Kiama kingine cha Majina wenye vyeti feki J’tano
WAKATI watumishi wa umma 9,932 wakiwa wamebainika kuwa na vyeti feki
mpaka sasa, idadi hiyo inatarajiwa kuongezeka Jumatano ijayo, siku
ambayo Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi itatangaza majina zaidi.
Ijumaa iliyopita, serikali ilitangaza kukamilika kwa zoezi la uhakiki wa
vyeti vya kuhitimu kidato cha nne, sita na ualimu kwa watumishi wa
Sekretarieti za Mikoa, Tawala za Mikoa, Wakala wa Serikali, Taasisi za
umma na Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa umma.
Akizungumza na waandishi wa habari jana, Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais,
Menejimenti ya Utumishi wa Umma, Dk. Laurean Ndumbaro, alisema uhakiki
wa vyeti unaendelea kwa watumishi wa wizara zilizosalia na taasisi
mbalimbali.
Alisema uhakiki huo wa awamu ya pili na ambao utafuatiwa na awamu ya tatu, unatarajiwa kukamilika Jumatano.
Alisema baada ya matokeo ya uhakiki huo kuwekwa hadharani, uamuzi wa serikali utatolewa.
“Maamuzi ya watumishi 9,932 waliobainika kuwa na vyeti vya kugushi
ilikuwa ni kuondolewa kwenye orodha ya malipo ya mishahara mara moja, na
waendelee kuondolewa ili mwisho wa mwezi Mei wasipate mishahara yao,”
alisema Dk. Ndumbaro.
Alisema watumishi hao wanaachishwa kazi kulingana na taratibu, sheria na kanuni za utumishi wa umma.
Ndumbaro alisema watumishi 1,538 wenye vyeti vyenye utata vinavyotumiwa
na watumishi wawili, watatu au zaidi wanatakiwa kuhakiki umiliki wa
vyeti vyao Baraza la Mitihani (Necta) kabla ya Mei 15.
Aidha alisema wakati watumishi hao wakiendelea kuhakiki vyeti vyao,
mishahara yao itasimamishwa hadi zoezi litakapokamilika na kwa
atakayethibitika ni mmiliki halali wa cheti atapewa mshahara wake.
Aidha, Dk. Ndumbaro alisema watumishi 11,596 ambao waliwasilisha vyeti
pungufu pamoja na wale ambao hawajawasilisha vyeti vyao kabisa
wanatakiwa kufanya hivyo kabla ya Mei 15 pia kwa ajili ya uhakiki na
ambaye hatawasilisha hatua za kinidhamu zitachukuliwa.
VYETI HALALI
Katibu Mkuu huyo alisema mara baada ya taarifa ya Ijumaa kutolewa mbele
ya Rais John Magufuli hapa Dodoma, walijitokeza watumishi wakieleza kuwa
wanavyo vyeti au walivyo navyo ni halali.
“Watumishi wanaodai kuwa na vyeti halali wanaruhusiwa kukata rufani kwa utaratibu," alisema.
"Waandike barua kwa Katibu Mkuu Utumishi kukata rufani hiyo; barua
ambayo inapitia kwa waajiri wao wakieleza uthibitisho wao wa umiliki wa
vyeti ambavyo ni halali.
“Pamoja na kuandika rufani hizo, waajiri wao watatakiwa kuwasilisha
vyeti au nakala ya vyeti vya kidato cha nne na sita Necta kwa njia ya
mtandao ili uhakiki uende haraka.”
Aliwataka waajiri watakapopata nakala ya vyeti ambavyo wanadai ni halali
watume nakala laini (scan) kwa barua pepe ya Necta ambayo ni
esnecta@necta.go.tz au pshea@necta.go.tz ili viweze kuhakikiwa upya na
pia nakala hiyo itumwe kwa Katibu Mkuu Utumishi kwa barua pepe ya
ps@utumishi.go.tz na inatakiwa kukamilika kabla ya Mei 15 pia.
Alisema malalamiko mawili yalikuwa yamepokelewa mpaka jana kutoka kwa watumishi waliodai kuwa na vyeti halali.
“Hawa waliwasilisha vyeti au nakala ya vyeti kwa waajiri wao tofauti na
vile wanavyoviwasilisha," alisema. "Sasa na hawa ni wale watumishi ambao
walibadili alama za ufaulu kwenye cheti yaani mtu alipata daraja la nne
lakini amebadilisha na kutumia cha daraja la tatu.”
Alifafanua katika kundi hilo, cheti ni hicho hicho chenye jina na namba
hiyo hiyo lakini siku zote mtumishi alikuwa akitumia cheti chenye ufaulu
wa daraja la tatu lakini alichowasilisha kina daraja la nne na ambacho
ndiyo halali.
“Kwa hiyo wakifika Necta wakiangalia cheti cha daraja la nne ni sahihi
lakini siku zote alikuwa hatumii, alikuwa anatumia cha kugushi chenye
daraja la tatu na ndio kilimuwezesha akasome hiyo taaluma," alisema.
"Bado watumishi wa namna hii vyeti vyao ni feki.”
Alisema wale wenye vyeti halali wakate rufani na hakuna mtumishi ambaye ana cheti halali ataondolewa.
“Wale wenye vyeti halali ikithibitika watarudishwa kwenye utumishi wa umma, wasio na vyeti halali wataondolewa.”
Comments
Post a Comment