Jambazi Sugu Mwanamke Auawa


NAIROBI: Mwanamke anayedaiwa kuwa jambazi sugu, Claire Mwaniki ambaye amekuwa akipakia mtandaoni picha zake akiwa amejipodoa na kujipamba, ameuawa na polisi katika Mtaa wa Kayole jijini Nairobi, Jumatano alfajiri.
Gazeti la Daily Nation limeeleza mwanamke huyo alikuwa na majambazi wengine wanne wa kiume wakati walipofumaniwa na polisi wakitekeleza tukio la kupora kwa kutumia sialaha (ujambazi) katika eneo la Lower Chokaa, Mtaa wa Kayole.
Mwanamke huyo anadaiwa kuwafyatulia risasi maofisa wa polisi akiwa na jambazi mwingine lakini polisi walipambana nao hadi kuwaua majambazi wawili akiwemo Claire Mwaniki huku wenzao wakifanikiwa kutoroka.
Taarifa za Gazeti la Daily Nation inasema polisi waliwaandama baada ya kupokea taarifa kutoka kwa wenzao kupitia mtandao wa WhatsApp kwamba majambazi hao walikuwa wamekwepa mtego waliokuwa wamewekewa ambapo polisi walijiandaa na kisha wakawakabili katika Mtaa wa Lower Chokaa.

Mkuu wa Polisi wa Mtaa wa Kayole, Joseph Gichangi amenukuliwa na Daily Nation akisema: “Kwa mujibu wa vyanzo vyetu, mwanamke huyo alikuwa mke wa mshukiwa wa ujambazi ambaye anafahamika vyema, ambaye bado anasakwa na polisi.”
Alisema visa vya wanawake kujihusisha na magenge yanayotekeleza wizi wa kutumia mabavu vinaongezeka.
Wakenya mtandaoni wamekuwa wakisambaza picha za Mwaniki na kumjadili sana mtandaoni ambapo katika mtandao wa Facebook, mwanamke huyo amekuwa akijitambulisha kama mwanafunzi wa zamani wa Chuo Kikuu cha Nairobi na mtu anayependa kufurahia maisha.
Kuna wakati alipakia picha yake, ya mwanamume na mtoto, na kuongeza kwamba hiyo ni “familia”. Mkuu wa Polisi Nairobi, Japheth Koome anasema magenge mengi ya wahalifu huwa na wanawake.
“Wanawake hutumiwa kusafirisha silaha, kukusanya habari na hata kushiriki katika ujambazi,” Bw Koome alisema. Aliongeza kuwa wakati mwingine hutumiwa na majambazi wa kiume kuwapelekea chakula mafichoni.

Comments

Popular posts from this blog