MZEE NDESAMBURO ALIVYOIPASUA CHADEMA KASKAZINI
Wiki
iliyopita kulikuwa na uchaguzi ndani ya Chadema ulilenga kuwapata
viongozi wa Kanda ya Kaskazini lakini ukahirishwa ghafla na siku ya
mwisho.
Kuahirishwa kwa huo, licha ya kunaonekana kama ni tukio la kawaida kulizingira na mambo mengi yaliyojificha nyuma ya pazia.
Chadema
imekuwa ikiendelea na mipango yake ya kupanga safu za uongozi kwa
kuzingatia sera yake ya kugatua madaraka ya chama kitaifa kwa ngazi za
Kanda na wiki iliyopita ilikuwa zamu ya Kanda ya Kaskazini – yaani mikoa
ya Arusha, Kilimanjaro na Tanga ambako uchaguzi huo ulikuwa ufanyike.
Uchaguzi
huo kulingana na vyanzo mbalimbali ndani ya chama hicho uliahirishwa
kutokana na mvutano ulioibuka ndani ya Kamati Kuu ya Chadema iliyoketi
Tanga, baada ya kuwapo shinikizo la kutaka mwenyekiti wa Chadema
Kilimanjaro, Philemon Ndesamburo asigombee nafasi ya mwenyekiti wa
Kanda.
Ndesamburo
ambaye amekuwa mbunge wa Jimbo la Moshi mjini (2000-2015) alipoamua
kutogombea, aliamua kuwania nafasi hiyo ya juu zaidi katika kanda
akibebwa na rekodi yake ya kukijenga chama hicho mkoani Kilimanjaro na
kuwa na nguvu kubwa.
Kilichozua
sintofahamu ni juu ya mwanasiasa huyo maarufu kama Ndesa Pesa kuambiwa
aondoe jina lake kutokana na uzee huku kukiwapo tuhuma za kukivuruga
chama, madai yanayoelezwa kuanzia ndani ya Kamati Kuu ya chama iliyoketi
Tanga.
Nyuma ya pazia
Taarifa
zilizovuja kutoka ndani ya chama hicho zinadai katika kikao hicho
kilichohudhuriwa na wajumbe wa Kamati Kuu na wabunge wa Kanda ya
Kaskazini, Ndesamburo alihojiwa na Kamati Kuu kwa madai ya kukivuruga
chama mkoani Kilimanjaro.
“Ndesamburo
alihojiwa hasahasa madai kuwa yeye ndiye anakivuruga chama pale Moshi,
kwamba ameshindwa kukisaidia na ndiye analea migogoro Kilimanjaro,”
kilidokeza chanzo chetu.
Mbali
na madai hayo, Ndesamburo aliombwa aondoe jina lake kwa sababu ya kile
wajumbe wa Kamati Kuu walidai kuwa umri umemtupa, lakini inadaiwa
mwanasiasa huyo alikataa kuondoa jina lake.
“Ndesamburo
alikataa kuondoa jina lake kwa sababu miongoni mwa watu walioijenga
Chadema Kilimanjaro ni yeye na katiba haijatoa kigezo cha umri wa
kugombea uenyekiti.”
Imedokezwa
kuwa baada ya kukataa kwake, iliundwa kamati ndogo yenye wajumbe wanne
ikapewa jukumu la kwenda kumshawishi Ndesamburo aondoe jina.
“Hiyo
kamati ilimfuata Ndesamburo na kumuomba aondoe fomu yake kwa ahadi kuwa
wangempa nafasi ya mjumbe wa kudumu wa Kamati Kuu ya Chadema, lakini
alikataa,” kilidokeza chanzo kingine.
Baada
ya hatua hiyo kukwama, ndani ya kikao cha Kamati Kuu kuliibuliwa madai
mengine kutoka kwa meya mmoja kuwa fomu za kugombea nafasi hiyo
zilifichwa na alipewa Ndesamburo peke yake.
Inaelezwa
kuwa meya huyo ambaye inadaiwa alikuwa na kundi linalomuunga mkono
mgombea mwingine, Daniel Porokwa alipendekeza uchaguzi uahirishwe ili
wanachama wengi wapate fursa ya kugombea.
Hata
hivyo, habari zinasema madai hayo yalipingwa na uongozi wa Chadema na
kueleza kuwa matangazo ya uchukuaji fomu yalitangazwa kwa uwazi na bila
kificho na ilitolewa miezi minne.
Mbali
na hoja hiyo, inadaiwa kuwa Mbunge wa Rombo, Joseph Selasini alisimama
na kuwatuhumu Mbunge wa Moshi Mjini, Jaffar Michael na Lazaro kuwa ndiyo
wanavuruga uchaguzi kwa vile hawamtaki Ndesamburo.
“Hiyo
kauli ilichafua hali ya hewa kwa vile Jaffar alisimama na kurushiana
maneno makali na (Joseph) Selasini (mbunge wa Rombo). Kama wangekuwa
wenyewe ngumi zingelia mle ndani,” alidokeza mjumbe mmoja.
“Mgogoro
wote huu ni uchaguzi wa 2020. Jaffar na Anthony Komu (mbunge wa Moshi
Vijijini) wanaona kama Ndesamburo atakuwa mwenyekiti wa Kanda, nafasi
yao ya kupitishwa itakuwa ndogo,” kilidokeza chanzo chetu.
Inadaiwa
kuwa hofu hiyo inajengeka kwa sababu Ndesamburo na Jaffar hawaivi
chungu kimoja na hawasalimiani, wakati Komu ana hofu inayotokana na
kuenguliwa jina la binti wa Ndesamburo, Lucy Owenya kwenye ubunge na
nafasi kupewa yeye.
Katika
kura za maoni zilizopigwa, Owenya alipata kura 266 wakati Komu alipata
kura 25, lakini Kamati Kuu ya Chadema baadaye ilimwengua Owenya na
kurejesha jina la Komu na akashinda ubunge.
Mmoja
wa watu waliokuwa viongozi wa Chadema mkoani Tanga ambaye aliomba jina
lake lisitajwe, alidai kiongozi pekee wa kumlaumu kwa hicho kinachotokea
ni Mwenyekiti wa Taifa, Freeman Mbowe.
“Binafsi
namlaumu mwenyekiti wangu. Aliruhusije mzee Ndesamburo adhalilishwe
vile ndani ya kikao cha Kamati Kuu? Hivi leo tunamlipa mzee wa watu yule
wema kwa ubaya?” alihoji.
Hata
hivyo, kiongozi mwingine alidai kuna mpasuko mkubwa ndani ya Chadema
katika Manispaa ya Moshi unaochangiwa na kutokuelewana kati ya
Ndesamburo na Jaffar.
Ndesamburo, Komu watoa ya moyoni
Ndesamburo
alipotafutwa na gazeti hili kuzungumzia hatua ya yeye kutakiwa
asigombee uenyekiti wa kanda, alisema yaliyojitokeza ndani ya kikao
hawezi kuyazungumzia kwa sababu ni faragha.
“Unataka
nikueleze nini? Mimi yote yanayoendelea namwachia Mungu na wala
sitaongeza neno zaidi ya hapo. Mchango wangu kwenye chama unajulikana.
Namwachia Mungu,” alisema Ndesamburo.
Alipoulizwa
kuhusu mtafaruku huo, Komu alisema ni kweli hamuungi mkono Ndesamburo
kuwa mwenyekiti wa kanda na hilo amelisema hata ndani ya kikao.
“Mimi
ni kweli simuungi mkono mzee Ndesamburo kuwa mwenyekiti wa Kanda,
lakini sina kundi ambalo nakaa nalo eti kufanya mikakati ya kumkataa.
Mimi siyo mnafiki na ni muwazi. Kwenye hicho kikao nilitoa hoja ya umri.
Hata kwenye Kanisa Katoliki ukiwa na umri wa miaka 75 unaacha uaskofu,
lakini mzee Ndesamburo ana umri wa miaka 84,” alisisitiza Komu.
Mbali
na hoja ya umri, mbunge huyo alisema anapinga Ndesamburo kuwa
mwenyekiti kwa sababu katika uongozi wake wa mkoa wa Kilimanjaro
kumekuwapo na vurugu na mpasuko ndani ya chama.
“Kila
mahali hapo (Kilimanjaro) kuna vurugu watu hawaelewani, kwa hiyo
mnataka tuhamishie vurugu zihamie kwenye kanda? Huu ndiyo msimamo wangu
wala simpingi kwa sababu nyingine,” alisema.
Hata
hivyo, mbunge mmoja kutoka moja ya mikoa ya Kaskazini ambaye alikataa
kutajwa alitaka suala la umri lisiwe kigezo kwani siyo la kikatiba,
hivyo wapigakura ndiyo wapewe fursa ya kuchagua kiongozi wanayemtaka.
“Tusimbebeshe
Ndesamburo migogoro kwenye majimbo ya Hai, Moshi Vijijini, Moshi Mjini
na Rombo, tena huko kuna viongozi wa kitaifa. Migogoro ni kielelezo
taasisi iko hai,” alisema.
Selasini
alipotafutwa aeleze tafrani iliyotokea kati yake na Jaffar alisema
hawezi kuzungumza lolote na anaheshimu taratibu za vikao.
Akizungumzia mtafaruku huo, Jaffari alisema hayo ni mambo ya ndani ya chama hawezi kuyazungumzia nje.
Comments
Post a Comment