Hiki ni kizaazaa kingine fao la kujitoa

NI kizazaa kingine! Baraza la Uongozi la Chama cha Mawakili wa Tanganyika(TLS), limeazimia kushirikiana na wadau kwenda mahakamani kuhoji kuhusu utata juu ya fao la kujitoa uanachama wa mifuko ya hifadhi ya jamii.

Hivi karibuni wakati serikali ikiwa katika maandalizi ya kuliondoa fao hilo, kulizuka taharuki kwa baadhi ya wafanyakazi walio wanachama wa mifuko hiyo.
Ilielezwa kuwa fao la kujitoa likiondolewa litaletwa fao la kutokuwa na ajira.

Katika mapendekezo hayo mapya, inaelezwa kuwa mfanyakazi ambaye amechangia zaidi ya miezi 18, atalipwa asilimia 30 ya mshahara wake wa mwisho baada ya kupoteza ajira.

Mbali na hilo, pia atalipwa kwa miezi sita mfululizo, kisha malipo hayo yatasitishwa. Anayestahili malipo hayo ni yule ambaye hakuacha kazi kwa hiari yake (resignation).

Inaelezwa katika mapendekezo hayo ya awali kuwa baada ya miaka mitatu tangu kusitishwa kwa fao la kujitoa, mfanyakazi atakayekuwa hajapata ajira ataruhusiwa kuhamisha michango yake kutoka kwenye mfuko wa lazima (Compulsory Scheme), kwenda mfuko wa hiari (Supplementary Scheme).

Kutokana na mabadiliko hayo, mfanyakazi atakuwa na hiari kuchukua fedha zake kulingana na mfuko wa hiari aliojiunga nao na pia atakuwa na haki ya kuendelea kuchangia.

“Na kwa mfanyakazi aliyeachishwa kazi akiwa amechangia chini ya miezi 18, atakuwa na haki ya kuchukua asilimia 50 ya michango yake mara baada ya ajira kukoma,” ilieleza sehemu hiyo ya mapendekezo ya sheria hiyo.

Mapendekezo hayo ndiyo yanayolekea kuzua kizaazaa kingine mahakamani kutokana na maazimio ya TLS.

Akitangaza maazimo ya kikao cha baraza hilo, Rais wa TLS Tundu Lissu alisema wameamua kwenda mahakamani kwa ajili ya suala hilo na pia masuala mengine kadha wanayoona kuwa hayako sawa.

“Tumeamua jana(juzi) ili twende mahakamani kwenye haya masuala jambo la kwanza ni lazima TLS iteue jopo la mawakili watakaopeleka hili suala mahakamani na pia watakaoendesha hizi kesi,”

Alisema watakapoliteua jopo hilo, TLS itakuwa ni mshitaki na mdai.

"TLS ndio itakuwa mshtaki na mdai hivyo hatutatafuta mtu huko mitaani, Chama cha Mawakili kina mamlaka ya kushtaki na kinaweza kushtakiwa kama ambavyo kilikuwa ‘Comprender’ kama tulivyofanya kwenye kesi ya Takrima ya miaka ile, tutakwenda mahakamani tutakapokuwa tayari,” aliongeza Lissu.

Aidha alisema pamoja na fao la kujitoa pia watahoji mambo mengine ambayo yanaathiri ustawi wa jamii, ikiwa ni pamoja na masuala ya makato ya madeni ya wafanyakazi kwa Bodi ya Mikopo ya Elimu ya juu; kukaimiwa kwa nafasi ya Jaji Mkuu na pia suala la katiba mpya.

KAIMU JAJI MKUU
Akizungumzia kuhusu nafasi ya Kaimu Jaji Mkuu, Lissu alisema TLS itahakikisha utawala wa sheria unalindwa nchini na wenye mamlaka ya umma wanafuata na kuheshimu sheria za nchi.

Alisema Baraza hilo limeazimia kufungua mashauri katika Mahakama Kuu ya Tanzania kuhoji uhalali Kikatiba wa Rais kushindwa hadi sasa kuteua Kiongozi Mkuu wa Mahakama, yaani Jaji Mkuu.

Alisema dhamira ya kwenda mahakamani ni kupata tafsiri ya kisheria juu ya ukomo wa nafasi ya Kaimu Jaji mkuu kwa kuwa wanaamini ibara ya 118(4) haikutungwa kwa lengo la kumwezesha Rais kuteua Kaimu Jaji Mkuu bila kikomo cha muda.

“Serikali imetamka bungeni kwamba mamlaka ya Kaimu Jaji Mkuu hayana kikomo cha muda, kwa sababu hiyo suala hili sasa linahitaji tafsiri ya vifungu vya Katiba na Mahakama kuu ndiyo yenye mamlaka ya kutoa tafsiri hiyo,” alisema Lissu.

Alifafanua kuwa mhimili huo kutokuwa na kiongozi kwa miezi mitano baada ya kustaafu Jaji Mkuu Othman Chande kunatoa taswira kuwa ina hadhi hafifu ukilinganisha na mihimili mingine kama Bunge na serikali.

Alisema TLS itateua jopo la mawakili wenye uzoefu na ujuzi mkubwa wa kesi za Kikatiba ili kutekeleza uamuzi huo kwa kuwa masuala mbalimbali ya mhimili huo kwa sasa yamekwama kutokana na Kaimu Jaji Profesa Ibrahim Juma kushindwa kuongoza vikao vya Tume ya Kimahakama kwa kukosa sifa.

Kuhusu mchakato wa Katiba Mpya, Lissu alisema limeazimia kuandaa Kongamano la Kitaifa juu ya mchakato wa Katiba Mpya ili kujadili hatma ya mchakato huo.

Aliongeza kuwa TLS itashughulikia pia tatizo sugu la migogoro kati ya wakulima na wafugaji na ukiukaji mkubwa wa haki za wafugaji katika maeneo mengi nchini

Comments

Popular posts from this blog