Mwanafunzi Kukishitaki Chuo Kikuu cha UDSM
Mwanafunzi huyo aliyekuwa akisoma shahada ya kwanza ya sheria alifukuzwa baada ya kufutiwa usajili Januari 26, pamoja na mambo mengine akidaiwa kusajiliwa kwa makosa kwasababu aliwahi kufukuzwa chuoni hapo.
Lusako anayewakilishwa na Wakili Jebra Kambole anaiomba Mahakama impe kibali cha kuishtaki UDSM na itoe amri ya kuzuia uamuzi wa kumfutia usajili. Maombi hayo yamepangwa kusikilizwa Mei 23 na Jaji Pellagia Khaday.
Lusako alijiunga na UDSM kwa mara ya kwanza mwaka 2009 akiwa amedahiliwa kusoma Shahada ya Biashara katika Uhasibu.
Hii ni mara ya pili kwa Lusako kufukuzwa chuoni hapo, mara ya kwanza ni Desemba 13, 2011, pamoja na wenzake kadhaa, akiwa mwaka wa tatu walifukuzwa na kufutwa katika mfumo wa elimu nchini wakidaiwa kuratibu mgomo wa wanafunzi UDSM.
Hata hivyo, anadaiwa alikuwa akipinga ufisadi katika Tume ya Vyuo Vikuu (TCU) kwa kusajili wanafunzi hewa na katika Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB).
Baada ya kukaa uraiani kwa muda mrefu, aliamua kuomba usajili, TCU ilimsajili na kumpanga UDSM kusoma kozi ya sheria.
Baada ya kusoma muhula mmoja, alipewa barua ya kufutiwa usajili ikieleza alisajiliwa kimakosa chuoni hapo kwa kuwa tayari alishawahi kufutiwa usajili.
Comments
Post a Comment