Msukuma afunguka mazito, Ni kuhusu alivyokamtwa na Polisi

JOSEPH Kasheku “Msukuma” Mbunge waa Jimbo Geita Vijijini na Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Mkoa wa Geita ametoa siku tano za kuombwa na radhi na wanaodaiwa kuwa ni maofisa usalama wa Taifa waliotoa taarifa za uongo dhidi yake na kusababisha akamatwe Mjini Dodoma, anaandika Charles William.
Juzi Jeshi la Polisi Mkoa wa Dodoma, liliwatia nguvuni Msukuma, Hussein Bashe, Mbunge wa Jimbo la Nzega Mjini na Adam Malima, aliyewahi kuwa Mbunge wa Jimbo la Mkuranga kwa madai ya kupanga kufanya vurugu katika Mkutano Mkuu wa CCM uliofanyika jana.
Wanasiasa hao walikamatwa na kuhojiwa, kabla ya kuachiwa kwa dhamana. Hata hivyo Msukuma amesema hawezi kukaa kimya juu ya suala hilo na kwamba wapo maofisa usalama waliosambaza taarifa juu yake na kusababisha hofu lazima wamuombe radhi.
“Hawa ni wapiga dili, Rais lazima aiangalie upya Idara ya Usalama wa Taifa. Wameniundia mimi zengwe, mpaka nikakamatwa, na nchi ikawa kwenye presha, kama chama kisipozungumza mimi nitaenda kuzungumza na watoto wangu kama Askofu Gwajima (Josephat),” amesema.
Mbunge huyo anayesifika kwa vituko visivyoisha, amesema atapigania heshima yake kwani hajawahi kupata kashfa na lazima atashinda.
“Sitazungumza kitaifa, nitaenda kuzungumza na wapiga kura jimboni kwangu, nieleze kwanini watu wametengeneza kinyago wakakiweka sebuleni halafu kinawatisha wenyewe. Kama kuna usalama wa taifa aliyeshiriki natoa siku tano awe ameniomba msamaha,” amesema Msukuma.
Hofu ya kuibuka kwa vurugu katika mkutano mkuu wa CCM uliofanyika jana iliibuka baada ya juzi Halmashauri Kuu – NEC ya chama hicho kuchukua uamuzi wa kuwafukuza viongozi mbalimbali wanaodaiwa kuwa walikisaliti chama hicho katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2015.
Waliofukuzwa uanachama ni pamoja na wenyeviti wa CCM katika mikoa minne wakiwemo Ramadhani Madabida (Dar es Salaam) na Jesca Msambatavangu (Iringa). Sophia Simba, Mwenyekiti wa Umoja wa Wanawake wa CCM (UWT) ambaye pia ni Mbunge wa Viti Maalum alikutana na kadhia hiyo.
Chanzo: Mwanahalisi.
 

Comments

Popular posts from this blog