EVERTON KUCHEZA NA SIMBA AU YANGA,JULAI 13 UWANJA WA TAIFA JIJINI DAR ES SALAAM
Timu ya
Everton ya England yenye wachezaji nyota akiwemo Mbelgiji, Romelu
Lukaku, itazuru Tanzania kucheza mechi za kujiandaa na msimu mpya wa
2017/18, tovuti ya klabu hiyo imeandika.
Ziara
hiyo ambayo itakuwa sehemu ya sherehe zao za udhamini mpya wa kampuni ya
SportPesa, itaifikisha The Blues kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam
unaomeza mashabiki 60,000 kucheza mechi Alhamisi ya Julai 13. Everton
itakuwa timu ya kwanza ya Ligi Kuu ya England daima kucheza mechi ukanda
wa Afrika Mashariki – na itamenyana na bingwa wa mashindano ya
SportPesa Super Cup. Nchi mbili, Tanzania na Kenya zitakutanisha timu
zao nane, nne kutoka kila upande katika michuano hiyo, kuwania nafasi ya
kucheza na kikosi cha Ronald Koeman.
Mapema
mwezi huu, Everton ilitangaza udhamini mnono wa rekodi na SportPesa wa
miaka mitano na baada ya hapo kampuni hiyo ikaingia Afrika Mashariki
kufunga ndoa na klabu kadhaa kubwa, zikiwemo SImba na Yanga.
Michuano
ya SportPesa Super Cup inatarajiwa kuanza Juni 5 hadi 11 mjini Dar es
Salaam, ikishirikisha timu za Simba SC, Yanga SC, Singida United na
Jang’ombe Boys za Tanzania, Gor Mahia, AFC Leopards, Nakuru All Stars na
Tusker FC za Kenya.
Bingwa wa michuano hiyo itakayofanyika Uwanja wa Uhuru mjini Dar es Salaam ndiye atamenyana na Everton.
Comments
Post a Comment