FAHAMU UKWELI JUU YA VITA VYA KARANSEBES AMBAVYO ZAIDI YA WANAJESHI 10000 WALIUANA
Unaweza
kudhani ni hadithi ya kutunga lakini hii kweli ilitokea! Vita ya
Karansebes, ni miongoni mwa matukio yaliyoushangaza sana ulimwengu baada
ya wanajeshi wa jeshi moja la Austria, kushambuliana wenyewe kwa
wenyewe na kusababisha wanajeshi zaidi ya 10,000 kupoteza maisha.
Ilikuwaje?
Usiku wa Septemba 17, 1788, wanajeshi zaidi ya 100,000 wa Jeshi la
Austria lililokuwa linaundwa na makabila mbalimbali, walikuwa wameweka
kambi katika Mji wa Karansebes (Romania ya sasa) wakijiandaa kuvamia
Himaya ya Ottoman (Uturuki ya sasa).
Ili
kurahisisha uvamizi, wanajeshi waligawana katika makundi, wengine
wakaenda upande mmoja na wengine upande mwingine. Wakati wakijiandaa
kufanya shambulio, kukatokea kutoelewana kati yao, wakaanza
kushambuliana wenyewe kwa wenyewe kimakosa wakidhani wanawapiga
wanajeshi wa Ottoman.
CHANZO CHAKE KINASHANGAZA
Inaelezwa
kuwa kundi moja kati ya yale mawili, lilivuka Mto Timis na kuingia Mji
wa Hussar uliokuwa ngome ya wanajeshi washirika, Wahussar waliokuwa
wakisaidiana kuwapiga Waturuki. Baada ya kuingia, wanajeshi wa Austria
waliomba hifadhi kwa wenyeji wao ambao waliwakarimu kwa pombe na chakula
wakati maandalizi ya vita yakiendelea.
Hata
hivyo, kutokana na wingi wa wanajeshi hao, pombe iliisha wakati
wanajeshi wakiwa bado wanaihitaji, wakaanza kuwashinikiza wenyeji wao
wawaongeze, jambo lililosababisha kutokea kwa hali ya kutoelewana na
kurushiana maneno. Mmoja kati ya wanajeshi wa Austria, ambaye tayari
alishaanza kulewa, kwa hasira alifyatua risasi juu akishinikiza
waongezwe pombe.
Mlio wa
risasi ulisababisha taharuki kubwa eneo hilo, wenyeji wakahisi
wamevamiwa na wanajeshi wa Ottoman (Waturuki), wakawa wanakimbia huku na
kule wakitamka neno ‘Turci! Turci!’ (Waturuki! Waturuki).
Mkanyagano
ulipozidi kuwa mkubwa, ilibidi viongozi wa jeshi la Austria waingilie
kati na kuanza kuwatuliza wanajeshi wao ambao nao walishachanganyikiwa
wakidhani kweli wamevamiwa na Waturuki! Viongozi hao wakawa wanatumia
neno Halt! Halt! Ambalo kijeshi hutumika kuwaamuru wanajeshi kuacha kila
wanachokifanya na kutulia mara moja.
Kwa kuwa
kabila la wenyeji, Wahussar hawakuwa wakijua Kiingereza wala Kijerumani,
waliposikia neno hilo walilifananisha na ‘Allah! Allah!’ ambalo
lilikuwa likitumiwa na wanajeshi wa Uturuki wanapokuwa vitani.
Wakaamini
walikuwa wamevamiwa na Waturuki, wakaanza kuwashambulia, mapigano
makali yakatokea kati yao. Kundi la pili lililokuwa upande wa pili wa
mto, liliposikia mapigano yamekolea, nalo lilivuka mto na kwenda uwanja
wa vita. Kwa kuwa tayari giza lilikuwa limeingia, wakaanza kuwashambulia
wenzao ambao nao walijibu mapigo, vita ikazidi kupamba moto, kila mmoja
akiamini anapigana na Waturuki.
Mpaka
kunapambazuka, wanajeshi 10,000 walikuwa wamekufa huku wengine wengi
wakiwa wamejeruhiwa. Kila mmoja aliyepona akawa anashangaa iweje katika
wote waliokufa, wawe ni wa upande mmoja wa wanajeshi wa Austria na
washirika wao wa Hussar, hapo ndipo ukweli ulipofahamika kwamba kumbe
walikuwa wakipigana wenyewe kwa wenyewe.
Waturuki
waliposikia taarifa hizo, walifika haraka eneo hilo na kufanikiwa
kuuteka mji wa Hussar na mingine hivyo kushinda vita hiyo kiulaini.
Comments
Post a Comment