Alichokisema Waziri Mkuu Kassim Majaliwa Kwenye Sherehe za Maulid, Singida
Katika
kusherekea siku ya Maulid ya kuzaliwa Mtume Muhammed (S.A.W), Waziri
Mkuu, Kassim Majaliwa amesema kuwa Serikali itaendelea kuwatumikia
Watanzania wote bila kujali imani zao za kidini.
Majaliwa ameyasema hayo katika sherehe
za kitaifa za Maulid ambazo zimefanyika mkoani Singida na kusema kuwa
kuna matukio ambayo yamekuwa yakijitokeza katika jamii na katika
kuyachukulia hatua za kisheria vitendo hivyo Serikali haitakuwa ikibagua
mtu kutokana na imani yake ya kidini kama jinsi inavyofanya kwa
shughuli za maendeleo.
“Serikali inawashukuru sana kwa
kuendelea kuunga mkono jitihada ya Serikali ya Rais Magufuli, tunaamini
juhudi tunazofanya za kuweka nidhamu kwa watumishi wa umma na taasisi
binafsi mtaendelea kutuunga mkono, tutaendelea kuruhusu uhuru wa kuabudu
na kushirikiana na viongozi wa dini lakini tu mafundisho yanayotolewa
yasikiuke sheria na kanuni za nchi,
“Serikali ipo macho kupambana na
tukio lolote lenye nia ya kupoteza amani ya nchi yetu, Watanzania
tushirikiane kutoa taarifa ili hatua zichukuliwe, ni vyema mtambue ninyi
kama viongozi na waumini ndiyo walinzi wa nchi yetu, niwambie tu kuwa
Serikali itaendelea kuwatumikia Watanzania wote bila kujali dini ya mtu
wala kabila,” amesema Majaliwa.
Nae Mufti Mkuu wa Tanzania, Sheikh Abubakar Zubeiry amesema
“Jambo ambalo Waislamu tunatakiwa kuwa nayo ni kupendana, tufanye kama
Mtume wetu, yeye alikuwa akijenga mshikamano, akijenga upendo akijenga
umoja na kama tunataka kumfata tumwige Mtume katika kupendana, tuache
majungu, fitna na tuache kila kitu kisicho na faida,
“Kwanini mnagombana Waislamu na
nyie ni watu wa Mungu, Waislamu tuwe na mshikamano kama tuliokuwa nao,
pia tunao undugu wa Tanzania, tupendane kama Watanzania na mwenyezi
Mungu ametwambia tusibague hata kama sio Waislamu, Mungu hakatazi mtu
kumtendea wema mtu mwingine kama tu hakufanyi mabaya na hayo ndiyo
mafunzo ya Uislamu.”
Comments
Post a Comment