Baada ya Waziri Mkuu Majaliwa Kukabidhiwa Pembe, Mapya Tena Yaibuka Kifo cha Faru John
Dar es Salaam. Kifo cha Faru
John aliyehamishiwa Hifadhi ya Creta ya Ngorongoro kimeendelea kupunguza
idadi ya wanyama hao ambao wanatafutwa kwa udi na uvumba na majangili
kutokana na pembe zake kuuzwa ghali kwenye magendo, mara tatu zaidi ya
dhahabu au dawa za kulevya aina ya cocaine.
Hivi karibuni Waziri Mkuu Kassim
Majaliwa aliliibua sakata la kutoweka kwa Faru John katika Hifadhi ya
Sasakwa Black Rhino Sanctuary akidaiwa kufa.
Kutokana na utata wa sehemu alipokuwa
Faru huyo, makachero saba walifika Ngorongoro kufanya uchunguzi na
kuwakamata maofisa watano waliotajwa kuhusika katika kumhamisha faru
huyo.
Hata hivyo, juzi Waziri Mkuu, Kassim
Majaliwa alikabidhiwa pembe ikiwa ni kithibitisho kuwa Faru John
amekufa. Pia, alipewa taarifa kuhusu utaratibu uliotumika kumhamisha
kutoka Ngorongoro kwenda Sasakwa.
Kilichosababisha Waziri Mkuu awe mbogo
baada ya kuwapo kwa utata wa alipo faru huyo, ni upekee wake, thamani
yake kiutalii na kuwa ni miongoni mwa wanyama walio katika hatari ya
kutoweka duniani.
Ujangili wa wanyama hao, hususan faru
weusi, umepaa kwa kasi barani Afrika ndani ya miaka saba iliyopita
kutokana na kuongezeka kwa mahitaji yake barani Asia, hasa China na
Vietnam ambako inaaminika unga wa pembe za wanyama hao unatibu saratani,
kuondoa mning’inio wa pombe au kumtibu aliyeumwa na nyoka bahari.
Hata hivyo, wanasayansi hawajathibitisha kama pembe hizo ni dawa kama inavyodaiwa.
Idadi ya faru weusi kama marehemu John
(38), ni ndogo zaidi Afrika na inazidi kupungua kutokana na ujangili na
wanapatikana katika nchi chache kama Tanzania, Afrika Kusini, Kenya,
Zimbabwe, Cameroon, Chad na Rwanda ambako walishatoweka.
Kamisheni ya kuwalinda wanyama hao
barani Afrika (AfRSG) ya Shirika la Kimataifa la Kulinda Maliasili
(IUCN) inakadiria kuwa hadi Desemba, 2015 kulikuwa na faru weusi kati ya
5,042 na 5,455, wengi wao wakiwa Afrika Kusini.
Faru weupe, kwa mujibu wa kamisheni
iliyopewa majukumu ya kukusanya takwimu za wanyama hao, wanakadiriwa
kuwa kati ya 19,682 na 21,077 na idadi ya kila nchi imefichwa ili
kuwalinda dhidi ya majangili. Hata wakati biashara ya kimataifa ya pembe
hizo ikipigwa marufuku tangu mwaka 1977 na nchi wanachama wa Mkataba wa
Kimataifa wa Kulinda Wanyama na Mimea Iliyo Hatarini Kutoweka (Cites),
ujangili wa wanyama hao unazidi kupaa kutokana na biashara hiyo haramu
kulipa zaidi.
Mei mwaka jana, gazeti la The Washington
Times la Marekani lilimnukuu Profesa wa Ekolojia wa Chuo Kikuu cha
Oregon, William Ripple akieleza kuwa thamani ya pembe ya faru kwa kilo
katika soko haramu imezidi ile ya dhahabu, almasi au cocaine.
Profesa huyo aliyeshiriki katika utafiti
wa wanyama wala majani waliopo hatarini kutoweka (Collapse of The
World’s Largest Herbivores), alikaririwa akisema pauni moja (gramu 450)
ya pembe ya faru inauzwa Dola 60,000 za Kimarekani, hivyo kufanya pembe
moja ambayo huwa na zaidi ya kilogramu tatu (Pauni 6.6) kuuzwa zaidi ya
Dola 396,000 (sawa na zaidi ya Sh859.3 milioni).
Hadi juzi wakati masoko ya bidhaa
duniani yakifungwa kwa ajili ya wikiendi, dhahabu ilikuwa ikiuzwa kwa
wastani wa Dola 37,250 za Marekani (Sh80.8 milioni) kwa kilo. Thamani ya
kilo moja ya pembe ya faru kwenye soko haramu ni Dola 132,000 zaidi ya
Sh286 milioni. Hii ina maana kuwa thamani ya dhahabu kwa kilogramu
inaingia zaidi ya mara tatu kwa ile ya pembe ya faru.
Uthamani wa pembe hizo, huenda ndiyo
chanzo kilichomfanya Waziri Mkuu, Kassimu Majaliwa kuhakikisha pembe ya
Faru John inamfikia ofisini ili kujiridhisha iwapo alikufa kwa kifo
asili au aliuawa kwa manufaa ya kijangili.
Jarida la National Geographic
lililojikita katika habari za maliasili Septemba mwaka huu lilieleza
kuwa tofauti na pembe nyingine kama za ng’ombe, pembe ya faru
imetengenezwa kwa keratin, protini inayopatikana pia kwenye kucha na
nywele. Iwapo ukiikata pembe ya faru inaota tena.
ICUN inaeleza kuwa idadi ya faru
wanaouwa na majangili Afrika inazidi kukua licha ya jitihada za
kuwalinda na kati ya mwaka 2008 hadi mwaka jana faru walikuwa 5,940.
Mwaka jana pekee waliuawa faru 1,338, kiwango cha juu kwa miongo miwili.
National Geographic linasema mwaka 2008,
faru 262 pekee waliuawa lakini hadi Desemba, 2015 faru 1,342
waliteketezwa na majangiri, idadi ya faru wanne zaidi ya wale
walioripotiwa na ICUN.
Tanzania ni miongoni mwa nchi ambazo
zinahusishwa na ujangili wa wanyama hao adimu ambao mwaka 1996 waliwekwa
na ICUN kwenye orodha ya viumbe vilivyopo katika hatari ya kutoweka.
Ili kuhakikisha wanyama hao wanaendelea
kuwapo, Tanzania imekuwa ikishirikiana na wadau kuwaleta faru hao weusi
wenye asili yake Afrika Mashariki kutoka mataifa mengine hususan Afrika
Kusini ili kuongeza uzao wao.
Miongoni mwa jitihada hizo ni baada ya
Serikali kuwaleta faru weusi watano kati ya 32 waliotakiwa kuletwa
kutoka Afrika Kusini Mei 2010. Hata hivyo, miaka ya awali mmoja
alifariki kwa kifo cha asili, huku mwingine aitwaye George akiuawa na
majangili.
Lakini mpaka mauti yanamfika, Faru John
alikuwa amezaa watoto 26 huku akiacha majike saba yakiwa na mimba.
Majike hayo yakizaa, faru huyo atakuwa ameacha uzao wa faru 33.
Mpaka sasa kuna faru kati ya 47 na 52 wanaoishi maisha ya asili katika Hifadhi ya Ngorongoro.
Comments
Post a Comment