Halima Mdee na Ester Bulaya Kulipwa nusu Mshahara
Wabunge wa Chadema, Halima
Mdee (Kawe) na Ester Bulaya (Bunda Mjini) ambao wamesimamishwa
kuhudhuria vikao vya Bunge, watalipwa nusu mshahara na posho
zinazoambatana nao kwa miezi kumi.
Stahiki hizo ni kwa mujibu wa kanuni
ya 75 ya Bunge inayosema, “mbunge aliyesimamishwa hataingia tena sehemu
yoyote ya ukumbi na maeneo ya Bunge kwa muda wote atakapokuwa
amesimamishwa na atalipwa nusu mshahara na nusu posho zinazoambatana na
mshahara huo.”
Vilevile, kutokana na uamuzi huo
wabunge hao watakosa siku 65 za Bunge zinazojumuisha siku 25 zilizobaki
za Bunge la bajeti linaloendelea, Bunge la Oktoba na lile la Februari,
2018. Vikao vya mabunge hayo mawili; la Oktoba na Februari kila kimoja
huwa na mikutano ya wiki mbili mbili.
Wabunge hao walisimamishwa juzi kwa
azimio la Bunge licha ya kutokuwapo au kujitetea kutokana na tuhuma
zilizokuwa zinawakabili za kudharau kiti cha spika.
“Tukutane Bunge lijalo la bajeti,” alisema juzi Spika wa Bunge, Job Ndugai. Bunge la bajeti huanza mwezi Aprili.
Kufikia uamuzi huo, kamati ya haki,
maadili na madaraka ya Bunge ilisema iliwatafuta kwa simu wabunge hao,
lakini haikuwapata. Pia, iliwatumia ujumbe mfupi ambao haukujibiwa na
ilipowapelekea hati ya wito haikuwakuta majumbani kwao.
Kwa kutambua umuhimu wa agizo
ililonalo na kuzingatia matakwa ya kisheria, hati hizo ziliachwa baada
ya kuelezwa kwamba wahusika hawapo kwani wamesafiri. Baada ya jitihada
hizo kushindwa kuzaa matunda, kamati iliendelea kuwajadili bila wao
kuwapo na kutoa maazimio hayo.
Comments
Post a Comment