GARI LA MBUNGE LAUA, MWENYEWE ANUSURIKA
Mtumishi
wa Hospitali ya Wilaya ya Magu mkoani Mwanza, Moses Mjuni amefariki
dunia baada ya kugongwa na gari la Mbunge wa Tarime Mjini (Chadema),
Esther Matiko katika Kijiji cha Kishamba wilayani humo.Mkuu wa Wilaya ya
Magu, Khadija Nyembo alisema jana kwamba ajali hiyo ilitokea juzi saa
mbili usiku, “Gari la mbunge lilimgonga mtumishi wetu wa Hospitali ya
Magu ambaye alikuwa anaendesha pikipiki na dereva wa gari hilo
amekamatwa yupo polisi,” alisema Nyembo.
Akizungumza
kwa simu jana, Matiko alisema ajali hiyo ilitokea takribani kilomita 10
kutoka Daraja la Mto Simiyu wakati akitoka Mwanza ambako walikutana na
mwendesha pikipiki na dereva wake, Kelvin Matango alikuwa akimkwepa
baada ya kuingia upande wake.
“Nilitoka
Mwanza saa 12:00 jioni kwenda jimboni kwangu (Tarime), tulipopita mbele
kidogo karibu kilomita10 kutoka daraja la Mto Simiyu, ghafla
alijitokeza mwendesha pikipiki akawa anaendesha kwa kuyumbayumba na
dereva alishindwa jinsi ya kumkwepa akamgonga, mimi nilikuja kuona yule
mtu ameshafariki dunia,” alisema Matiko.
Matiko
alisema licha ya kwamba hakupata majeraha, baada ya kutokea ajali hiyo
alipelekwa katika Hospitali ya CF ya jijini Mwanza ambako alipewa dawa
na kuruhusiwa.
Hata
hivyo, Matiko alisema alikuwa akisikia maumivu makali ya mgongo na mbavu
hivyo kutakiwa kwenda kufanyiwa vipimo kuona kama atakuwa amepata
madhara.
“Nasikia
maumivu makali ya mgongo na mbavu za kulia, nahisi mkanda wa gari
ulinibana zaidi, nilitakiwa kwenda hospitali ya CF kufanyiwa uchunguzi
lakini nimeshindwa kwa sababu hapa tunapozungumza naenda Magu kumaliza
masuala ya polisi kwani dereva na gari vipo polisi,” alisema Matiko.
Alisema baada ya kumaliza kushughulikia masuala hayo ndipo atarudi tena hospitali kufanya uchunguzi wa afya yake.
Comments
Post a Comment