Umoja wa Mataifa waingilia kati sakata la kupotea kwa Ben Saanane
Sakata
la kupotea kwa mkuu wa Idara ya Sera na Utafiti wa Chadema, Ben Saanane
limechukua sura nyingine baada ya Umoja wa Mataifa (UN) kusema upo
tayari kutuma watu nchini kwa ajili ya uchunguzi.
Saanane, ambaye pia ni msaidizi wa mwenyekiti wa Chadema, Freeman
Mbowe, alipotea katika mazingira ya kutatanisha Novemba 18 mwaka jana na
hadi sasa haijaeleweka kuwa alitekwa au kuuawa, ingawa Chadema
imehusisha kutoweka kwake na taarifa ambayo Saanane aliitoa kwenye
mitandao ya kijamii kuhusu utata wa elimu ya baadhi ya viongozi.
Siku chache baada ya kupotea kwa Saanane, Mwanasheria Mkuu wa
Chadema, Tundu Lissu aliitaka Serikali kueleza kama inamshikilia kada
huyo au ifanye uchunguzi wa kina kuhusu kupotea kwake.
Sanjari na hilo, Lissu aliitaka Serikali kufuatilia ujumbe wa
vitisho ambao Saanane aliwahi kutumiwa kwenye simu yake ya mkononi na
mtu ambaye bado hajafahamika.
Akisisitiza msimamo wa chama chake, Lissu alizitaka mamlaka zote
husika na usalama wa raia ziseme hali halisi inayozingira sintofahamu ya
mahali alipo, ikiwa yuko ndani ya nchi au nje, au hata kama amefariki
na kuzikwa kwa kutotambuliwa.
Wakati utata huo ukiendelea, ofisi ya kamishna mkuu wa haki za
binadamu duniani ya UN yenye makao yake makuu jijini Geneva, Uswisi,
imesema iko tayari kutuma timu ya uchunguzi.
Uamuzi huo ulifikiwa katika mkutano uliotishwa na ofisi hiyo, Kanda
ya Afrika uliohusisha nchi za Sudan, Rwanda, Burundi, Kenya, Uganda,
Ethiopia, Djibouti na Tanzania.
Jana, mkurugenzi wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), Dk
Hellen Kijo- Bisimba alisema suala hilo liliibuka baada ya wajumbe wa
mkutano huo kutaka kujua undani wa sakata hilo, lakini hakukuwa na
taarifa za kina.
“Wajumbe walionyesha kuguswa na suala la mtu kupotea katika
mazingira ya utata na kutaka tuelezee kwa undani ilivyokuwa. Hatukuwa na
taarifa za kina hivyo wakasema wako tayari kulifanyia kazi endapo
tutatuma urgent alert,” taarifa ya dharura.
“Taarifa tutakayotuma ndiyo itakayowawezesha wao kutuma timu ya
uchunguzi ije hapa baada ya hapo watajua ni kitu gani waseme kwa
Serikali.”
Dk Bisimba alieleza kuwa bado taarifa hiyo haijaandikwa kutokana na
kuwasubiri ndugu wa Saanane ambao wanatakiwa kutoa maelezo kwa kina.
“Tuliwaambia ndugu zake waje tupate maelezo yatakayotuwezesha
kuandika hiyo urgent alert, lakini bado hawajaja. Watakapofika
tutaandika na kuituma ili uchunguzi ufanyike.”
Alipotafutwa kuhusu maendeleo ya uchunguzi wa suala hilo,
Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai(DCI), Kamishna Robert Boaz
alisema: “Nitafute Jumatatu kwa sasa nipo kwenye kikao.”
Comments
Post a Comment