Vilio vya Mastaa kwa Wanafunzi Waliokufa Arusha

MAJONZI yamegubika nchi nzima kufuatia tukio la kihistoria la ajali ya basi lililosababisha vifo vya wanafunzi 33, walimu wawili na dereva iliyotokea Karatu mkoani Arusha.
Taarifa zinasema kuwa basi hilo aina Toyota Coaster lililokuwa limebeba wanafunzi, walimu na dereva ambalo ni mali ya Shule ya Lucky Vincent liliacha njia na kutumbukia katika Mto Marera uliyopo kilometa 25 kutoka kwenye geti la Hifadhi ya Taifa ya Ngorongoro.
Mbali na ajali hiyo kuwagusa wengi ndani na nje ya nchi, mastaa kutoka kwenye tasnia mbalimbali nchini wameibuka na kuzungumza na Wikenda, wakiweka wazi hisia zao za namna walivyoguswa na ajali hiyo. Wasikie;
PROFESA JAY:
Mungu azilaze roho za marehemu pema peponi. Kiukweli hili ni pigo kubwa sana kwa taifa letu, natoa pole sana kwa ndugu, jamaa wa marehemu na viongozi wote wa Mkoa wa Arusha kwa msiba huu mkubwa. Kwa mara nyingine tena kama taifa tunapoteza watoto wetu kwa idadi kubwa sana ambao wangeweza kuja kuwa hazina kubwa kwa taifa.
BABY MADAHA:
Barabara bado ni mbaya hasa kipindi hiki cha mvua, ajali bado zinaendelea tatizo ni nini? Miundombinu iendelee kuboreshwa na watu wazingatie hali ya hewa kabla ya kusafiri.
BARAKAH THE PRINCE:
Ni maafa ya taifa kwa jumla, kikubwa ni kuwaombea na kuwatakia wapumzike kwa amani. Kwa pamoja kama taifa tumepoteza nguvu kazi na ni vigumu kuipangua mipango ya Mungu.
DAYNA NYANGE:
Kiukweli hata sijui nianze kwa kuongea kitu gani! Lakini kiukweli sina nguvu kwa kile nilichokiona.
Hatukatai kuwa kifo tumeumbiwa binadamu, lakini ukweli ni kwamba mazingira mengine ya kifo yanaumiza sana na yanafanya watu waliobaki kuhuzunika sana.


ESTER KIAMA:
Natoa pole kwa wazazi wenzangu na wote ambao wameguswa na msiba huu kwa asilimia mia. Hii ni mipango ya Mungu na hatuwezi kuongea mengi, kikubwa tuwaombee waliotangulia mbele ya haki.
BILL NAS:
Bwana ametoa na Bwana ametwaa jina lake lihimidiwe. Mimi kama kaka ambaye nina wadogo zangu wanaosoma, roho imeniuma sana kuona kilichotokea.
Lakini hakuna namna, kikubwa ni kukubaliana na hali iliyotokea na kuwaombea ndugu zetu wapumzike kwa amani.
DUMA:
Imeniuma sana kama Mtanzania. Lakini kwa upande mwingine mimi ni baba, sasa kama baba ninafahamu uchungu wa watoto kwa hiyo ni swala linalouma mno na kusikitisha. Kikubwa nawapa pole wazazi wote ambao wameguswa na huu msiba mkubwa wa kitaifa.
AMANDA POSHI:
Inauma sijui hata nianzie wapi? Nimebubujikwa mno na machozi, kiukweli ninawaonea mno huruma wazazi wa hao watoto waliopoteza maisha.
LAMECK DITTO:
Natoa salamu za pole kwa familia zilizoguswa na tukio hili la kihistoria pamoja na Watanzania kwa jumla.
Ninachoweza kusema ni kwamba tuendelee kuwaombea kwa Mungu marehemu wapumzike kwa amani na majeruhi wapate auhueni.
ESHA BUHETI:
Kama mzazi nimeumizwa sana na ajali hiyo. Ukweli ni kwamba nilipozipata taarifa hizi kwa kuona kwenye mitandao ya kijamii nilihisi tumbo la uzazi likikata ghafla.
Kiukweli ni muhimu kwa wasimamizi wa shule na watu mbalimbali wanaofanya safari katika kipindi hiki kutazama hali ya hewa kabla ya kusafiri kuepusha matukio kama haya.
JENIFFER MGENDI:
Ni msiba ulionigusa sana kwani hakuna kitu kinachouma kwa mzazi kama msiba wa mtoto. Naomba mamlaka husika ziwe zinaangalia uwezo wa chombo na miundombinu yenyewe kwa ajili ya maisha ya Watanzania.
Ni kweli ajali hazizuiliki lakini sheria zikifuatwa tutapunguza idadi ya vifo na majeruhi kwa ajali ambazo zinaepukika.
JACKLINE WOLPER:
Nimesikitika sana kwa sababu ni msiba mzito na mkubwa kutokea kwa watoto kufariki dunia wengi kwa wakati mmoja. Inauma sana, nawapa pole wazazi walioondokewa na watoto wao.
Ushauri wangu kwa serikali, tunaweza kuziia vifo vingi kama hivi, tuchukue tahadhari na changamoto na tukatae vifo vya ajali kama hii ya watoto na nyingine.
Imeandaliwa na Boniphace Ngumije na Gabriel Ng’osha.

Comments

Popular posts from this blog