VIONGOZI WA DINI WAJUMUIKA KUFANYA DUA MAALUM KUZIOMBEA MKURANGA NA KIBITI

Rufiji. Viongozi wa dini ya Kiislamu Mkoa wa Pwani, wamefanya dua maalumu ya kuuombea mkoa huo ili kuirejesha hali ya usalama.Dua hiyo imefanywa wakati wilaya tatu za mkoa huo, Kibiti, Mkuranga na Rufiji zikikabiliwa na matukio ya mauaji ya mara kwa mara ya wenyeviti wa vijiji na maaskari polisiAlhamisi iliyopita watu wasiofahamika waliwashambulia na kuwaua polisi wanane waliokuwa doria katika Kijiji cha Jaribu, wilayani Kibiti. Askari mmoja alinusurika na kujeruhiwa mkononi.Mauaji mengine yanayotokea katika maeneo hayo ni kama lile la kuuawa kwa Mkuu wa Upelelezi Wilaya ya Kibiti, Peter Kubezya.Hadi sasa viongozi wa vijiji zaidi ya 10, katika wilaya hizo wameuawa kwa kupigwa risasi au kukatwa mapanga tangu mwaka jana.
Wakizungumza katika dua hiyo iliyofanyika katika Msikiti wa Ijumaa, Ikwiriri juzi, Mwenyekiti wa Baraza la Waislamu Tanzania (Bakwata) Wilaya ya Mkuranga Sheikh Mohammed Katundu alisema wao kama viongozi wa dini wamelazimika kufanya ibada hiyo kuziombea amani wilaya hizo ili matukio ya mauaji yasiendelee kutokea.“Endeleeni kushirikiana na vyombo vya dola kuwafichua wanaojihusisha na mauaji ya viongozi wa vijiji pamoja na polisi kwa kuwa wauaji hao wanakiuka maagizo ya Mwenyezi Mungu,” alisema.
Aliiomba jamii kushirikiana na vyombo vya dola kuwafichua wahalifu wote wanaojihusisha na mauaji ambayo ni kinyume na maagizo ya Mwenyezi Mungu.Dua hiyo maalumu pia ilihusisha kuwaombea wote waliopoteza maisha yao katika matukio hayo ikiwamo polisi wanane waliofariki juzi kwa kupigwa risasi.Mjumbe wa Bakwata Mkoa wa Pwani, Sheikh Ramadhan Kinjumbi akizungumza mara baada ya dua hiyo alisema matukio ya mauaji katika wilaya hizo yanawanyong’onyesha wananchi na kudhoofisha utendaji kazi.
Alisema kutokana na hali hiyo jamii inapaswa kuzingatia na kutii maagizo yanayotolewa na Serikali na kutii amri zinazotolewa na Jeshi la Polisi hapa nchini.“Kiini cha mauaji bado hakijajulikana huku Jeshi la Polisi likiendelea na msako kuwakamata wahalifu hao na wakati uchunguzi dhidi ya matukio ya mauaji hayo ukiendelea, jamii inapaswa kuendelea kuwafichua wanaohusika,” alisemaMkazi wa Ikwiriri, Hamisi Libonike akizungumza katika eneo hilo alisema matukio hayo yamezidi kuleta simanzi kwa wananchi.
“Naamini mauaji haya yataondoka iwapo tu wananchi wataendelea kushirikiana na Jeshi la Polisi kuwafichua wahalifu hao,” alisema.
Alitoa wito kwa Polisi kuimarisha ulinzi wilaya za Mkuranga, Kibiti na Rufiji na kutaka juhudi ziendelee kuwasaka watu wote wanaojihusisha na vitendo vya mauaji.Mapema akizungumza jana Ijumaa jijini Dar es Salaam na waandishi wa habari, Kamishna wa Operesheni na Mafunzo wa Polisi Nsato Marijani alisema matukio ya mauaji yanayoendelea kutokea si ya kigaidi.
Alisema ni kundi la watu wachache la uhalifu ambao wamezuiliwa na Jeshi la Polisi kufanya shughuli zao. Alitoa wito kwa wananchi kuliunga mkono Jeshi la Polisi kwenye operesheni ya kuwasaka wahalifu hao.
Mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi na Usalama mkoa wa Pwani, ambaye pia ni Mkuu wa Mkoa wa huo, Mhandisi Evarist Ndikilo aliwatoa hofu wananchi wa wilaya hizo akisema hali ya ulinzi na usalama ni nzuri.
Alisema wananchi wanapaswa kuendelea na shughuli zao kama kawaida kwani Serikali imeimarisha ulinzi maeneo yote ya wilaya za Kibiti, Rufiji na Mkuranga huku akisisitiza wahalifu watakamatwa siku si nyingi.
Pia Ndikilo aliwataka viongozi wa dini zote kutokukubali nyumba za ibada kutumiwa na wahalifu na badala yake wawahimize waumini wao kufichua wahalifu.

Comments

Popular posts from this blog