KESI YA MALKIA WA MENO YA TEMBO KUSIKILIZWA TENA WIKI IJAYO
Kesi
inayomkabili raia wa China, Yang Feng Glan (66) maarufu kama Malkia wa
tembo inayosikilizwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu jijini Dar
es Salaam itaendelea kusikilizwa kuanzia Aprili 5 hadi 7, mwaka huu.
Wakili
wa Serikali, Elia Athanas alidai katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu
mbele ya Hakimu Mkazi, Huruma Shaidi kuwa kesi hiyo imekuja kwa ajili
ya kusikilizwa na kwamba mawakili wanaosikiliza kesi hiyo hawapo.
Hata
hivyo, Wakili wa utetezi, Hassan Kiangio alidai kuwa kesi hiyo
imeahirishwa kwa mara ya pili tangu mshitakiwa Manase Philemon (39)
kudai amepigwa na kuteswa wakati akichukuliwa maelezo yake, ambapo
upande wa mashitaka ulitakiwa kuleta mashahidi ili kuthibitisha tuhuma
hizo.
Hatua
ya upande wa mashitaka kuleta mashahidi ni kusikiliza kesi ndogo ndani
ya kesi kubwa baada ya shahidi Sajenti Beatus (46) kutoka Wizara ya
Mambo ya Ndani ya Nchi, kudai kuwa aliandika maelezo ya mshitakiwa huyo
na baadaye mshitakiwa kupinga kupokelewa kwa maelezo hayo kwa madai kuwa
aliteswa na kupigwa.
Kiangio
alidai kuwa mashahidi watakaoletwa na upande wa mashitaka
watathibitisha ni kwa namna gani maelezo hayo yalichukuliwa. Kesi hiyo
imeahirishwa hadi Aprili 5 hadi 7, mwaka huu, kesi itakaposikilizwa
mfululizo.
Mbali
na mshtakiwa huyo, washitakiwa wengine ni Salvius Matembo (39) na
Philemon (39). Watuhumiwa hao wanatuhumiwa kufanya biashara ya vipande
vya meno ya tembo 706 vyenye uzito wa kg 18892 thamani yake ikiwa ni
shilingi bilioni 5.4 bila leseni ya Mkurugenzi wa wanyama pori.
Comments
Post a Comment