BILLICANAS YA MBOWE YAANZA KUBOMOLEWA RASMI
Shirika
la Nyumba la Taifa (NHC) limeanza kubomoa jengo la iliyokuwa Klabu
Bilicanas na ofisi za Free Media inayomiliki gazeti la Tanzania Daima
zinazomilikiwa na Mwenyekiti wa Taifa wa Chama cha Demokrasia na
Maendeleo (Chadema) Taifa, Freeman Mbowe, lililopo makutano ya barabara
ya Mkwepu na Indira Gandhi lenye kitalu namba 725-726/24 na hati namba
C. T No. 186018/15 and C. T No. 186018/10.
Ubomoaji
huo ulioanza jana unafanyika wakati Mbowe ameingia katika mgogoro na NHC
baada ya kampuni ya udalali ya Poster and General Traders kumtolea
vyombo nje mwanzoni mwa Septemba, mwaka jana kwa kudaiwa Sh bilioni 1.2
ambayo ni deni la pango ya miaka 20.
Mwanzoni
mwa Septemba, mwaka jana NHC kwa kushirikiana na Kampuni ya Poster and
General Traders, ilifika katika jengo hilo kwa maelekezo ya kutoa
thamani mbalimbali zilizokuwa katika ofisi za jengo hilo na kumpa Mbowe
siku 14 kulipa deni analodaiwa na kuweza kugomboa mali hizo.
Mpango
huo ulisimamiwa na Meneja wa Ukusanyaji Madeni wa NHC, Japhet Mwanasenga
na alisema Mbowe alikuwa na muda wa wiki mbili kwa wakati huo kulipa
fedha hizo kabla ya vifaa vyake kupigwa mnada.
Mwanasenga
alisema taratibu zote zilifuatwa kabla ya kumwondoa mteja huyo ikiwamo
notisi na kwamba vifaa hivyo vitashikiliwa kwa muda huo na endapo
akishindwa kulipa jengo hilo atapangishwa mtu mwingine.
Alisema
shirika hilo linahitaji fedha kwa ajili ya ujenzi na uendelezaji wa
majengo yake hivyo mteja anayedaiwa ajiandae kuondolewa wakati wowote
huku baadhi ya watu wakilihusisha tukio la Mbowe kuondolewa katika ofisi
hizo na masuala ya siasa.
Hata hivyo, Mwanasenga, alisema uamuzi wa kumwondoa katika ofisi hizo hauna uhusiano na masuala ya siasa.
Kutokana
na hali hiyo, Mbowe kupitia Mawakili wake, John Malya na Peter Kibatala,
walifungua shauri la kupinga kuondolewa katika jengo hilo Mahakama Kuu
ya Tanzania na kutaka kurudishwa katika jengo hilo.
Hata
hivyo, maombi hayo yalitupiliwa mbali Oktoba 17, mwaka jana na Jaji
Sivangilwa Mwangesi na kusema kuwa mahakama hiyo imechukua uamuzi huo
baada ya kujiridhisha na hoja kuu tatu kuwa hakuna mkataba wa ubia
uliopo baina ya NHC na Mbowe Hotels Limited na kuwa uhusiano pekee
uliosalia ni wa mpangaji na mpangishaji.
Pia Jaji
Mwangesi alisema mahakama imejiridhisha kuwa NHC imefuata taratibu zote
katika kuiondoa Mbowe Hotels Limited kwa kutoa ilani ya siku 30 na
baadaye siku 14 kabla ya kumtoa mteja wao huyo.
Kuhusu
kusajiliwa au kutosajiliwa kama dalali rasmi wa mahakama wa kuendesha
mchakato wa kumhamisha Mbowe katika jengo hilo, alisema hiyo nayo
haikuwa hoja yenye mashiko na kwamba waombaji walitakiwa kuwasiliana na
Msajili wa Mabaraza ya Ardhi.
Comments
Post a Comment