Kamati Kuu ya CCM: Leo ni Kikao cha Kwanza kwa Mwenyekiti JPM, Yatakayojadiliwa Yapo Hapa
Dar es Salaam. Kamati Kuu ya CCM
inakutana leo huku kaulimbiu ya “Hapa Kazi Tu” ikitarajiwa kutawala
kikao hicho cha kwanza kwa mwenyekiti John Magufuli, ambaye ameonyesha
dalili za kufumua sekretarieti wakati huu wa kuelekea uchaguzi wake
mkuu.
Kikao hicho cha siku mbili
kitachofuatiwa na kikao cha Halmashauri Kuu ya Taifa, pia kinatarajiwa
kujadili mambo mengine nyeti, kama maandalizi ya uchaguzi utakaofanyika
mwakani kuanzia ngazi ya wilaya hadi taifa kwa kuchagua kamati Kuu mpya
na suala la uchaguzi wa meya wa Kigamboni ambayo sasa ni wilaya.
Pia kikao hicho kinatarajiwa kujadili
chaguzi ndogo za mbunge wa Dimani na madiwani pamoja na ripoti ya
wasaliti ambayo Magufuli alikabidhiwa na mtangulizi wake, Jakaya Kikwete
Julai 23 baada ya kuchaguliwa kuwa mwenyekiti.
Suala jingine linalotarajiwa kuchukua
nafasi ni hali ya kisiasa nchini, ikijumuisha suala la Zanzibar, upigaji
marufuku mikutano ya hadhara, hali ya kiuchumi ambayo inalalamikiwa na
watu wa kada tofauti wakiwemo wafanyabiashara, wananchi na wabunge ambao
walidiriki kuomba ushirikiano na wapinzani wakati wa Bunge la Bajeti
kumshinikiza Waziri wa Fedha na Mipango arekebishe mwenendo wa uchumi.
Kutokana
na jukumu la Kamati Kuu kuwa ni kuandaa ajenda za kikao cha Halmashauri
Kuu, masuala hayo yanatarajiwa kuwasilishwa kwenye chombo hicho cha
pili kwa ukubwa kwa ajili ya maamuzi.
Lakini mabadiliko ambayo yanaonekana ni bayana ni ya sekretarieti.
Rais Magufuli, ambaye alikabidhiwa
nafasi ya uenyekiti baada ya kupata kura zote 2,398 za wajumbe wa
mkutano mkuu wa CCM, amekuwa akiteua wajumbe wa sekretarieti kushika
nafasi kadhaa, hali inayomaanisha kuwa anaweza kuwasilisha mapendekezo
ya majina ya wajumbe wapya.
Mabadiliko ya kiuongozi yanayotarajiwa
ni kusuka upya sekretarieti inayoongozwa na katibu mkuu wa CCM,
Abdulrahman Kinana ambaye anasifika kwa kukipa nguvu chama hicho wakati
wa kuelekea Uchaguzi Mkuu uliopita.
Kinana, aliyeshikilia nafasi hiyo tangu
mwaka 2012, aliomba kujiuzulu pamoja na sekretarieti nzima baada ya Rais
Magufuli kuchaguliwa kuwa mwenyekiti Julai mwaka huu, lakini Rais
akakataa ombi lake.
Kwa kuwa Kinana ameshaonyesha nia ya
kutaka kuachia ngazi, kuna uwezekano mkubwa wa mwenyekiti kuwasilisha
pendekezo la jina la kada atakayeendana na kasi ya “Hapa kazi Tu”
kumbadili mwanasiasa huyo mkongwe.
Hata hivyo, uwezekano mkubwa ni Kinana kuendelea na nafasi yake mpaka Uchaguzi Mkuu wa CCM mwakani.
Kutokana na msimamo wa Rais kuwa hawezi
kumpa mtu mmoja nafasi mbili, ni dhahiri kuwa nafasi ya aliyekuwa katibu
wa itikadi na uenezi, Nape Nnauye itatakiwa kujazwa baada ya kuteuliwa
kuwa Waziri wa Habari.
Kutokana na uteuzi wa Nape, CCM ilimteua
Christopher Ole Sendeka kuwa msemaji wa chama, lakini sasa naye
ameteuliwa kuwa mkuu wa Mkoa wa Njombe na hivyo nafasi yake sasa
inakaimiwa na Selemani Mwenda.
Wengine walioondoka kwenye sekretarieti
ni walioteuliwa kuwa mabalozi, ambao ni naibu katibu mkuu wa CCM-Bara,
Rajab Omari Luhwavi na naibu katibu wa Halmashauri Kuu anayehusika na
siasa na uhusiano wa kimataifa, Dk Pindi Chana.
CCM inatarajiwa kupanga mikakati ya
kuweka mgombea atakayeshinda kwenye uchaguzi wa meya wa wilaya mpya ya
Kigamboni jijini Dar es Salaam, kwa kuzingatia nguvu ya upinzani
iliyopo.
Kwa sasa jiji la Dar es Salaam
linaongozwa na Meya kutoka Chadema, Isaya Mwita, huku manispaa za Ilala
na Ubungo zikiongozwa pia na mameya kutoka chama hicho.
Katika uchaguzi wa marudio uliofanyika
hivi karibuni na kulalamikiwa na vyama vya upinzani, mgombea wa CCM
Benjamin Sitta alishinda na kuwa meya wa Manispaa ya Kinondoni.
Jina la Edward Lowassa limekuwa
likitawala vikao vya CCM tangu waziri huyo mkuu wa zamani aondoke chama
hicho na kujiunga na upinzani mwaka jana. Hakuna shaka kwamba safari hii
jina hilo litarudi wakati wajumbe watakapokuwa wakijadili ripoti ya
wasaliti ambao wanasadikiwa kumuunga mkono Lowassa wakati wa uchaguzi.
Ripoti hizo ziliandaliwa kuanzia ngazi
ya wilaya na baadaye kupatikana moja ambayo Kikwete alimkabidhi Magufuli
Julai mwaka jana.
Mabadiliko hayaepukiki
Wakitoa maoni kuhusu kikao hicho cha
kwanza kwa Rais Magufuli, baadhi ya wasomi na wachambuzi wa masuala ya
siasa wamesema mabadiliko CCM hayaepukiki, lakini yanatakiwa yawe ya
kimfumo. “Ninachotegemea ni kuona mabadiliko,” alisema kada mkongwe wa
CCM, Njelu Kasaka.
“Kwanza tayari baadhi ya waliokuwa
viongozi kwenye kamati kuu na sekretarieti wamepangiwa kazi nyingine,
hivyo ni lazima azibe mapengo ili awe na chombo imara cha kufanyia
kazi,” alisema.
Kuhusu utendaji mpya wa Rais Magufuli
ambaye ndiye mwenyekiti wa CCM, Kasaka alisema ili chama kiendelee kuwa
hai lazima kifanye operesheni za hapa na pale.
“Mtu aliyekabidhiwa madaraka hayo lazima
alete mabadiliko, lazima aweke watu watakaokiinua chama. Hawezi kubaki
palepale alipokikuta. Kwa hiyo tutarajie kuona mikutano ya kukuza
chama,” alisema waziri huyo wa zamani.
Mhadhiri wa sayansi ya siasa wa Chuo
Kikuu cha Dar es Salaam, Dk Alexander Makulilo alisema, mtindo wa
utendaji wa Rais Magufuli serikalini, hautatofautiana na wa kwenye
chama, hivyo lazima atafanya mabadiliko makubwa.
“Nadhani kutakuwa kuna mageuzi kwenye
chama. Anataka kuona chama kwenye mtazamo mpya na anaweza kubadilisha
muundo wa chama. Kwa mfano anaweza kupunguza muundo wenye watumishi
wengi ili kubana matumizi,” alisema.
“Kuna matatizo ameyakuta kwenye chama
kama vile watumishi kudai stahiki zao, lazima atayatatua na kwa kuwa
sasa chama kimetoka kwenye uchaguzi kumekuwa na makundi, lazima ataleta
suluhu ili chama kiwe kimoja.”
Kwa upande wake Profesa Gaudence
Mpangala wa Chuo Kikuu cha Ruaha mkoani Iringa alisema hakutakuwa na
mabadiliko makubwa zaidi ya watu.
“Tusubiri tuone yatakayoamuliwa kwenye
kikao hicho, lakini sitarajii makubwa maana wengine wameshaanza kutabiri
mabadiliko kwenye kamati kuu. Anaweza kubadilisha watu, lakini mfumo
ukabaki pale pale,” alisema Profesa Mpangala.
Comments
Post a Comment