Fainali Uefa Champions League… Leo Shughuli Ipo

 NA MWANDISHI WETU
SIYO siri leo Jumamosi watu duniani watasimamisha shughuli zao kwa muda kutazama fainali ya 62 ya Ligi ya Mabingwa Ulaya inayozikutanisha Juventus na Real Madrid kwenye Uwanja wa Millennium.
Mwamuzi Felix Brych wa Ujerumani ndiye atakayechezesha mechi hii kali iliyojaa historia nyingi ambayo ni ngumu kutabiri mshindi moja kwa moja.
Mpaka inafi ka fainali chini ya Kocha Massimiliano Allegri, Juventus iliitoa Monaco kwa jumla ya mabao 4-1, wakishinda mabao 2-0 halafu 2-1. Madrid ikiongozwa na Kocha Zinedine Zidane iliitoa Atletico Madrid kwa jumla ya mabao 4-2.
Madrid ilishinda 3-0 halafu ikafungwa 2-1. Fainali hii inakumbusha fainali ya Uefa ya Mei 20, 1998 ambapo timu hizi zilikutana kwenye Uwanja wa Amsterdam na Madrid ikashinda bao 1-0 lililofungwa na Predrag Mijatovic.
Ni miaka 19 sasa tangu timu hizo zilipokutana katika fainali hiyo, wakati huo Zidane alikuwa akiichezea Juventus sambamba na Kocha wa Chelsea sasa, Antonio Conte.
Juventus licha ya kuwa na Zidane na Conte, kikosini ilikuwa na wachezaji kama Alessandro Del Piero, Filippo Inzaghi kipa Angelo Peruzzi. Madrid ilikuwa na nyota kama Raul, Fernando Morientes, Mijatovic na Davor Suker ila ilionekana kama haina nguvu ya kuifunga Juventus iliyokuwa chini ya Kocha Marcello Lippi.
Chini ya Kocha Jupp Heynckes, Madrid iliweza kujiandikia historia kwa kuifunga Juventus katika fainali hiyo ambayo wakati inachezwa, nyota wa Monaco, Kylian Mbappe alikuwa na umri wa miezi sita tu.
Mambo mengi yamebadilika ndani ya miaka hiyo 19, lakini ambalo halijabadilika ni kwamba Juventus na Madrid zimebaki kuwa timu kubwa Ulaya.
Kama ilivyo katika fainali ya leo, fainali ya mwaka 1998 pia ilichezeshwa na mwamuzi raia wa Ujerumani, Hellmut Krug. Pia  Madrid ilikuwa ugenini katika fainali iliyopita na hata leo!
WOTE KIBOKO
Timu zote zimeonyesha uwezo mkubwa hadi kufi ka fainali japokuwa Juventus ndiyo yenye rekodi nzuri ya kutofungwa hadi sasa.
Makocha wote yaani Zidane na Allegri wanajua namna ya kumsoma adui na kutumia vizuri wachezaji walionao katika kusaka ushindi na ukapatikana.
Hii ni mara ya 19 kwa timu hizi kukutana katika mechi za Uefa iwe Ligi ya Mabingwa Ulaya au Europa League hata Super Cup, jambo la kufurahisha ni timu zote zimeshinda mara nane na kutoka sare mbili.
Katika mara 18 walizokutana, Juventus imefunga mabao 21 na Madrid ina mabao 18.
Timu hizi zinaingia uwanjani leo zikiwa na mafanikio katika ligi zao kwani Madrid ina ubingwa wa Ligi Kuu Hispania ‘La Liga’, pia ni bingwa mtetezi wa fainali wanayocheza.
Kama Madrid ikitwaa ubingwa itakuwa imejiandikia historia ya kuwa timu ya kwanza kutetea ubingwa kwa kuutwaa mara mbili mfululizo.
Juventus nayo si timu ya kubeza kwani imeweza kutetea ubingwa wao wa Ligi Kuu Italia yaani Serie A licha ya kuwakosa nyota kadhaa iliokuwa nao msimu uliopita akiwemo Paul Pogba.
Hata hivyo, ikiwa na kipa mkongwe Gianluigi Buff on, Juventus iliweza kupambana msimu huu na kutwaa ubingwa chini ya Kocha Allegri.
VITA YA LEO CAR-DIFF
Mkongwe Buff on akiwa na umri wa miaka 39 atakuwa langoni Juventus kuwazuia Cristiano Ronaldo, Karim Benzema hata Gareth Bale na Isco wasimfunge, huyu hajawahi kutwaa taji la Uefa licha ya kucheza fainali mwaka 2003 na 2005 ambapo alipoteza zote dhidi ya AC Milan na Barcelona.
Madrid langoni itakuwa na Keylor Navas, huyu anatakiwa kuwa makini na mashuti ya Gonzalo Higuaín na Paulo Dybala.
Katika msimu huu, Buffon amefungwa mabao 28 katika mechi 42 na amecheza mechi 21 bila kuruhusu bao sawa na asilimia 50 ya mechi zote. Hata hivyo, ukuta imara wa Leonardo Bonucci na Giorgio Chiellini ni msaada mkubwa kwa Buff on.
Akiwa langoni katika robo fainali ya Uefa msimu huu, aliwadhibiti MSN yaani Lionel Messi, Luis Suarez na Neymar na hawakuweza kumfunga katika mechi mbili walizocheza.
Navas yeye kafungwa mabao 49 katika mechi 40 msimu huu huku akiwa hajaruhusu bao katika mechi saba tu, hata hivyo licha ya kuweza kuwalaumu mabeki, Navas msimu ujao asipoondoka Madrid anaweza kuwa kipa namba mbili.
Kama Buff on au Navas wakipata matatizo, katika benchi la Juventus yupo Neto ambaye amecheza mechi 14 msimu huu na msaidizi wa Navas ni Kiko Casilla aliyecheza mechi 19.
Katika beki ya kati, Madrid ni wazi itamkosa Pepe ambaye amevunjika mbavu hivyo bado Raphael Varane atacheza sambamba na Sergio Ramos.
Juventus yenyewe katika beki ya kati itakuwa na Bonucci na hiellini. Wakati Juventus katika kiungo ikiwa na Miralem Pjanić na
Alex Sandro, Madrid wao imani yao bado ipo kwa Toni Kroos na Casemiro kwani hao ndiyo wakata umeme wao.
Katika viungo washambuliaji pia burudani itakuwepo kati ya Sami Khedira na Luka Modric wa Madrid pia mashabiki watataka kujua ubora wa Dybala wa Juventus na Isco wa Madrid kama akianza.
HAPA RONALDO PALE HIGUAIN
Vita nyingine ya kujua nani bora itakuwa kati ya washambuliaji Ronaldo wa Madrid na Higuain wa Juventus kwani wawili hawa wamekuwa wakifanya vizuri katika michuano hii.
Ronaldo ana mabao 10 katika dakika 1,110 alizocheza katika Uefa msimu huu akipitwa bao moja na Messi, hivyo atataka afunge leo ili amfi kie ikiwezekana kumpita Messi.
Higuain yeye ana mabao matano sawa na Karim Benzema wa Madrid huku akiwa amecheza dakika 949. Nyuma ya Ronaldo yupo Benzema na pembeni ya Higuain yupo Mario Mandžukić.
ISCO AU BALE?
Swali lililopo sasa katika kikosi cha Madrid ni nani anaanza kati ya Bale au Isco, lakini Zidane amesema wote ni wazuri na mmoja anaweza kuanza pia anaweza kuwaanzisha wote kwa pamoja.
“Bale na Isco wote ni wachezaji wangu, ni wazuri na wanaweza kuamua matokeo kwenye mechi ngumu, mmoja anatakiwa aanze lakini nina nafasi ya kuwatumia wote kwa pamoja,” anasema Zidane.
MAKOCHA WAKO POA
Kocha wa Juventus, Allegri kuelekea mechi hii ya fainali anasema; “Sisi ni timu kubwa kama ilivyo kwao (Madrid), tumefika fainali kwa juhudi zetu kama timu, tunataka kuhakikisha tunarudi na kombe.
“Huu ni mtihani mkubwa wa pili kwangu nikiwa kocha. Nilipoteza fainali ya kwanza Berlin na Jumamosi (leo) tunatakiwa kushinda. Tunatakiwa kupata ushindi mkubwa.
“Katika miaka mitatu sisi tunacheza fainali hii kwa mara ya pili lakini wao hii ni fainali yao ya tatu katika miaka minne, wana nafasi ya kutwaa ubingwa lakini siyo kirahisi.”
Kwa upande wake, Zidane anasema; “Najua uchungu wa kufungwa katika fainali kama hii, nimewahi kufungwa katika fainali ya Uefa nikiwa naichezea Juventus mwaka 1997 na 1998.
“Nilitwaa ubingwa huu nikiichezea Madrid, nikiwa kocha msaidizi na sasa nataka kutwaa kwa mara nyingine ubingwa huu na kuandika historia, wapinzani ni wazuri ila kuna kitu umezidiana.”
MADRID JEZI ZA ZAMBARAU
Tofauti na ilivyozoeleka, Madrid katika mchezo huu itavaa jezi za rangi ya zambarau au pinki kwani ni mgeni
 na hiyo ndiyo jezi yao ya ugenini katika mechi zao.
Jezi ya Madrid ya rangi ya zambarau imethibitishwa waandaaji wa mechi ya leo, Shirikisho la Soka Ulaya (Uefa) kuwa ndiyo itakayovaliwa na timu hiyo wakati Juventus itavaa jezi zake za siku zote zenye rangi nyeupe na nyeusi.
MECHI YA UTATA
Msimu wa 1961/62 wa Ligi ya Mabingwa wakati huo Kombe la Klabu Bingwa, timu hizi ilibidi zicheze mechi tatu za robo fainali badala ya mbili tu, kwani mwanzo Madrid ilsihinda bao 1-0.
Waliporudiana Juventus ikashinda bao 1-0, lakini waliporudiana tena jijini Paris, Ufaransa, Madrid ikishinda mabao 3-1.
MADRID KIBOKO YA JUVENTUS
Licha ya kucheza mechi 18 na kufungana mara nane na kutoka sare mbili, bado Madrid ina mafanikio makubwa katika Uefa mbele ya Juventus kwani imetwaa ubingwa mara 11 na kufika fainali mara 14.
Juventus yenyewe imetwaa ubingwa mara mbili na kufika fainali mara nane tu.
BINGWA KULAMBA SH BILIONI 141
Mshindi wa mechi ya leo atapata zawadi ya euro milioni 15.5 sawa na Sh bilioni 38.3 wakati atakayefungwa atapata euro milioni 11 sawa na Sh bilioni 27.1. Bingwa atapata hadi euro milioni 57.2 sawa na Sh bilioni 141.4 ukijumlisha na bonasi zote.
Kombe la ubingwa lina urefu wa sentimita 74 na limetengezwa kwa madini ya fedha likiwa na uzito wa Kilogramu 11. Mbunifu wa kombe hili ni Jörg Stadelmann wa Bern, Uswisi ambaye alifanya kazi hiyo baada ya lile halisi la kwanza kupewa Madrid mwaka 1966 baada ya kutwaa ubingwa kwa mara ya sita. Lina thamani ya faranga za Uswisi 10,000 sawa na Sh milioni 24.
Kama ilivyo tangu msimu wa 2012/13, timu bingwa itapewa medali 40 za dhahabu na mshindi wa pili atapewa medali 40 pia.

Comments

Popular posts from this blog