RAIS MAGUFULI: OLE WAKE ATAKAYEIZUIA KAMATI YA KUCHUNGUZA MCHANGA WA DHAHABU
Hafla
ya kiapo kwa wajumbe wa kamati hiyo imefanyika Ikulu Jijini Dar es
Salaam na kuhudhuriwa na viongozi mbalimbali wakiwemo Mwanasheria Mkuu
wa Serikali Mhe. George Mcheche Masaju, Katibu Mkuu Kiongozi Mhe. Balozi
John Kijazi, Kamishna wa Maadili Mhe. Jaji Harold Nsekela na viongozi
wa vyombo vya ulinzi na usalama.
Kamati
hiyo ya wanasayansi 8 walioteuliwa na Mhe. Rais Magufuli tarehe 29
Machi, 2017 inaongozwa na Mwenyekiti wake Prof. Abdulkarim Hamis Mruma
na itafanya kazi ya uchunguzi kwa siku 20 kisha kuwasilisha ripoti yake
kwa Mhe. Rais.
Akizungumza
baada ya kuwaapisha, Mhe. Rais Magufuli amesema ameamua kuunda kamati
hiyo yenye wasomi waliobobea katika masuala ya jiolojia, kemikali na
uchambuzi wa kisayansi ili wawawakilishe Watanzania zaidi ya Milioni 50
ambao wanataka kujua ukweli kuhusu rasilimali yao ya madini.
“Hivi
sasa duniani kuna vita nyingi na vita mojawapo ni vita ya uchumi, kwa
hiyo tunawatuma nyinyi mwende mkapigane vita hii katika sekta hii ya
madini, mkawawakilishe Watanzania zaidi ya Milioni 50, mkapate ukweli
wote na wala msikubali kuyumbishwa na mtu yeyote, tumieni utaalamu wenu,
busara zenu, uzalendo wenu kwa Taifa na upendo wenu kwa Watanzania hasa
masikini wenye shida nyingi” amesema Mhe. Rais Magufuli.
Mhe.
Dkt. Magufuli amewahakikishia kuwa Serikali itatoa kila aina ya
ushirikiano kufanikisha kazi hiyo na ametaka wawe huru kutumia vitendea
kazi vyovyote vinavyohitajika zikiwemo maabara mbalimbali za taasisi za
Serikali na nyinginezo.
“Nendeni
popote mnapohitaji kufanya kazi tutawapa ushirikiano, fungueni
makontena popote yalipo, chukueni sampuli na mkazipime mjue kilichomo na
naviagiza vyombo vya dola vihakikishe hakuna mtu
atakayewakwamisha”amesisitiza Mhe. Rais Magufuli
Aidha,
Mhe. Dkt. Magufuli amesema baada ya kuunda kamati hii ya wanasayansi
ataunda kamati nyingine ya wachumi na wanasheria kwa ajili ya kufanya
tathmini na kuiangalia sera na sheria ya madini kwa lengo la kupata
taarifa zaidi juu ya biashara ya madini hapa nchini.
Wakati
huo huo, Mhe. Rais Magufuli amekutana na kufanya mazungumzo na Kiongozi
Mkuu wa Jumuiya ya Kihindu ya BAPS Swaminarayan Sanstha Duniani Mtukufu
Mahant Swami Maharaj ambaye yupo nchini kwa ziara ya siku 7.
Pamoja
na kumshukuru kwa ujio wake hapa nchini, Mhe. Rais Magufuli
amemhakikishia kuwa Serikali ya Tanzania itaendeleza na kuimarisha zaidi
uhusiano na ushirikiano wake na Jumuiya hiyo na amewaalika
wafanyabiashara walio chini ya Jumuiya hiyo kuja nchini Tanzania
kuwekeza katika viwanda, kilimo na shughuli nyingine za biashara na
uwekezaji.
“Nimefurahishwa
sana na ujio wako Mtukufu Mahant Swami Maharaj, sisi Tanzania tumekuwa
tukishirikiana na Jumuiya ya Hindu tangu miaka mingi, nitafurahi kama
mtaungana na juhudi za Serikali ya Tanzania kujenga viwanda, njooni
mjenge viwanda na Serikali itawapa ushirikiano wowote
mtakaohitaji”amesema Mhe. Rais Magufuli.
Mtukufu
Mahant Swami Maharaj ambaye amefanya dua ya kuliombea Taifa na Rais,
amemshukuru Mhe. Rais Magufuli kwa kukutana nae na amemhakikishia kuwa
uhusiano na ushirikiano kati ya Jumuiya hiyo na Tanzania ulioanzishwa
tangu enzi za utawala wa Awamu ya Kwanza ya Tanzania unaendelezwa na
kukuzwa zaidi.
Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Dar es Salaam
01 Aprili, 2017
Comments
Post a Comment