ASKARI WAUA WATU 4 ARUSHA
WATU
wanne wameuawa kwa kupigwa risasi na askari wa ulinzi wa Shirika la
Uzalishaji Mali la Jeshi la Kujenga Taifa (SUMA JKT) huku mwanafunzi wa
darasa la tatu anayesoma Shule ya Msingi Lemingori iliyopo Oldonyosambu
wilayani Arumeru, Isaya Thomas (13) akiwa miongoni mwa majeruhi wa
shambulio lililofanywa na askari hao.
Kutokana
na tukio hilo, Polisi inawashikilia askari sita wa Suma JKT kwa
uchunguzi dhidi ya tukio hilo lililotokea Kijiji cha Kandaskirieti Kata
ya Oldonyosambu Tarafa ya Mukulati huku miili ya watu wanne waliokufa
kutokana na shambulio hilo, ikiwa imehifadhiwa katika Hospitali ya Mkoa
ya Mount Meru.Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha, Charles Mkumbo
akizungumzia tukio hilo, alisema juzi saa 11 jioni katika Kijiji cha
Kandaskirieti, watu wanne walikufa baada ya kupigwa risasi na askari wa
Suma JKT.
Alisema
taarifa za awali zimebaini kuwa askari hao wa Suma JKT ambao ni walinzi
wa shamba la miti la serikali la Meru Usa Plant, walianza kufanya
operesheni ya kuondoa mifugo, ambako walikamata ng’ombe 45, mbuzi na
kondoo 65 kisha kuwapeleka zizi la serikali lililopo Kituo cha Polisi
Oldonyosambu.
Alisema
saa 11 jioni waliendelea tena na operesheni hiyo na kukamata ng’ombe
wengine 80, mbuzi na kondoo wakiwa 70 na kuwapeleka kwenye zizi la
serikali na wakati wanarudi, ndipo walipokutana na kundi la wananchi
wakiwa na silaha mbalimbali za jadi na kuanza kushambuliwa, hivyo askari
hao walirusha risasi hewani ili kuwatawanya.
Aliongeza
kuwa lakini askari hao walipokuwa wakiwatawanya wananchi hao,
waliendelea kuwashambulia, ndipo na wao walipoamua kuwapiga risasi na
watu wanne walifariki dunia huku wengine watano wakijeruhiwa.
Kamanda
Mkumbo aliwataja waliokufa kuwa ni Mbayani Melau (27), Julius Kilusu
(45), Lalashe Meibuko (25) na Seuri Melita (32) ambao miili yao
imehifadhiwa Mount Meru.
Pia
aliwataja majeruhi waliojeruhiwa kwenye tukio hilo kuwa ni William
Ngirangwa (29), Mathayo Masharubu (34), Julius Lazaro (32), Evelyn Melio
(28) na Isaya Thomas (13), ambao wamelazwa Mount Meru wakiwa
wamejeruhiwa sehemu mbalimbali za miili yao huku hali zao zikiwa si
nzuri.
Akisimulia
tukio hilo, mwanafunzi huyo Thomas alisema alitoka shule vizuri juzi na
kwenda kwao na alifika vizuri nyumbani, kisha baada ya muda akiwa
Oldonyosambu madukani, alishangaa kuona askari wakifyatua risasi ovyo
karibu na watu waliokuwa wakishangaa tukio hilo.
“Mimi
nimetoka shule sijui lolote wakati nashangaa tukio hili nami nimejikuta
nimepigwa risasi mgongoni na mpaka sasa sijapata matibabu nasubiri
kupewa huduma, lakini sijui lolote kuhusu tukio hili kilichoniponza ni
kushangaa ni kwa nini watu wanapigwa risasi,” alibainisha mwanafunzi
huyo.
Majeruhi
mwingine, Julius Lazaro (32), alisema alikuwa kijiweni eneo la
Oldonyosambu madukani ghafla walishangaa kuona askari wakishuka na
kuuliza nani amewapiga mawe, na kuwajibu kuwa hawajui ndipo walipoambiwa
watawanyike na walipotawanyika ghafla alishangaa kusikia milio ya
risasi na yeye kujeruhi wa mguuni.
“Hawa
askari walikuwa ni mchanganyiko maana waliwapiga watu risasi bila kujali
wanahusika na tukio hili au la. Ukweli tumepigwa risasi tusiostahili
kama ni operesheni ya kukamata mifugo msituni kwa nini siye wengine
tupigwe risasi ovyo na hapa hospitali wanahitaji hela na sisi hatuna
sasa sijui hizi risasi tulizonazo itakuwaje,” alieleza Lazaro.
Akizungumzia
tukio hilo, Diwani wa Kata ya Oldonyosambu, Raymond Lairumbe alisema ni
la juzi kati ya saa 11 na 12 jioni, ambako kulikuwa na oparesheni ya
kuondoa mifugo kwenye shamba la Meru Usa Plant ambalo ni shamba la miti
la serikali.
“Hawa
askari walikamata ng’ombe na mbuzi asubuhi kisha kuwaswaga na kuwapeleka
Kituo cha Polisi Oldonyosambu, lakini jioni walikwenda msituni tena na
kuanza kuwapiga hao watu waliokufa kisha kuanza kupiga risasi ovyo
wananchi wangu ambao wengine wamekufa wengine ndio majeruhi akiwemo
mwanafunzi,” alidai diwani.
Alisema
wananchi hao hawatazika miili hiyo hadi hapo viongozi wa serikali,
watakapofika na kuzungumzia suala hilo, kwani wengine wamepigwa risasi
bila ya makosa na walikuwa wakitoka kwenye shughuli zao.
Comments
Post a Comment