BOSI ALIYEMPA RC MAKONDA HEKARI 1500 AHOJIWA

Mkurugenzi wa kampuni ya Azimio Housing Estate, Mohamed Ikbal, ambaye hivi karibuni alimgawia ardhi, Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda amehojiwa na jeshi la polisi kwa tuhuma za kughushi nyaraka za Serikali.

Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Simon Sirro alithibitisha jana kwamba mfanyabiashara huyo aliitwa kwa ajili ya mahojiano, lakini aliachiwa kwa dhamana baada ya muda kuonekana hautoshi.

“Alikuja na wakili wake, lakini ameachiwa kwa dhamana ataripoti siku nyingine (hakutaja siku),” alisema Sirro. “Anatuhumiwa kughushi nyaraka za Serikali na sasa upelelezi unaendelea.”

Mfanyabiashara huyo inadaiwa kuwa aliripoti polisi jana saa tano asubuhi na kuhojiwa kabla ya kuachiwa kwa dhamana jioni.

Kuhojiwa kwa Ikbal, ambaye kampuni yake iliwahi kushirikiana na Shirika la Hifadhi ya Jamii (NSSF) katika miradi kadhaa tata ya ujenzi, kumekuja siku chache baada ya kumgawia Makonda eneo la ekari 1500 katika kitongoji cha Ligato kijiji cha Kisarawe II wilayani Kigamboni kwa ajili ya viwanda vidogo vidogo.

Siku mbili baadaye, Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi aliibuka na kueleza kwamba eneo aliloligawa mfanyabiashara huyo si lake bali linamilikiwa na serikali na wanakijiji.

“Eneo lile ni la Serikali si la yule mtu aliyejitangaza anampa Makonda na kwa sababu amemdanganya na mimi ndiye msimamizi wa ardhi, nitamsaidia Makonda kuchukua hatua ili watu wasijipendekeze kusafisha maovu yao kwa kutumia migongo ya viongozi,” alisema Lukuvi.

“Hadi siku ile alipokuwa anajipendekeza kwa Makonda, ardhi ile haikuwa yake, wananchi walishashinda kesi mahakamani kwa sababu hakuwa na vielelezo. Ukimdanganya Mkuu wa Mkoa umeidanganya Serikali. Makonda hakuomba ile ardhi ila yeye (Ikbal) ndiye alikwenda kumgawia na amemgawia akijua kwamba alishashindwa kesi,” alisema Lukuvi.

Kwa mujibu wa hukumu ya kesi hiyo Na 147 ya mwaka 2015 iliyofunguliwa na Ikbal katika Baraza la Ardhi la Wilaya ya Temeke dhidi ya Baraza la Ardhi la Kijiji, mfanyabiashara huyo alishindwa.

“Maombi haya yanatupiliwa mbali pamoja na gharama,” ilisema hukumu hiyo ya Januari 13, 2016.

Ijumaa iliyopita mtu aliyejitambulisha kuwa ni mwakilishi wa Ikbal, Kamugisha Katabaro aliibuka na kudai Lukuvi amewasikitisha Watanzania na wataalamu mbalimbali wanaofahamu ukweli wa jambo hilo.

Katabaro alidai Ikbal anamiliki ardhi yenye ukubwa wa ekari 3,500 ambayo aliinunua tangu mwaka 2005 kutoka kwa wananchi wa eneo la Lingato. “Wananchi waliliuza hilo eneo bila ya kushurutishwa kwa kufuata taratibu za kisheria na umiliki wa ardhi,” alidai.

Mwananchi lilimfuata siku hiyo, Waziri Lukuvi aweke wazi kuhusu mmiliki halali wa eneo hilo naye alisema, “Kama mfanyabiashara huyo anaona ameonewa akate rufaa mahakamani.”

Alisisitiza kuwa eneo hilo ni la serikali na watu waliodhulumiwa wameanza kuorodhesha majina yao na wataalamu wa ardhi wapo kwenye eneo hilo wakiendelea na upimaji. “Hiyo ardhi ataipateje wakati mimi ninayo, na kama ana nyaraka zinaonyesha ameshinda mbona hataki kuonyesha anataka kuudanganya umma?” alihoji Lukuvi.

Juhudi za kumpata Ikbal hazikuzaa matunda lakini alipoulizwa Katabaro kuhusu mkurugenzi huyo kuitwa polisi alisema ni kweli alitii wito kama alivyotakiwa na polisi. Taarifa kwamba alikamatwa siyo za kweli kwani alihojiwa na kutoka jana jioni baada ya kuwasili kituoni hapo saa tano asubuhi jana,” alieleza.

Eneo jingine ambalo Azimio ilizua utata ni umiliki wa ardhi na uthaminishaji wake kwa ajili ya mradi wa ujenzi wa mji wa kisasa uitwao Dege Eco Village, Kigamboni. Ulisimama Februari mwaka jana kutokana na utata wa ubia.

Comments

Popular posts from this blog