Nape amtaka Rais Magufuli aunde tume
Mbunge wa Jimbo la Mtama mkoani Mtwara kupitia tiketi ya CCM, Mhe. Nape
Nnauye amtaka Rais Magufuli aunde tume huru ambayo itaweza kuchunguza
matukio ya uhalifu ya uvamizi wa studio unaoendelea nchini.
Mbunge Nape Nnauye akilia kwa furaha baada ya wananchi wa jimbo lake
wakimtaka kupita juu ya migongo ya wamama ambao walijipanga ili kiongozi
wao huyo apite juu yao, kwa heshima.
Hatua hiyo inatokana na matukio ya kiuhalifu yanayoendelea Tanzania na
kuacha maswali mengi vichwani mwa wananchi kushindwa kufahamu kuwa watu
hao na vikundi hivyo vya kihuni vinavyofanya vitendo hivyo vinapata wapi
mamlaka hayo kuwa na nguvu kushinda Dola.
“Ombi langu kwa Rais namuomba aunde tume huru ichunguze matendo haya
yasijirudie tena kwa sababu yasipochukuliwa hatua yataharibu sura ya
Tanzania pia yataweza kuibuka makundi ya wahuni kuanza kuteka watu nao
kwa kuwa hakuna hatua zinazochukuliwa. Tumsaidie Rais Magufuli kwa
kumwambia ukweli naimani atasikia na atafanyia kazi kwa kuwa Rais wetu
anapenda kusikiliza watu”. Alisema Nape
Aidha Mbunge huyo amesema watu wanaofanya mambo hayo wanalengo la
kuwagombanisha wananchi na Rais wao jambo ambalo sio zuri kwa taifa.
"Juzi amepotea msanii Roma Mkatoliki na wengine lakini mpaka sasa
haifahamiki wapo wapi, yaani kama vile amepotea Nzi, tulisikia kijana
mmoja wa CHADEMA anaitwa Ben Sanane amepotea saizi miezi mitano imepita,
matendo haya ya kina Ben Sanane, Roma Mkatoliki, na wengine yanajenga
chuki ya wananchi kwa Rais, lakini pia yanajenga chuki kwa wananchi na
Chama Cha Mapinduzi (CCM) ". Alisema Nape Nnauye
Vile vile Nape amesema yeye mpaka sasa haamini yule mtu aliyemtolea
silaha siku ya mkutano wake na wanahabari kama alitumwa ila shida
aliyokuwa nayo ni kutaka kujua vyombo vya ulinzi na usalama vinafanya
nini mpaka matukio yote yanatokea.
Comments
Post a Comment