Waziri Nape: Sikupinga vita dhidi ya biashara ya dawa za kulevya bali nilishauri busara itumike



Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Nape Nnauye ametoa ufafanuzi juu ya kauli iliyonukuliwa ikionyesha kuwa alipinga vita dhidi ya dawa za kulevya iliyoanzishwa na Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda. Amedai kuwa hakupinga vita hiyo bali alitaka busara itumike kwa washukiwa.

Waziri Nape alitoa ufafanuzi huo katika kipindi cha dakika 45 cha ITV, alipoulizwa swali na mtangazaji wa kipindi hicho kutaka kujua kuhusu kauli yake iliyoonesha kupinga utaratibu uliotumika wa kuwakamata au kuwapata watuhumiwa wa dawa za kulevya.

“Niseme kwanza ilitokea nilikuwa na mkutano na waandishi wa habari, ukienda leo ukanitaja Nape ukaniambia baada ya siku mbili njoo kituoni, hata kama nilikuwa na madawa ya kulevya nyumbani kwangu hivi unayakutaje? 

'Kwasababu kwa vyovyote vile nitayachukua, ntayaficha, ntakuja kituoni ntaripoti utanibana ntakwambia twende nyumbani kwangu ukakague mnaenda mnakagua mnakuta hamna, si basi! 

"Kwahiyo nikawa na wasiwasi kwamba inawezekana kabisa nia ilikuwa njema lakini nilidhani pangeweza kutengenezwa utaratibu bora zaidi ya namna ya kuwapata, kwasababu hapa kuna watumiaji, kuna wauzaji na wale ambao wanaleta sasa madawa ya kulevya,” alisema Nape.

Aliendelea, “Ukishughulika na mtumiaji huyu ukadhani ndiye mhalifu wako unakosea, kwasababu huyu ni muathirika na muathirika anahitaji dawa anahitaji huduma ameshaathirika, hapa wahalifu wetu nikuanzia huyu anayemletea halafu kuna huyu anayempa yule aliyemletea, sasa ili uwapate hawa wawili lazima umtumie huyu vizuri ili akupeleke kwa hawa wawili. Lakini ukimkamata huyu ukamtia ndani sasa hawa wawili watakimbia.”

“Kwahiyo mimi nikaona kwamba tunaivuruga vita yenyewe, anayeingiza madawa ya kulevya na anayesambaza kwa maana ya kuyauza, hawa ndiyo tatizo letu. Na ndio maana nikasema hebu tutumieni busara, watu wakadhani nimepinga. 

"Tena mimi nilisema mara nyingi sana tumieni busara namna ya kuiendesha vita hii. Madhara ya kutotumia busara katika vita hii ni makubwa sana, kwasababu ukimweka huyu mtu mmoja ndani hawa wengine wataendelea kuwaathiri wengine na ndiyo maana nasema hii vita tutumieni busara. 

"Hii vita ni ya kupigana kimya kimya kwasababu wanaofanya biashara hii hawaifanyi hadharani wanafanya kwa kificho. Shughulika nao kwa kificho, hii vita hakuna mahali ambapo wameshawahi pigana hadharani, tukitajana hadharani hata wenye chuki watatajana humo humo,” alisisitiza.

Comments

Popular posts from this blog