Wanachuo Wengi kukosa tena mikopo
BUNGE limeishauri serikali kuongeza bajeti ya Bodi ya Mikopo ya
Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB) baada ya kubaini wanafunzi wengi
watakosa fedha hizo mwakani kutokana na bajeti ndogo iliyotengwa.
Ushauri huo ulitolewa bungeni mjini hapa juzi na Kamati ya Kudumu ya
Bunge ya Huduma na Maendeleo ya Jamii ilipokuwa ikiwasilisha taarifa
yake kuhusu utekelezaji wa bajeti ya Wizara ya Elimu, Sayansi,
Teknolojia na Ufundi na makadirio ya wizara hiyo kwa mwaka ujao wa
fedha.
Akiwasilisha taarifa hiyo, mjumbe wa kamati hiyo, Hussein Bashe, alisema
wamebaini wanafunzi wengi watakosa mikopo mwaka ujao wa fedha licha ya
kuwa na ufaulu mzuri.
Alisema mwaka huu wa fedha wanafunzi 48,502 walijaza fomu kwa ukamilifu
lakini 25,555 tu ndiyo walipata mikopo na hivyo kuacha wengine 22,947
wakiwa hawana mikopo kutokana na bajeti iliyotengwa ya Sh. bilioni 427.5
kutotosheleza mahitaji.
Bashe ambaye pia ni Mbunge wa Nzega Mjini (CCM), alisema mwaka ujao wa
fedha HESLB imeombewa Sh. bilioni 427.5 (sawa na bajeti ya mwaka huu)
ilhali ufaulu wa wanafunzi waliohitimu kidato cha sita umeongezeka
kutoka asilimia 88 mwaka 2012 hadi kufikia asilimia 99 mwaka huu.
"Kamati inaona kwamba, suala la elimu ya juu ni haki ya msingi kwa watu wenye sifa," alisema.
"Kamati inashauri serikali kuongeza bajeti ya HESLB ili wanafunzi wengi
zaidi wanaostahili waweze kupata mikopo kwa maendeleo ya taifa letu."
Comments
Post a Comment