VIROBA VYA BILIONI 5 VYAKAMATWA DAR
KATONI 32,634 za pombe kali
zilizofungashwa kwenye vifungashio vya plastiki (viroba) zenye thamani
ya zaidi ya Sh bilioni 5.18 zimekamatwa jana, katika operesheni maalumu
ya utekelezaji wa maelekezo ya Serikali ya kusitisha uzalishaji,
usambazaji, uingizaji, uuzaji na matumizi ya pombe hizo.
Pombe hizo zimekamatwa katika
operesheni inayoendelea katika mikoa mitatu ya Kikodi ya Mamlaka ya
Mapato Tanzania (TRA) Dar es Salaam ambayo ni Temeke, Kinondoni na
Ilala.
Akizungumza katika operesheni
hiyo, Mkaguzi kutoka Mamlaka ya Chakula na Dawa (TFDA), John Nzila
alisema walikamata katoni 14,393 za konyagi, katoni 9,964 za Vradmill,
Zanzi 31 na Valeur. 268.
Alisema mzigo huo ulikutwa
katika ghala la Loverira Enterprises lililopo Kimara Temboni na kwamba
mzigo huo umezuiwa kwa hatua zaidi.
Kwa upande wake Mwanasheria
Mwandamizi wa Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira
(NEMC), Heche Suguta alisema kuwa walikamata katoni 7,000 za viroba vya
aina mbalimbali zikiwemo Konyagi, Zanzi pamoja na Burudani vyote vikiwa
na thamani zaidi ya Sh bilioni 2.
Alisema vinywaji hivyo
vilikutwa katika duka la Love Kira Enterprises lililopo Wazo na kwamba
mzigo huo umezuiwa hadi utaratibu mwingine utakapotangazwa.
Kwa upande wa Temeke
yalikamatwa maboksi matano ya Konyagi, maboksi 15 ya Black Bee, maboksi
nane ya Zanzi na Maboksi matano ya Valeur.
Ofisa Afya wa Manispaa ya
Temeke ambaye pia ni mratibu wa Masuala ya Chakula katika Manispaa hiyo,
Rehema Sadick alisema katika operesheni hiyo wamegundua kwamba
wafanyabiashara wengi hawana vibali vya TFDA na leseni za biashara.
Hata hivyo katika operesheni
hiyo pia kulibainika kuna baadhi ya wafanyabiashara wanauza vileo
vilivyokwisha muda wake na hivyo kuvikamata kwa ajili ya kuokoa afya za
watumiaji.
Comments
Post a Comment