Wezi Watokomea na Mashine ya ATM Ikiwa na Pesa
NAIROBI:
Polisi jijini Nairobi nchini Kenya wamemkamata mlinzi wa Benki ya
Equity kuhusiana na tukio la wizi lililotokea Jumamosi iliyopita ambapo
watu wanaoaminika kuwa ni wezi waliiba mashine ya kielektroniki ya
kutolea pesa, Automatic Teller Machine (ATM) pamoja na pesa taslim
ambazo hazijafahamika kiasi chake.
Wezi hao walichimba ukuta wa nyuma wa
Benki hiyo na kutoweka na sanduku la uhifadhi wa pesa pamoja na mtambo
wa ATM, pesa zikiwa ndani.
Wakati wakitekeleza tukio hilo,
washukiwa waliweza kuzima kamera za CCTV na pia kengele ya usalama kabla
ya kutekeleza adhma yao ya kuiba mashine na pesa hizo.
Akizungumza na wanahabari, Kamanda wa
Polisi wa Jimbo la Nairobi, Japheth Koome amesema kwamba polisi waliweza
kupata mitungi ya gesi na vifaa vingine ambavyo hutumuka kukata chuma.
Alipoulizwa kama wezi siku hizi wamepata
maarifa na mbinu nyingi kama wacheza filamu, alisema kwamba kwa siku za
hivi karibuni matukio ya wizi kwenye mabenki yanazidi kuongezeka na
yanakuwa ya aina tofauti na wezi hutumia mbinu tofauti kila kukicha.
Mwaka uliopita, wezi waliojifanya
wakaguzi wa hesabu walifika katika benki hiyo na kuingia ndani ambapo
walifanikiwa kupora pesa taslim kiasi cha dola za Marekani 300,000.
Comments
Post a Comment