Tatizo la Kuvimba Miguu Wakati wa Ujauzito

KWA kawaida katika kipindi cha miezi mitatu ya mwisho ya ujauzito hali ya mama mjamzito miguu yake kujaa au kuvimba huonekana ni kawaida lakini ni mara chache aina hii ya kujaa hutokea usoni na mikononi endapo itatokea huko basi ni vyema kuchunguza matatizo mengine zaidi kama tutakayoyaona.  


CHANZO CHA TATIZO
Vyanzo vya tatizo hili vimegawanyika katika sehemu kuu mbili; kwanza ni hali ya utendaji kazi mwilini ambayo ni kawaida. Hii ni matokeo ya mabadiliko katika mfano wa homoni mwilini ambapo husababisha madini ya sodium kubaki mwilini badala ya kutolewa kwenye mkojo. Uvimbe huu wa miguu husababishwa na kizazi chenye mimba kugandamiza mshipa mkubwa wa vena unaochukuwa damu toka sehemu za chini za mwili kupeleka kwenye moyo. Mshipa huu unaitwa inferior vena cava.
Mgandamizo huu wa inferior vena cava hutokae endapo mwanamke atalalia mgongo. Kingine ni kuziba kwa mishipa ya damu ya kwenye nyonga iitwayo femoral veins.
Chanzo cha pili cha kuvimba miguu kinaitwa pathogic, au patholojia kunakosababishwa na magonjwa. Magonjwa hayo ni yale ya mishipa ya damu iitwayo kitaalamu deep venous thrombosis au kwa kifupi DVT na kupanda kwa shinikizo la damu kunakoathiri figo na kusababisha uwepo wa protini
kwenye mkojo, kitaalamu hali hii inaitwa preeclmpsia. 

DVT hutokea zaidi wakati wa ujauzito kwa kuwa katika kipindi hiki damu huwa na tabia ya kuganda haraka, kitaalamu tunaita hypercoagulable state na huchangiwa zaidi na kutojishughulisha sana na kutumia muda mwingi kukaa au kulala tu.
Na hali ya preeclmpsia kama tulivyoona husababishwa na shinikizo la damu kuwa juu, ingawa siyo lazima au siyo wanawake wote wenye shinikizo la damu wanavimba miguu. Endapo hali ya kuvimba miguu itaendelea kwa muda mrefu na itaendelea kuongezeka, mama mjamzito ataanza kuhisi miguu inawasha, atajikuna na kupata vidonda, hali hii kitaalamu inaitwa selulitis.

UCHUNGUZI
Siyo kila mwanamke mjamzito anayevimba miguu ana shinikizo la juu la damu au ugonjwa wa preeclampsia ‘DVT’. Ni vizuri uchunguzi wa kina ufanyike na kuangalia uwezekano wa hali hiyo kuwa ni kifiziolojia. Uchunguzi utazingatia jinsi tatizo lilivyoanza, limechukua muda gani, linaongezeka wakati gani na linapungua wakati gani, kwa kulala au analalia upande gani, analalia mgongo au upande wa kushoto?
Pia kuchunguza visababishi hatarishi.
Visababishi hatarishi kwa ugonjwa wa DVT ni mishipa ya damu ya vena kutojaa vizuri, kuumia sehemu za miguuni, matatizo ya mfumo wa mwili yanayosababisha damu kuganda, uvutaji wa sigara kwa wanawake hasa wajawazito, mwanamke mjamzito kuwa mvivu wa kujishughulisha, muda mwingi analala tu au anakaa na uwepo wa saratani katika kipindi cha ujauzito hasa saratani ya shingo ya kizazi.
Sababu hatarishi zinazosababisha ugonjwa wa preeclampsia unaoambatana na kupanda kwa shinikizo la damu na uwepo wa protini kwenye mkojo ni kuwa na shinikizo la damu la muda mrefu hata kabla ya kuwa mjamzito, endapo kwenye familia ya mwanamke kuna historia ya kuwepo kwa ugonjwa huu.
Tatizo pia huwapata wasichana wanaopata ujauzito katika umri mdogo, yaani chini ya miaka kumi na saba na wanawake wanaobeba mimba katika umri zaidi ya miaka thelathini na mitano, hutokea pia kwa wanawake wengi wenye ujauzito wa mapacha, wenye ugonjwa wa kisukari, wenye magonjwa ya mishipa ya damu na matatizo mengine yahusuyo ujauzito.

DALILI ZA UGONJWA
Dalili hutegemea na chanzo cha tatizo, kwa wenye tatizo la preeclampsia hupata kichefuchefu na kutapika, kuumwa na tumbo na manjano machoni na kwenye ulimi hadi vidoleni. Kwa wenye DVT hupata maumivu ya miguu iliyovimba, joto miguuni na kutokwa na vidonda.
Uvimbe pia husababisha mapafu yaweze kujaa maji na kumfanya mgonjwa ashindwe kupumua vizuri hasa katika tatizo linaloambatana na shinikizo la damu kuwa juu. Shinikizo la damu likiwa juu na protini kwenye mkojo ikizidi, mgonjwa huhisi kuchanganyikiwa, kuumwa kichwa, macho kutokuona vizuri na kutikisika mwili kama mgonjwa wa kifafa.
Hivyo tayari tunasema mama amepata kifafa cha mimba. Mguu pia unaweza kuvimba mmoja au yote miwili katika tatizo hili la DVT, mguu unaweza kuuma na vidonda kutoka hali ikiambatana na homa au la.

MATIBABU NA USHAURI
Tiba inatakiwa itolewe kwa kuzingatia chanzo cha ugonjwa, mgonjwa atachunguzwa vyanzo vinavyohusisha DVT na preeclampsia . Uchunguzi utafanyika katika hospitali ya mkoa. Wahi hospitali kwa uchunguzi na tiba.
DK. CHALE | IJUMAA | AFYA
 
Tupia Comment Yako, Matusi Hapana

Comments

Popular posts from this blog