Mwanaye Madega Aua, Naye Auawa Ajalini

Aliyekuwa Makamu Mwenyekiti wa TFF, Iman Omary Madega.
MWANDISHI WETU | CHAMPIONI |HABARI
MWENYEKITI wa zamani wa Yanga, Imani Madega amepata msiba mkubwa baada ya mwanaye, Omary Madega kupata ajali iliyosababisha kifo na baadaye kuuawa kwenye ajali nyingine. Omary anayekadiriwa kuwa na umri wa miaka 32, aliuawa wakati akiwakimbia madereva wa bodaboda katika eneo la Chalinze mkoani Pwani akiwa anatumia gari la baba yake mdogo, Madega ambaye kitaalamu ni mwanasheria.
Akizungumza na Championi Jumatano, Madega aliyeonyesha masikitiko makubwa alisema gari lililosababisha ajali ni Mitsubishi Pajero, mali yake.
“Nina msiba mkubwa sana ndugu yangu. Nilisafiri kutoka Dar es Salaam hadi Chalinze ambako nilipitiliza kwenye project yangu. Nikiwa huko gari lilisumbua.  “Nikamuita Omary ambaye ni mtoto wa kaka yangu aje alishughulikie. Alipofika pale alikuwa na fundi, akamchukua na mtu ambaye amekuwa akisimamia nyumba yangu ninapokuwa Dar es Salaam pamoja na msimamizi wa mifugo yangu. “Wote wanne waliondoka kwenda kuifuata gari nilipoiacha. Walipofika haikuwa na tatizo kubwa, kawaida ikishapoa huwa inawaka, basi wakaichukua. Sasa si unajua vijana, wakaona waingie mtaani kidogo.
“Kama dakika 10 tokea waondoke, nikapigiwa simu kwamba Omary kagonga
watu watatu pale sheli na inasemekana mmoja amepoteza maisha na alikuwa anabishana na madereva bodaboda. Mwisho aliondoa gari kwa kasi kama akielekea Dar es Salaam. “Dakika tano baadaye sijajua hata cha kufanya, nikapigiwa simu kuwa ile gari imepata ajali na Omary amefariki dunia pamoja na yule fundi na mtunza nyumba,” alisema Madega. Kwa mujibu wa Madega, Omary alizikwa Jumapili, mtunza nyumba wake kazikwa juzi na msimamizi wa mifugo yake bado ana hali mbaya katika Hospitali ya Tumbi Kibaha kwa kuwa mguu wake umevunjika vibaya na unahitaji upasuaji, huku ndugu wa fundi wakiwa katika mipango ya kuchukua mwili wa marehemu.

Comments

Popular posts from this blog