Pedeshee Ndama Kortini Kwa Kugushi Nyaraka na Kutakatisha Bil 1.77
DAR ES SALAAM: Mfanyabiashara wa
jijini Dar, Ndama Shaaban Hussein almaarufu Pedeshee Ndama Mutoto ya
Ng’ombe, aliyewahi kuwa mfadhili wa bendi ya muziki wa dansi ya FM
Academia ‘Wazee wa Ngwasuma’ leo amepandishwa kizimbani katika Mahakama
ya Hakimu Mkazi Kisutu, kwa kosa la utapeli wa dola za Kimarekani 540,
390 sawa na zaidi ya shilingi bilioni 1.18.
Ndama amesomewa mashtaka sita mbele ya
Hakimu Victoria Nongwa na Mwendesha Mashtaka Leonard Msigwa akisaidiana
na Christopher Challo kuwa, mnamo Februari 20, 2014 mkoani Dar, Ndama
alitengeneza nyaraka feki, zikionesha kupata kibali cha kusafirisha
sampuli za madini ya dhahabu kutoka Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo
(DRC).
Shtaka la pili, tatu na nne pia yalikuwa
ya kugushi nyaraka, ikiwemo iliyotoka Umoja wa Mataifa, iliyoisafisha
kampuni yake ya Muru Platnum Tanzania Investment Company Ltd kuwa
imeruhusiwa kusafirisha maboksi manne ya dhahabu.
Nyaraka hizo zililenga kuiaminisha
Kampuni ya Trade TJL DTYL Ltd ya Australia kuwa Muru ni Kampuni halali
kwa biashara hiyo. Pia Ndama alidaiwa kugushi nyaraka zilizoonesha kuwa
alilipa kiasi cha dola 331, 200 sawa na shilingi milioni 728 kwa TRA
kama kodi ya kupitisha mzigo huo hapa nchini.
Shtaka la tano la Ndama ni kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu, kiasi cha dola 540,390 (sawa na shilingi bilioni 1.177)
kutoka kampuni hiyo ya Australia zilizowekwa katika akaunti ya Kampuni
ya Muru katika Benki ya Stanbic na shtaka la sita lilihusu kosa la
utakatishaji fedha hizo.
Ndama amekana mashtaka yote na kesi yake imeahirishwa hadi Desemba 13, mwaka huu itakapotajwa tena. SO
Comments
Post a Comment