Wabunge wapania kumbana Kassim Majaliwa


WABUNGE wa upinzani wamebainisha mambo manane ambayo wamepanga kumbana Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, atakapowasilisha makadirio ya bajeti ya ofisi yake kwa mwaka ujao wa fedha.

Kwa mujibu wa ratiba ya vikao vya Bunge iliyotolewa Jumatatu na Ofisi ya Katibu wa Bunge, kikao cha leo ambacho ni cha tatu tangu kuanza kwa mkutano wa saba wa Bunge la 11, Waziri Mkuu atawasilisha makadirio ya bajeti yake.

Wakizungumza na Nipashe nje ya Ukumbi wa Bunge jana, wabunge wa upinzani walibainisha mambo manane ambayo leo wangependa wapate ufafanuzi kutoka kwa Waziri Mkuu wakati wa mjadala wa bajeti yake.

Baadhi ya mambo hayo ni uchunguzi wa miili ya watu iliyoopolewa kwenye Mto Ruvu ikiwa imefungwa ndani ya sandarusi mwishoni mwa mwaka jana, utekelezaji wa kutoa Sh. milioni 50 kila kijiji, kusuasua kwa utekelezaji wa bajeti ya serikali kwa mwaka huu wa fedha, shughuli za serikali kuhamishiwa Dodoma na ukiukwaji wa haki za binadamu na misingi ya utawala bora.

KUFYEKWA BAJETI YA BUNGE
Mbunge wa Kigoma Mjini, Zitto Kabwe (ACT-Wazalendo) alisema atahakikisha anambana Waziri Mkuu ili bajeti ya Bunge iongezwe baada ya kuwa imefyekwa mwaka huu.

Zitto pia alisema atahoji kwa Waziri Mkuu mambo ya kikatiba kwa kuwa kiongozi huyo ndiye mratibu wa shughuli za serikali.

"Mambo ya kikatiba ambayo nitayaamsha ni kwa nini vyama vya siasa mpaka sasa haviruhusiwi kufanya mikutano ya wazi.

Kwa nini mpaka sasa hakuna taarifa kuhusu aliko Ben Saanane [Msaidizi wa Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Freeman Mbowe]. Haya ndiyo mambo ambayo lazima mimi nitayazungumza kama nitapata nafasi hiyo," alisema Zitto.

UCHUNGUZI MIILI MTO RUVU
Baadhi ya wabunge wa upinzani walisema watamuuliza Waziri Mkuu kuhusu maswali ya masuala ya utawala bora, utu na haki za binadamu.

"Uchumi wa nchi umeanguka, biashara zinafungwa na bajeti yenyewe imetekelezwa kwa chini ya asilimia 40. Arusha maendeleo tulipaswa kupewa Sh. bilioni 3.6, lakini mpaka sasa wameleta Sh. milioni 360 tu," alisema Godbless Lema, Mbunge wa Arusha Mjini (Chadema).

Aliongeza: "Tunakwenda kwenye bajeti nyingine wakati bajeti inayoisha hatujaikamilisha kwa kiwango kikubwa. Tunakwenda kumuuliza Waziri Mkuu utekelezaji wa bajeti na masuala ya utawala bora maana sasa kuna matamko ya ajabu majukwaani. Viongozi wanatunga sheria majukwaani na kuleta athari kubwa.

"Pia tutamuuliza Waziri Mkuu kuhusu utu na haki za binadamu. (Peter) Lijualikali (Mbunge wa Kilombero - Chadema)  alihukumiwa kifungo cha miezi sita jela, lakini Mahakama Kuu imeona hana hatia.

Mimi nimekaa gerezani lakini kilichotokea kila mtu anajua, nilikuwa na haki ya dhamana lakini nikanyimwa kwa hila."

Lema ambaye pia ni Waziri Kivuli wa Mambo ya Ndani ya Nchi, alisema  upinzani pia utahoji kwa Waziri Mkuu sababu za kutumia gharama kubwa kusaka ushahidi wa Faru John badala ya kuchunguza miili ya watu iliyoopolewa Mto Ruvu.

Naye Mbunge wa Kibamba, John Manyika (Chadema), alisema atahoji kwa Waziri Mkuu kuhusu changamoto ya watendaji wa serikali hususan wakuu wa mikoa na wilaya kutumia vibaya madaraka.

"Kuna tatizo kimejitokeza katika masuala ya utawala, wakuu wa wilaya na mikoa kutumia vibaya madaraka yao. Kitendo cha Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam kuvamia kituo cha habari hakiwezi kukwepeka kuuulizwa kwa Waziri Mkuu," alisema.

"Ingawa Tamisemi (Tawala za Mikoa na Tawala za Mikoa) imehamishiwa Ofisi ya Rais, lazima tutaanzia kwa Waziri Mkuu kujadili suala hili maana yeye ndiye msimamizi wa shughuli za serikali."

Mbunge wa Ukonga, Mwita Waitara, mbali na kusisitiza kuwa atahoji sababu za kusuasua kwa utekelezaji wa bajeti ya serikali, alisema atambana Waziri Mkuu aeleze waliokotoa fedha za kuhamishia serikali Dodoma wakati Bunge halikuidhinisha fungu kwa ajili ya suala hilo.

Mbunge huyo pia alisema watahoji kwa Waziri Mkuu sababu za serikali kushindwa kutekeleza ahadi yake ya kutoa Sh. milioni 50 za mkopo kwa kila kijiji/ mtaa ambazo kwa kuanzia, mwaka huu zilitengwa Sh. bilioni 59 kwa ajili ya kufanikisha suala hilo.
chanzo: Nipashe

Comments

Popular posts from this blog