Mali za Lugumi Mikononi mwa TRA
Kampuni ya udalali ya Yono,
imefanikiwa kukamata mali za wafanyabiashara wanaodaiwa kodi ya serikali
inayofikia zaidi ya Sh bilioni 68.1. Operesheni ya kukamata mali hizo
kwenye maeneo mbalimbali ndani na nje ya Jiji la Dar es Salaam imefanywa
ndani ya wiki moja.
Katika operesheni hizo maofisa wa
Yono wamekuwa wakishirikiana na maofisa wa Mamlaka ya Mapato(TRA),
ambayo ndiyo imeipa kampuni hiyo kazi ya kukusanya kodi kwenye maeneo
mbalimbali nchini.
Kwa mujibu wa Mkurugenzi Mtendaji wa
Kampuni ya Yono, Scholastica Kevela, Yono imepewa kazi na TRA kukusanya
madeni yake ya kodi kwenye mikoa ya Dar es Salaam, Pwani Njombe, Mbeya,
Iringa na Zanzibar.
Aliwataka watanzania kuunga mkono
jitihada za Rais John Magufuli za kuleta maendeleo kwa kulipa kodi bila
shuruti ili zipatikane fedha za kujenga miundombinu kama barabara, reli,
shule, madaraja, hospitali na zahanati.
Kuhusu taarifa zilizozagaa kwenye
mitandao ya kijamii kwamba hata baadhi ya mali za Kampuni ya Lugumi
zimeshikiliwa, Mkurugenzi huyo alithibitisha kuwa habari hizo ni za
kweli ambapo wanashikilia nyumba za kifahari za mfanyabiashara huyo.
“Mmeniuliza
kwamba mmesikia nyumba za Lugumi zimefungiwa ni kweli, amefungiwa
nyumba zake za kifahari na anadaiwa Sh bilioni 14, yupo mtu anaitwa Gm
Dewji naye anadaiwa Sh bilioni 1.8, Kampuni ya ujenzi ya Mutluhan
Construction anadaiwa Sh bilioni 45,” alisema.
Alisema wanaodaiwa wanapaswa kulipa
madeni yao TRA ndani ya siku 14 na kwamba muda huo ukipita watapewa
maelekezo na serikali kama ni kuuza mali hizo ili kufidia madeni yao.
Ofisa Mwandamizi wa TRA, ambaye
hakupenda jina lake litajwe alithibitisha kwamba nyumba ya Lugumi
iliyoko Upanga mtaa wa Mazengo inashikiliwa na mamlaka hiyo na ghorofa
la kifahari lililoko Mbweni JKT, Dar es Salaam.
“Hakuna
siri maana mkienda kwenye hizo nyumba mtakuta alama ambazo huwa Yono
wanaweka kwa nyumba inayoshikiliwa, nendeni Upanga na kule Mbweni JKT
mtakuta hizo nyumba tunazoshikilia,” alisema
Comments
Post a Comment