SAKATA LA RC PAUL MAKONDA KUVAMIA CLOUDS LAVUKA MIPAKA YA TANZANIA
Asasi
za kiraia 33 barani Afrika zimelaani kitendo cha kuvamiwa kwa studio za
televisheni ya Clouds na kulazimisha maudhui yasiyostahili yarushwe
hewani.
Tamko
la asasi hizo limetolewa ikiwa ni siku chache baada ya Tume ya Haki za
Binadamu na Utawala Bora, (THBUB), Jukwaa la Wahariri (TEF) na Kituo cha
Sheria na Haki za Binadamu (LHRC) kulaani kitendo hicho kinachodaiwa
kukandamiza uhuru wa vyombo vya habari.
Asasi
hizo zinazohusika na utawala bora, demokrasia, haki za binadamu na
uhuru wa habari zilikutana hivi karibuni mjini Kampala nchini Uganda
katika mkutano uliokuwa ukizungumzia uhuru wa kujieleza na kupata
habari.
Tanzania
kwenye mkutano huo iliwakilishwa na Mtandao wa Watetezi wa Haki za
Binadamu (THRDC) , miongoni mwa mijadala iliyotawala ni kukemea vitisho
na vitendo vya kunyanyasa waandishi.
Pia,
wajumbe katika mkutano huo waligusia mabadiliko madogo ya baraza la
mawaziri yaliyofanywa na Rais John Magufuli kwa kumtoa Nape Nnauye
kwenye nafasi ya Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo.
Asasi
hizo zilimpongeza Nape ambaye kabla ya kuondolewa kwenye nafasi hiyo
aliunda kamati iliyochunguza tukio la uvamizi wa studio za Clouds,
wakisema uamuzi huo ulionyesha ujasiri wa kusimamia uhuru wa vyombo vya
habari na uhuru wa kujieleza.
Taarifa
kwa vyombo vya habari iliyotolewa na asasi hizo, ilidai kwa siku za
karibuni Tanzania imekuwa na matukio zaidi ya 40 yanayolenga kukandamiza
uhuru wa vyombo vya habari.
“Waandishi
wamekuwa wakizuiwa au wakati mwingine kubughudhiwa ili wasifanye kazi
yao. Vitendo hivyo vimekuwa vikifanywa hasa na wakuu wa wilaya na
polisi,” ilibainisha taarifa hiyo.
Wajumbe
walikumbusha kifungu cha pili cha Azimio la kanuni za uhuru wa
kujieleza Afrika la mwaka 2002, kinachoelekeza Serikali ihakikishe
inachukua hatua stahiki kuzuia uvamizi kwenye vyombo vya habari.
Kifungu
hicho kinaelezea endapo uvamizi huo utatokea, Serikali ina wajibu wa
kuchunguza na kuwaadhibu wahusika kwa mujibu wa kosa lao.
CHANZO:UDAKU SPACIAL
Comments
Post a Comment