BABU KIKONGWE WA MIAKA 80 AISHI KWA KULA UDONGO
Katika
hali ya kushangaza na kusikitisha sana, kikongwe mmoja aitwaye Athuman
Ngusa Kulaba (80) amekuwa akiishi kwa kula udongo wa nyumba anayoishi
kwa sababu ya kukosa chakula cha kibinadamu.Kikongwe huyo
alikutwa na Uwazi hivi karibuni nyumbani kwake, Chanika wilayani Ilala,
Mkoa wa Dar es Salaam baada ya majirani kusema kwamba wamekuwa
wakimshuhudia akipata mlo huo kwa karibu mwaka mmoja sasa.
Baada ya kuona hali yake inazidi kuwa mbaya, mjumbe wa eneo hilo, John
Kanguya na majirani zake walimchukuwa hadi kwenye Kituo cha Afya cha
Chanika kwa ajili ya kumpima afya yake ambapo madaktari walisema tayari
alipatwa na ugonjwa wa safura ambapo tumbo lake limejaa minyoo.
Uwazi lilishuhudia sehemu kubwa ya ukuta wa nyumba anayoishi kikongwe huyo ikiwa imemeguka kwa ajili ya kuchimbuliwa na kuliwa.
Majirani walilieleza Uwazi kwamba, nyumba anayoishi kikongwe huyo
aliachiwa kuilinda na mtu aliyetajwa kwa jina moja la Musada karibu
miaka 20 iliyopita bila kupewa huduma nyingine zikiwemo
fedha.Akizungumza na Uwazi kwa lugha ya Kisukuma, kikongwe huyo alikiri
kuwepo kwenye nyumba hiyo kwa miaka 20.
Alisema awali alikuwa akipewa pesa na tajiri yake lakini baadaye
utaratibu huo ukafa hivyo kwa sababu ya kukosa pesa ya kujikumu ndiyo
akaamua kula vyakula vya ajabu, ukiwemo udongo wa ukuta wa nyumba hiyo.
Alisema anawashukuru majirani wa eneo hilo ambao wameweza kutambua
maisha magumu anayoishi na kuamua kumpeleka hospitali na kumsaidia
chakula.“Kwa sasa naomba Watanzania wenzangu wanisaidie nauli ili niweze kurudi kwetu Bukene, Tabora, maisha hapa ni magumu sana,”alisema kikongwe huyo.
Kwa Watanzania watakaoguswa na maisha magumu ya mzee huyo wanaweza
kumsaidia nauli kwa kutumia namba ya simu ya Mwenyekiti wa Serikali ya
Mtaa Chanika, Mohamed Katungi 0784 295833 au 0715 295833.
Imeandikwa na Gazeti la Uwazi/gpl
Comments
Post a Comment