SERENGETI BOYS MGUU NDANI KOMBE LA DUNIA,YAIBUTUA ANGOLA AFCON U-17 NCHINI GABON
Timu ya
vijana chini ya miaka 17 ya Tanzania ‘Serengeti Boys’ imefanikiwa kupata
ushindi wa kwanza kwenye michuano ya AFCON U17 baada ya kuifunga Angola
kwa mabao 2-1 kwenye mchezo wa Kundi B uliochezwa Uwanja wa L’Amittee
mjini Libreville,nchini Gabon.
Vijana wa
Serengeti Boys ndio walikua wa kwanza kupata bao la kuongoza dakika ya
sita kipindi cha kwanza baada ya Kelvin Naftal kupasia kamba kwa kichwa
akiunganisha krosi ya Nickson Kibabage.
Dakika ya
18 Angola walisawazisha bao hilo kupitia kwa Pedro baada ya kutumia
vizuri makosa ya safu ya ulinzi ya Serengeti Boys na kufanya timu zote
kwenda mapumziko zikiwa sare kwa kufungana 1-1.Kipindi cha pili
Serengeti waliongeza kasi kutafuta bao na kufanikiwa kufunga dakika ya
69 mfungaji akiwa ni Abdul Suleiman baada ya kazi nzuri iliyofanywa na
Yohana Mkomola.
Serengeti
Boys imefikisha pointi 4 baada ya kupata pointi moja kwenye mchezo wa
kwanza kufuatia kutoka sare ya bila kufungana dhidi ya Mali ambao ndio
mabingwa watetezi.
Pointi
hizo zinaifanya Serengeti kuwa kwenye mazingira mazuri ya kufuzu hatua
ya nusu fainali ya michuano hiyo kwani watahitaji ushindi au sare dhidi
ya Niger kwenye mchezo wa mwisho wa kundi B.Endapo Serengeti Boys
itafuzu kucheza nusu fainali ya AFCON U17 itakua imefuzu pia kucheza
fainali za kombe la dunia kwa vijana wa U17 zitakazofanyika nchini India
baadae mwaka huu.
Comments
Post a Comment