Dakika 180 za Makonda Bungeni zilikuwa hivi...
MKUU wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda jana alihojiwa kwa saa tatu
mfululizo na Kamati ya Haki, Kinga na Madaraka ya Bunge kwa tuhuma za
kuingilia haki, uhuru na madaraka ya chombo hicho cha kutunga sheria.
Makonda aliwasili Bungeni Dodoma majira ya saa nne asubuhi kuitikia wito
wa Kamati hiyo uliotokana na Azimio la Bunge lililotolewa Februari 8 na
kuhojiwa na kamati hiyo kwa muda wa saa tatu kuhusu tuhuma
zinazomkabili.
Katika kikao hicho, Bunge liliamua Makonda aitwe kujieleza kwenye Kamati
ya Bunge ya Haki, Kinga na Madaraka kwa tuhuma za kukashfu chombo
hicho.Sambamba na uamuzi huo, pia Bunge liliagiza mbunge yeyote ambaye kwa
namna yoyote anadhani amekashfiwa na Makonda, awasilishe malalamiko yake
kwa Spika ili hatua zaidi zichukuliwe.
Hatua ya kutaka Makonda aitwe mbele ya kamati hiyo, ilitokana na
mwongozo uliotolewa na Mbunge wa Mkuranga(CCM), Abdallah Ulega, kwa
Mwenyekiti wa Bunge, Andrew Chenge, aliyedai mkuu huyo wa mkoa
ameudharau mhimili huo wa dola na wabunge.
Akizungumza mara baada ya kumaliza kazi yao, Mwenyekiti wa Kamati ya
Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge, George Mkuchika alisema Makonda
alidaiwa kutoa kauli kupitia televisheni ya Clouds akidai kwamba wabunge
wanasinzia bungeni jambo lililoonekana kwamba ni kudharau mhimili huo
wa dola.
“Napenda kutoa taarifa kwamba mheshimiwa Makonda leo amekuja mbele ya
Kamati na ametupa ushirikiano mzuri," alisema Mkuchika ambaye ni mbunge
wa Newala Mjini (CCM).
"Tumepokea maelezo yake na Kamati imemaliza kazi yake.”
Alisema Kamati yake itakabidhi taarifa yake kwa Spika Job Ndugai kwa
mujibu wa kanuni, ambaye ndiye atakayeamua namna ya kutoa taarifa kuhusu
kazi ya kamati hiyo.
Katika mwongozo wake kwa Spika, Ulega kwa kutumia Kanuni ya 68 (7),
alisema kupitia vyombo vya habari, kuna taarifa kwamba Makonda ametoa
kauli ambazo zinaashiria na kuonyesha dharau kwa Bunge.
“Sisi wabunge tuko mstari wa mbele katika kuhakikisha tunapambana na
kumsaidia Rais (John Magufuli) kwenye vita dhidi ya dawa za kulevya.
Ikumbukwe kwamba sheria inayosimamia vita dhidi ya dawa hizo imeundwa
kwenye Bunge hili," alisema Ulega.
“Kama haitoshi wabunge bado tunayo kumbukumbu siku alipokuja kipenzi
chetu, Rais Dk. John Magufuli na kuhutubia, tulimshangilia sana
alipotangaza rasmi kwa nguvu zake zote juu ya vita dhidi ya dawa za
kulevya.
"Leo wabunge wameambiwa kwamba hawana jambo isipokuwa wanakuja kufanya kazi ya kulala kwenye Bunge hili.”
KIJANA MZALENDO
Mbunge huyo alisema akiwa kijana mzalendo na Makonda kuwa mdogo wake na
rafiki yake pia, ni lazima Bunge kama chombo huru kiendelee kuheshimika.
“Sisi tunadhani ya kwamba mawili... ama kijana mwenzangu huyu hakuwa anajua anachokisema au amefanya dharau ya makusudi.
"Ninaomba kutoa hoja zifuatazo ili unipe mwongozo tuone tunaendaje
kutoka hapa tulipo, hasa ukizingatiwa sisi ndio ‘number one’ wa
kumsaidia Rais katika vita hii.”
Katika hoja hizo, Ulega aliomba Waziri Mkuu Kassim Majaliwa akiwa
kiongozi mkuu wa serikali, achukue hatua za makusudi ili kuwalindia
heshima wabunge.
“Au kwa kutumia kanuni za Bunge na sisi tunayo kanuni ya haki, kinga na
madaraka ya Bunge, kanuni na sheria basi hatua zichukuliwe kupitia
muhimili huu, au atumie tena vyombo vya habari vile vile kusema kwamba
amekosea na anaomba radhi, naomba mwongozo,” alisema Ulega.
Mbali na Ulega, Mchungaji Peter Msigwa wa Iringa Mjini (Chadema),
alimpongeza Ulega kuomba mwongozo huo wa msingi kwa hadhi ya Bunge.
“Naomba kwenda kwenye kanuni ya 51 ya Bunge ili wabunge tujadili kuhusu
tabia ya Mkuu wa Mkoa huyu anayedhalilisha chombo hiki ambacho ni
muhimili muhimu ambacho kinaweza ku-‘balance’
(kuweka mambo sawa) ili serikali ifanye kazi," alisema Msigwa.
"Naomba tujadili hadhi ya Bunge iweze kulindwa. Naomba kutoa hoja.”
Akijibu mwongozo huo, Chenge alisema: “Nimepokea ombi la mwongozo wa
Ulega na Msigwa ametaka kuchombeza kama hoja ijadiliwe. Mimi
nitajielekeza kwenye ombi la muongozo. Nimemuelewa Mheshimiwa Ulega
maelezo yake mazuri tu."
Chenge alisema Bunge kama taasisi na wajumbe wake na ni moja ya mihimili
mitatu ya dola (ikiwamo serikali na mahakama) lazima liheshimiwe na mtu
yeyote.
“Kwa vile tumejiwekea utaratibu wetu kupitia Kamati ya Kinga, Haki na
Madaraka ya Bunge, ili sasa ikathibitike kama ameyasema hayo (ya sisi
kulala tu ndani ya Bunge) na wapi, lini na kama yanaangukia ndani ya
sheria yetu ya kinga, huko ndiko ukweli wote utakapodhihirika.
“Kwa hiyo mimi kwa suala hili naagiza ofisi ya Katibu wa Bunge, kwa
taratibu zilizopo, wamtake Makonda atoe maelezo yake na kama kweli
amesema au la na watayapokea na kupelekwa kwenye Kamati ya Haki, Kinga
na Madaraka ya Bunge.
"Tutakuwa tupo ndani ya taratibu zetu za kikanuni na ndani ya sheria kwa
kuwa lazima ithibitike kama inaangukia kwa haki za Bunge zinazopaswa
kuheshimika.”
source:Muungwana
source:Muungwana
Comments
Post a Comment