Malima aachiwa kwa dhamana ya mil 5



Aliyekuwa Naibu Waziri Wizara ya Fedha, Mhe Adam Malima ameachiwa leo kwa dhamana ya shilingi milion 5 katika Mahakama ya Hakimu mkazi Kisutu akikabiliwa na shtaka la shambulio.

Malima ambaye aliwahi kuwa mbunge wa Mkuranga amedaiwa kumzuia Ofisa huyo kufanya kazi yake ya kumkamata Ramadhani Kigwande kwa kosa la kumshambulia Mwita Joseph.

Wakati akisoma mashtaka yaliyokuwa yakimkabili Mhe Malima, Wakili wa Serikali, Mwanaamina Kombakono alidai kuwa Mei 15,2017 katika eneo la Masaki kwa makusudi Malima alimzuia Ofisa wa polisi H.7818 PC ABDU kufanya kazi yake halali.

Wakili Kombakono aliendelea kudai kuwa mshtakiwa huyo akiwa na nia ya kumzuia Mwita Joseph ambaye ni Ofisa oparesheni wa kampuni ya Priscane Business Enterprises  wakati alipokuwa akimkamata kwa kupaki vibaya gari namba T 587 DDL alimshambulia(Mwita) na kumsababishia maumivu.

Kwa upande wa mshtakiwa wa kwanza, Ramadhani Mohammed Kigwande (Dereva wa Malima) naye anakabiliwa na shtaka la kumshambulia Mwita Joseph.

Hata hivyo baada ya kusomewa mashtaka hayo,washtakiwa wote waliyakana na upande wa mashtaka ulidai kuwa upelelezi bado haujakamilika.

Washtakiwa hao wawili  wanatetewa na wakili Peter Kibatala ambaye amewasilisha pingamizi dhidi ya shtaka la pili kuwa shtaka halifanani na maelezo ya kosa.

Hakimu Mkazi, Respicius Mwijage ameiahirisha kesi hiyo namba 168 ya 2017 hadi Juni 15,2017 kwa ajili ya kutajwa ambapo pia pingamizi hilo litasikilizwa, huku washtakiwa wakiwa wameachiwa huru kwa masharti ya dhamana ya kusaini bondi ya shilingi milioni 5.

Comments

Popular posts from this blog