JB RAY NA RICH WAFUNGUKA MAZITO KUHUSU TUHUMA ZA KUHONGWA VIWANJA NA PESA
Baada ya
kuwepo kwa madai kuwa mastaa wa filamu Bongo, Jacob Steven (JB), Single
Mtambalike (Rich) na Vincent Kigosi (Ray) walihongwa fedha na viwanja
ili ‘kuinjinia’ maandamano ya hivi karibuni kupinga sinema za nje,
mastaa hao wamebanwa na hatimaye kufungukia ishu hiyo inayowatafuna,
Risasi Mchanganyiko lina mkanda kamili.
Chanzo
kilicho karibu na tasnia hiyo kililiambia Risasi Mchanganyiko kuwa
kampuni moja ya usambazaji filamu (jina kapuni kwa sasa), iliwapa fedha
baadhi ya waigizaji ili wafanye maandamano ya kuziondoa sokoni filamu
hizo za nje, zinazodaiwa kukingiwa kifua na Rais wa Shirikisho la Filamu
Tanzania, Simon Mwakifwamba.
Inadaiwa
kuwa baada ya kampuni hiyo ya usambazaji ‘kupenyeza sumu hiyo’ waigizaji
hao walikwenda kwa kigogo mmoja wa kisiasa na kumshawishi kuwaunga
mkono, ambaye naye alikubali na kuwaomba waigizaji hao kufanya kila
wawezalo, kumtoa kwenye kiti chake, Simon Mwakifwamba, kwani ana ukaribu
na hasimu wake wa siasa.
“Kuna
watu wamevuta huku na huku katika hii ishu, wale wasambazaji hawazitaki
kabisa filamu za ndani kwa sababu zinaharibu soko lao, ingawa wana
kisingizio cha kodi, hawana lolote, watu hawataki sinema za Bongo kwa
sababu hazina ubora,” kilisema chanzo hicho.
Kiliendelea
kudai kuwa katika kuhakikisha lengo hilo linafanikiwa, kigogo huyo wa
kisiasa anadaiwa kutoa hongo ya viwanja kwa mastaa hao, ambavyo
vinadaiwa viko Kigamboni jijini Dar.
Ili kuujua ukweli juu ya tuhuma hizo, Risasi Mchanganyiko liliwatafuta waliotajwa na kuwabana ili wafungukie ishi hiyo.
Ray
alipoulizwa alijibu akisema; “Hiyo ishu ya kupewa viwanja hainiingii
akilini, kwanza ili iweje, mimi nilienda kwenye maandamano maana ni ishu
iliyokuwa inanihusu kama msanii wa filamu, huyo Mwakifwamba ambaye
anapinga suala hilo atakuwa ana mambo yake ya kisiasa, kwanza yeye mara
ya mwisho kutoa filamu sijui ni lini.
“Sisi
tunapigania haki yetu maana filamu za nje hazitozwi kodi, ndiyo maana
zinauzwa bei rahisi kitu ambacho kinaathiri soko la filamu zetu nzuri na
zenye ubora tunazozitengeneza.”
Kwa
upande wa JB alipoulizwa kuhusiana na hilo alijibu; “Ili iweje? Kwani
(anamtaja kigogo huyo) anapata wapi viwanja? Uongo huo wa kijinga. Mimi
nilienda pale kushiriki maandamano kwa sababu ni mdau, si vinginevyo.
“Hebu
fikiria, hivi unaona tofauti za bei za bia? Bia za nje na ndani ziko
sawasawa? Zinatofautiana kwa sababu ya kodi na ili kulinda viwanda vya
ndani,” alisema muigizaji huyo maarufu.
Kwa
upande wa Rich, naye kama walivyo wenzake, alisema madai ya kupewa hongo
ya viwanja na fedha ni ya uongo, kwani yeye alianza kushiriki kampeni
za kukamata filamu za nje tangu enzi zile Nape Nnauye akiwa Waziri wa
Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo.
“Kwanza
mimi siyo timu (kigogo), nilienda pale kama mdau na wala sikwenda pale
kupinga kazi za nje, nilienda pale kutaka filamu zote zilipe kodi.
Tatizo la filamu zetu siyo zile za nje, bali ni ubovu wa kazi zetu.
“Kama
tutatengeneza kazi nzuri zitauzika tu sokoni, lakini kama kila mtu
mwenye fedha anadhani anaweza kutengeneza filamu, hiyo ndiyo inayoharibu
soko letu. Ninakubali kuna udhaifu katika filamu za ndani, ambazo
nadhani ndiyo zinachangia kuua soko, si filamu za nje,” alisema.
Comments
Post a Comment