Tamasha la Dar Bodaboda Superstar Lafanyika
MAKAMPUNI ya JP Decaux pamoja na International Republican Institute (IRI) zilizokuwa zimeandaa Tamasha la Waendesha Pikipiki leo limefanyika katika Viwanja vya Tanganyika Parkers Jijini Dar es Salaam.
Kati ya washiriki wa tamasha hilo la bodaboda mmoja alijinyakulia pikipiki baada ya kuwashinda washiriki wengine kutokana na vigezo vya mashindano hayo kuvikidhi.
Akizungumza na mtandao huu, Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya JP Decaux, Shaban Makugaya alisema kuwa lengo la tamasha hilo lilikuwa ni kuweka uamsho, msisitizo na kuendelea kutoa elimu ya usalama barabarani kwa madereva wa pikipiki na abiria kwa madhumuni la kuzingatia sheria za usalama kwa matumizi ya barabara pamoja na kudumisha umoja, ushirikiano na mshikamano katika jamii.
Makugaya amesema kuwa, tamasha hilo ni la kwanza kufanyika nchini na kampuni hiyo imejipanga kulifanya kila mwaka nchi nzima ambapo jina la maonesho litabadilika kulingana na mji au mkoa ambao tamasha litafanyika.
Aliongeza kuwa usafiri wa pikipiki umekua njia rahisi za kumuwezesha msafiri kufika haraka hivyo mashirika hayo yameamua kuwakutanisha madereva hao na kuwapa elimu ya usalama barabarani ili waweze kuepuka ajali za barabarani zinazosababisha vifo vya Watanzania wengi.
Akifafanua zaidi, mkurugenzi huyo amesema kuwa waendesha bodaboda walioshiriki katika tamasha hilo walionyesha leseni zao na walitoka katika vikundi vyao vilivyosajiliwa na kutambulika kisheria.
Tamasha hilo pia lilihusisha michezo mbalimbali ikiwemo ya soka ambayo ilikuwa ya utangulizi kati ya timu ya Trafiki na Waendesha Pikipiki, burudani ya mziki wa kizazi kipya, taarabu na singeli pia zilikuwepo ili kuboresha tamasha hilo. Aidha zilitolewa zawadi za jezi na mipira kwa timu ya Trafiki iliyoshinda.
Comments
Post a Comment