Kama Unaumwa Tumbo Wakati Wa Hedhi soma hapa
KARIBU sana katika makala yetu inayohusu afya. Kutokana na simu nyingi
ninazozipata nikiulizwa maswali juu ya maumivu yanayowapata akina mama
wengi wakati wa hedhi nimeona ni bora niandike makala hii ili iweze
kuwasaidia na wengine kujua nini chanzo na mhusika afanye nini pale
anapopatwa na tatizo hilo.
Maumivu wakati wa hedhi (period pains) au kitaalamu dismenorrhea, ni
maumivu yanayojitokeza sehemu ya chini ya tumbo au kiunoni wakati
mwanamke anapoanza kupata siku zake au kabla ya hapo.
Maumivu hayo huweza kuwa madogo au ya wastani huku baadhi ya wanawake
wakipata maumivu makali sana. Maumivu hayo huanza pale yai linapotoka
katika mrija (fallopian tube) na kuteremka chini ya mrija huo wakati wa
Ovulation.
AINA YA MAUMIVU
Maumivu ya tumbo la hedhi yapo ya aina mbili. Ya kwanza ni maumivu
yasiyokuwa na sababu zozote za kimsingi za kitiba. Katika aina hii
maumivu ni ya kawaida na huhisiwa sehemu ya chini ya tumbo na kiunoni.
Maumivu hayo huanza siku moja au mbili kabla ya hedhi na humalizika
baada ya siku mbili au nne.
Aina ya pili ni yale maumivu yanayojumuisha maumivu yanayosababishwa na
sababu nyinginezo za kitiba kama vile matatizo katika kizazi, ugonjwa
wa nyonga (PID) na matatizo katika mirija ya mayai.
Nusu ya wasichana na wanawake hupata maumivu wakati wa hedhi na karibu
asilimia kumi mpaka kumi na tano wanasema kuwa hupata maumivu makali.
Uchunguzi unaonesha kuwa kuna sababu mbalimbali zinazoweza kuongeza uwezekano wa kuumwa tumbo wakati wa hedhi.
Sababu hizo ni kama kuwa na umri wa chini ya miaka 20, kuvunja ungo
wakati wa miaka 11 au chini ya miaka hiyo, kutoka damu nyingi wakati wa
hedhi, wanawake ambao hawajawahi kuzaa.
Magonjwa yanayoweza kusababisha mtu kupatwa na maumivu ya tumbo la hedhi. Miongoni mwa magonjwa hayo ni:
Endometriosis. Hii ni hali ambayo seli za ndani ya mfuko wa uzazi huanza kuoka nje ya fuko hilo, au hata sehemu nyinginezo
Adenomyosis: Huu ni ugonjwa wa wanawake ambapo tezi au uvimbe (tumors) zinaota katika mfuko wa uzazi.
PID au Ugonjwa wa uvimbe katika nyonga.
Magonjwa ya zinaa yanayotokana na bakteria au magonjwa ya kuambukiza ya zinaa.
Mlango wa uzazi unapokuwa mdogo kiasi kwamba unazuia damu ya hedhi isitoke kwa urahisi.
baadhi ya magonjwa yanayoweza kusababisha mtu kupatwa na maumivu ya
tumbo la hedhi. niliishia kuelezea ugonjwa wa uvimbe katika nyonga ambao
husababishwa na magonjwa ya zinaa yanayotokana na bakteria au magonjwa
ya zinaa.
Dalili za ugonjwa huo ni:
Maumivu kuja na kuondoka, kwa kiwango tofauti (spasmodic).
Maumivu zaidi huwa sehemu ya chini ya tumbo na huchanganyika na maumivu
ya sehemu ya chini ya mgongo ambayo husambaa mpaka mapajani.
Kujihisi kutapika, kichefuchefu na wakati mwingine hata kutokwa jasho.
Kupata choo laini au hata kuharisha na wengine hufunga choo.
TUMBO KUWA KUBWA AU KUWA GUMU.
Kupata maumivu ya kichwa, kujisikia kuchoka.
Kiwango cha maumivu ya tumbo la hedhi na mchanganyiko wa dalili
inategemea mtu na mtu, mtu mwingine anaweza akawa anapata karibu dalili
zote nilizozitaja hapo juu na mwingine ni baadhi tu au hata dalili moja.
Wanawake wengi hujitambua bila hata msaada wa daktari.
USHAURI
Iwapo mwanamke atapata maumivu makali sana ni bora akamuone daktari ili
wafanye vipimo kama vile Ultrasound, CT na CT-Scan, MRI na vinginevyo
ili kufahamu nini chanzo cha maumivu hayo kuwa makali
MATIBABU
Matibabu ya maumivu ya tumbo la hedhi kwa kawaida huweza kutibika kwa
urahisi kwa kutumia vidonge vya kupunguza maumivu, kama vile Ibuprofen,
naproxen au aina nyinginezo za vidonge visivyokuwa na steroids (NSAIDS).
Pia kuna wakati madaktari wanaweza kumshauri mgonjwa kutumia vidonge
vya kuzuia mimba, Vidonge hivyo huzuia mzunguko wa yai au Ovulation na
kupunguza ukali wa maumivu ya tumbo la hedhi.
Pia wanawake wanashauriwa kufanya baadhi ya vitendo ambavyo hupunguza
maumivu hayo, kama kuoga maji moto, kuweka kitambaa chenye joto katika
sehemu ya chini ya tumbo, kufanya mazoezi kama yoga, meditation,
kutumia vidonge vya vitamin E, Thiamine na Omega 3 kumetajwa kuwa
husaidia katika suala hilo. Wanawake wanaopatwa na matatizo kama
hayo ni bora wapumzike vyema na kupata usingizi wa kutosha.
Vilevile unaweza kujiepusha na kupatwa na maumivu ya tumbo la mwezi kwa kufanya yafuatayo:
Kujitahidi kula matunda, mbogamboga na kupunguza kula vyakula vyenye
mafuta mengi, pombe, kafeini, sodium na sukari, kufanya mazoezi ya
viungo, kujiepusha na wasiwasi na mawazo na kuepuka kuvuta sigara.
Comments
Post a Comment