Waziri Mkuu Majaliwa Ataka Nyaraka za Faru John Ifikapo Kesho
Waziri
Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Kassim Majaliwa ameugiza
uongozi wa Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro (NCAA), kumpelekea nyaraka
zote zilizotumika katika kumhamisha faru maarufu kwa jina la John katika
hifadhi hiyo ifikapo Desemba 8, 2016.
Majaliwa amesema ana taarifa kuwa
walimhamisha Faru John Kreta kwa siri na kumpeleka V I P Grumet
Serengeti Disemba 17, 2015 na waliahidiwa kupewa sh. milioni 200 ambapo
na wamepewa sh. milioni 100 kwa ahadi ya kumaliziwa sh. milioni 100
nyingine baadaye.
Amesema hayo Desemba 6, 2016
alipotembelea Ofisi za makao makuu ya NCAA, zilizoko wilayani Ngorongoro
mkoa Arusha wakati akizungumza na watumishi wa mamlaka hiyo pamoja na
Wajumbe wa Baraza la Wafugaji ikiwa ni sehemu ya ziara yake ya kikazi
mkoani hapa.
“Naomba niletewe nyaraka zote
zilizotumika kumuomba na kumuondoa faru huyo na barua zilizotumika
kujadili suala la faru John. Nasikia amekufa naomba pembe ziletwe
ofisini na iwapo itathibitika aliondoka bila ya kufuata taratibu
wahusika wote watachukuliwa hatua kali za kisheria,”.
Aidha, Majaliwa amepiga marufuku tabia
ya baadhi ya watumishi wa mamlaka hiyo ambao wanawakabidhi watoto
kupeleka ng’ombe wao ndani ya kreta. “ Watumishi wa Ngorongoro ndiyo
wanaopeleka ng’ombe ndani ya kreta na si wenyeji. Sasa marufuku na
tutakayemkuta hatutakuwa na msamaha naye,”.
Amewataka watumishi hao kuhakikisha
wanakuwa waadilifu na wanafanyakazi kwa kufuata misingi ya kiutumishi na
kuacha tabia za kuendekeza rushwa na wizi.
Wakati huo huo Waziri Mkuu
amemsimamisha kazi Mhasibu Mkuu wa NCAA, Sezzary Simfukwe kutokana na
tuhuma za ubadhilifu wa fedha zinazomkabili na tayari anahojiwa na
Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU).
“Haiwezekani mtumishi awe
anachunguzwa na TAKUKURU halafu aendelee kuwa ofisini si atavuruga
uchunguzi. Asimamishwe kazi kuanzia leo mpaka hapo uchunguzi
utakapokamilika na aikibainika kwamba hana hatia atarudi kazini,”
alisema.
Comments
Post a Comment