ya kuwa ndani ya gereza serikali ilifumfumbia macho kadiri ambavyo
ulimwengu ulivyo amini kuwa Pablo Escobar yuko gerezani anajutia.
Lakini
uvumilivu huu uliisha mara baada ya kuzuka skendali katika vyombo vya
habari kwamba Pablo aliwaita marafiki zake wa kibiashara wanne walioko
uraiani waende akawape maelekezo, walipofika huko aliamuru walinzi
wanaomlinda wawapigwe risasi marafiki zake hao kwa madai kuwa
wamemdhulumu hela na ilisemekana miili yao ilifukiwa ndani ya gereza.
Skandali
hii ilikuwa kubwa kiasi kwamba ilitishia kurudisha tena upya zama za
serikali kuumiza kichwa kuhusu Pablo. Ili kuepusha mambo yasiharibike
kabisa serikali ikaamua kuwa Pablo inabidi afungwe kwenye gereza maalumu
la kijeshi na aishi maisha ya kifungwa kama mfungwa mwingine yeyote.
Kutikana
ma makubaliano kuwa polisi wengine isipokuwa wanajeshi wanaomlinda
hawaruhusiwi kusogea hata maili 12 karibu na La Catedral, hivyo serikali
ikatuma waziri muandamizi na maafisa wengine watatu wa ngazi za juu
serikalini kumpelekea taarifa hiyo Pablo kuwa anaamishwa gereza.
Baada ya
kupewa taarifa hii Pablo akiwageuzia kibao na kuamuru wanajeshi
wanaomlinda waweke chini ya ulinzi vuongozi hao wa serikali. (Kumbuka
wanajeshi hawa wanaomlinda aliwachagua yeye hivyo ni dhahiri walikuwa
maswahiba wake wakikuwa tayari kumtii Pablo kuliko rais wa nchi)
Baada ya
taarifa kufika serikalini kuwa Pablo amewaweka chini ya ulinzi viongozi
wa serikali waliotumwa kufanya nae mazungumzo juu kuhamishwa gereza.
Serikali ikatuma kikosi cha wanajeshi 600 kulizunguka gereza hilo na
kumtaka Pablo ajisalimishe.
Pablo
akawajibu kuwa wakithubutu hata kukanyaga hatua moja ndani ya uzio wa La
Catedral basi ataamuru viongozi hao aliowashikilia mateka wapigwe
risasi.
Mabishano
haya yalidumu kwa takribani masaa kumi mpaka ambapo giza lilipoingia
kikosi cha wanajeshi waliokuwa wamelizunguka gereza walivamia ndani ya
La Catedral lakini jambo la ajabu waliwakuta viongozi hao wa serikali
wamefugwa kwenye viti na kuzibwa midomo lakini walikuwa salama salimini
ila Pablo na wapambe wake hawakuwepo. Na watu waliokutwa ndani ya La
Catedral walidai Pablo na wapambe wake hajaonekana/ameondoka kwa
taribani masaa manne yaliyopiata.
Ni kwa
jinsi gani Pablo aliwatoroka wanajeshi amabo walikuwa wamelizunguka
gereza kila kona kitendawili hiki mpaka leo hakuna aliyekitegea.
Hakukuwa na njia yoyote ya chini kwa chini wala handaki, hivyo huu utata
wa jinsi alivyowatoroka haujapata jibu la kuridhisha mpaka leo.
Kufumba
na kufumbua jinamizi la aibu kwa serikali ya Colombia na Marekani
kilikuwa limerudi. Na serikali zote mbili ziliapa kwamba sasa imetosha
ni lazima walizike jinamizi hili.
Kamandi
ya Oparesheni maalumu za kijeshi za marekani (Joint Special Operations
Command) kikaunda kikosi kazi maalumu cha kijeshi kilichoelekea nchini
Colombia kuungana na kikosi maalumu cha jeshi la Colombia kikichoundwa
maakumu kwa ajili ya kumsaka Pablo kilichoitwa 'Search Block' na kwa
pamoja wakaanza msako mkali wa kumtafuta Pablo. Pia walishirikiana na
kikundi cha Los Pepes kilichoapa kumteketeza Pablo na ukoo wake wote
ambao walitumia mwanya wa msako huu kuua watu 300 waliokuwa na uhusiano
na Pablo, yaani ndugu zake, marafiki na wafanyabiashara wenza.
Baada ya
mwaka mzima wa msako mkali hatimae siku ya desemba 2, 1993 jeshi la
Colombia lilifanikiwa kunasa mawasiliano ya simu kati ya Pablo na
wasaidizi wake. Wakatumia 'triangulation technology' kung'amua mahali
alipo ambapo alikuwa katika mtaa wa Los Olivos katika mji wa Madellín.
Baada ya kufanikiwa kufahamu nyumba aliyojihifadhi pasipo kupoteza mda
wakafanya shambulio la kushitukiza.
Wakati wanawafanyia shambulio hili la kushitukiza Pablo alikuwa yupo na mlinzi wake binafsi mmoja tu Alvaro de Jesús.
Baada ya
kuanza kushambuliwa nao wakarudisha mashambulio ya risasi kwa vikosi vya
jeshi la serikali. Majibizano haya ya risadi yalidumu kwa dakika kadhaa
ndipo Pablo na mlinzi wake wakakubali kuwa hakuna namna wao watu wawili
wataweza kuwashinda kikosi kizima cha kijeshi chenye silaha nzito.
Hivyo wakaamua warushe risasi huku wakiwa wanakinbilia juu ya paa la
nyumba. Lakini kabla hawajafika juu kabisa ya paa la nyumba mlinzi wa
Pablo alidunguliwa na risasi na kufariki papo hapo na Pablo mwenyewe
alipigwa risasi mguuni na akajikongoja mpaka juu ya paa.
Baada ya
wanajeshi wa serikali kuvamia nyumba na kufika juu ya paa walimkuta
Pablo amelala chini amefariki akiwa na tundu la risasi aliyopigwa kwenye
sikio kwenda ndani ya kichwa.
Haijulikani
ni nani alimpiga hii risasi lakini marafiki zake wa karibu pamoja na
kaka yake wa kuzaliwa wanasema kwamba siku zote Pablo akikuwa anasema
kuwa hatokubali kupigwa risasi ya mwisho na adui yake. Kama ikitokea
ameshambukiwa na adui na hana namna ya kujiokoa basi atajipiga risasi
sikioni itokee upande wa pili. Serikali haijawahi kupinga au
kuthibitisha suala hili la Pablo kujipiga risasi mwenyewe lakini huo
ndio ulikuwa mwisho wa Pablo juu ya uso wa dunia.
Mpaka leo
hii nchini Colombia hasa katika mji wa Madellín kila mwaka wanafanya
kumbu kumbu ya kifo cha Pablo kama shujaa wao lakini kwa watu wengi
duniani Pablo amebakia kama muhalifu aliyeitesa na kuisumbua dunia
kadiri atakavyo.
Binafsi
nadhani namna nzuri ya kumkumbuka Pablo ni sentesi moja maridhawa
iliyotolewa na Virginia Vallejo aliposema; Amando a Pablo, Odiando a
Escobar.! Akimaanisha kuwa lazima kuna upande fulani wa nafsi yako
utampenda Pablo kama mtu mwenyenye jitihada, umahiri na uthubutu lakini
upande wa pili wa nafsi lazima utamchukia Escobar kutokana na uhalifu
wake.
Lakini
kwa namna yeyote ile historia ya Dunia itaendelea kumkumbuka Pablo kama
binadamu aliyeufinyanga ulimwengu wa siri na hatari wa biashara haramu
na kuufanya uwe jinsi ulivyo leo hii. Vizazi vyote vijavyo vitaendelea
kusimulia historia ya kusisimua ya Pablo El Mágico. Pablo El Zar de la
Cocaína. Pablo Emilio Escobar
Comments
Post a Comment