Wananchi wa Cuba Watoa Heshima za Mwisho Kwa Mwili wa Rais Fidel Castro
HAVANA,
CUBA: Maelfu ya raia wa Cuba wanatoa heshima zao za mwisho kwa kiongozi
mwanamapinduzi Fidel Castro, aliyeaga dunia Ijumaa iliyopita akiwa na
umri wa miaka 90.
Ikiwa ni siku ya kwanza ya kipindi cha
siku tisa za maombelezi rasmi ya kifo chake, misafara mirefu
imeshuhudiwa katika uwanja wa Revolution Square katika Mji Mkuu Havana,
sehemu ambayo waombolezaji wameweka picha ya kiongozi huyo akiwa
ameshika bunduki.
Siku za maombolezi zitakamilika baada ya
majivu ya mwili wake kuzikwa siku ya Jumapili. Majivu ya Castro
yalitazamiwa kuwasilishwa kwa umma katika uwanja wa Revolution Square
lakini yamewekwa katika sehemu tofauti.
‘Roho ya Cuba’
Wananchi wengi wa Cuba walikuwa katika
milolongo hata kabla ya alfajiri kuwadia ili kuhakikisha wako miongoni
mwa watu wa kwanza kutoa heshima zao.
Tania Jimenez, mwenye umri wa miaka 53,
mwanahisabati, ameliambia shirika la habari la AP kwamba Fidel ni kila
kitu kwao, na ni kiungo muhimu kwa nchi hiyo aliyojitolea siku zote
maishani mwake.
Castro aliingia madarakani mwaka 1959,
na kuongoza mapinduzi ya Kikomunisti. Wanaomuunga mkono walisema
ameirejesha Cuba kwa watu wake na wakamsifu kwa mipango ya kijamii
aliyoifanya kama vile huduma za afya na elimu.
Lakini wakosoaji wamemtaja kama,
dikteta, aliyeiongoza serikali ambayo haikuhusiana vyema na upinzani na
kwamba hakuheshimu haki za kibinadamu.
Mtu mwenye ushawishi
Wananchi wamekuwa wakipanga misafara
mirefu eneo lenye picha kubwa ya urefu wa ghorofa tisa iliyotungikwa
kwenye ukuta wa jumba, huku wengi wao wakibeba picha za kiongozi huyo.
Kwa wakati mmoja mizinga 21 ilifyatuliwa
kuadhimisha mwanzo wa maombolezii rasmi mjini Havana na kusini
mashariki mwa mji wa Santiago de Cuba, kutoka sehemu ambayo Castro
alizindua chama cha mapinduzi mnamo mwaka 1959.
Hali katika mji huo ni tofauti
ikilinganishwa na wakati wa kifo cha kiongozi huyo kilipotangazwa.
Sherehe na michezo yote iliahirishwa, huku raia wengi wa Cuba
wakikusanyika kuzungumzia habari lakini walisalia kimya, mwandishi wa
BBC wa Cuba alisema.
Maombolezo yakindelea, maelfu ya raia wa
Cuba wanatarajiwa kuhudhuria sherehe ya makumbusho siku ya Jumatatu na
Jumanne mjini Havana.
Viongozi wa cuba wamesema ”Waombolezaji
wataweka saini za kiapo kuahidi kutekeleza uzalendo na pia kutii kanuni
ya ujamaa iliyodhihirika na kiongozi wao wa kihistoria.”
Revolution Square ndio itakuwa sehemu
ambayo ibada ya misa itakapofanyika ambayo itahudhuriwa na viongozi wa
kimataifa Jumanne jioni.
Rais wa Bolivia Evo Morales na Rais wa
Ecuador Rafael Correa ambao ni marafiki wa karibu wa Cuba,
wamethibitisha kuhudhuria huku Korea Kaskazini ikisema itatuma ujumbe
hadi kisiwa cha Caribbean.
Rais wa Urusi Vladimir Putin aliyempongeza Fidel Castro kama ”rafiki wa dhati na mwaminifu kwa Urusi,” hatahudhuria.
Rais mteule wa Marekani Donald Trump, aliyemtaja Castro kama”dikteta katili” hatahuduria pia.
Bw Trump alitoa tahadhari siku ya
Jumatatu kwamba huenda akafuta uhusiano ambao umekuwa ukiimarika kati ya
Cuba na Marekani chini ya uongozi wa Barrack Obama. Amesema serikali ya
Cuba inastahili kufanya hatua zaidi chini ya maafikiano yake na
Marekani.
Siku ya Jumatatu, safari ya kuzungusha
majivu ya Bw Castro itaanza Santiago de Cuba na inatarajiwa kuwa safari
ya kilomita 1,000.
Majivu yake yatazikwa siku ya Jumapili katika makaburi ya mji wa Santa Ifigenia, sehemu ambayo kiongozi Jose Marti alizikwa.
Comments
Post a Comment