MFANYABIASHARA Achomwa Visu 14 na Kaka’ke..!!!

 Mfanyabiashara wa samaki, Warioba Mtatiro, mkazi wa Kijiji cha Etalo, Musoma Vijijini,
amedaiwa kujeruhiwa vibaya kwa kisu na kaka yake (jina tunalihifadhi).

Tukio hilo la kusikitisha limetokea hivi karibuni katika Mtaa wa Nyamulinda, Kijiji cha Etalo, Musoma Vijijini. Kwa mujibu wa chanzo kilichoshuhudia mtiti huo, Mtatiro alikuwa akicheza kamari maarufu mkoani Mara kwa jina la Magaramka na kaka yake ndiye aliyekuwa akichezesha.

Alisema baada ya ‘kupunwa’, Mtatiro hakuwa na kiasi hicho cha fedha kilichohitajika katika mchezo huo ndipo ugomvi ukaibuka hadi kufikia hatua ya kaka kumchoma visu mdogo wake. “Mtatiro alipunwa shilingi mia tano. Sasa kaka yake akawa anamdai na yeye akawa hana ndipo alipoamua kuchukua kisu na kuanza kumchoma.

“Alimchoma sehemu mbalimbali mwilini, kichwani na mgongoni na kumsababishia majeraha makubwa. Kwani alikuwa anachoma kisha anachomoa na kuchoma sehemu nyingine kama mara 14,” kilisema chanzo hicho.

Chanzo hicho kilieleza kuwa, baada ya watu kuamulia, kaka mtu alikamatwa na kupelekwa Kituo cha Polisi Musoma kwa ajili ya hatua za kisheria huku majeruhi akikimbizwa katika Hospitali ya Mkoa wa Mara.

Majeruhi huyo anafanya biashara ya kuuza samaki katika kontena la samaki lililopo Mtaa wa Nyamulinda, jirani na eneo walilokuwa wakicheza kamari hiyo.

Akizungumza na Risasi Jumamosi kwa shidashida mara baada ya kutokea kwa tukio hilo, Mtatiro alisema kaka yake huyo alimchoma visu hivyo baada ya kushindwa kumlipa shilingi 500 aliyomshinda kwenye kamari.

“Baada ya kunipuna nilimwambia sina lakini yeye hakutaka kunielewa, akaanza kunishambulia kwa visu.

Kanichoma sana visu mgongoni, nashukuru Mungu kama si watu kuniamulia, angeniua
yule,” alisema Mtatiro. Risasi Jumamosi lilimtafuta Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mara, ACP Jafari Mohamed kuhusiana na tukio hilo ambapo alipopatikana alisema bado halijamfikia.

“Nashukuru kwa kunipa hizo taarifa, nitazifanyia kazi maana bado hazijafika mezani wangu hivyo nitafuatilia,” alisema Kamanda Mohamed.

Comments

Popular posts from this blog