Kauli ya Rais Mstaafu Mkapa Kuhusu Serikali Kubana Uhuru wa Habari
Rais Mstaafu wa awamu ya tatu, Mzee Benjamin Mkapa amevikosoa
vyombo vya habari barani Afrika na haswa kusini mwa Jangwa la Sahari kwa
kile alichosema vingi vimejikita katika kuripoti habari za kisiasa na
matukio ya nani kafanya nini au kawa nani, badala ya kuripoti habari za
uchumi za kuwasaidia wananchi.
Mzee Mkapa aliyasema hayo alipokuwa akifanya mahijiano na na Idhaa
ya Kiswahili ya Deutsche Welle (DW) ya nchini Ujerumani ambapo alisema
kwenye vyombo vya habari vya Afrika kuna upungufu mkubwa wa wa habari za
uchumi na maendeleo zilizofanyiwa utafiti wa kina.
“Tatizo moja kubwa la vyombo
vya habari vya nchi za Afrika hasa hasa Kusini mwa Jangwa la Sahara ni
kwamba habari nyingi zinazopewa kipaumbele ni zile za kisiasa na
zinazohusu nani ni nani na kafanya nini.”
“Kuna upungufu mkubwa wa
habari za kiuchumi na maendeleo zilizofanyiwa utafiti wa kina na
zinazochochea maendeleo. Kuna habari kidogo sana za utetezi wa
kimaendeleo na kujipanga ili tupige hatua.”
Kufuatia hali hiyo, Mzee Mkapa alisema kuwa uhuru wa vyombo vya
habari unaodaiwa kuwa umebanwa, unahusu vyombo vya habari ambavyo havina
mchango kwenye maendeleo ya uchumi wetu zaidi ya kuzungumzia matokeo
badala ya uchambuzi.
“Kwa hiyo, huo uhuru wa vyombo
vya habari unaosema unabanwa unahusu kundi la vyombo vya habari ambavyo
havina mchango wowote katika uchambuzi wa masuala ya uchumi utetezi wa
maendeleo wala kwenye kujipanga kujitafutia maendeleo. Nasi ni taifa
masikini linalohitaji kuendelea. Nadhani ni uamuzi sahihi.” alisema Mzee Mkapa.
Kauli hii ya Mzee Mkapa ilikuja baada ya kuulizwa kuhusu madai ya
kuwa serikali ya awamu ya tano chini ya Rais Dkt John Pombe Magufuli
inabana uhuru wa vyombo vya habari hali ambayo haikuwapo miaka ya nyuma.
Comments
Post a Comment