Hatima ya Dhamana ya Godbless Lema Kujulikana Leo
ARUSHA:
Mbunge wa Arusha Mjini (Chadema), Godbless Lema, leo, anatarajia kujua
hatima ya dhamana ya kesi ya uchochezi inayomkabili.
Lema anashikiliwa katika mahabusu ya Magereza ya Kisongo mjini Arusha.
Wakili wake, Peter Kibatala amesema walikata rufaa chini ya hati ya dharura kuomba Mahakama isikilize kesi hiyo mapema.
Amesema waliamua kufuata maelekezo ya
Kaimu Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Kanda ya Arusha, Sekela Mosha ya
kuwataka kukata rufaa.
Katibu wa mbunge huyo, Innocent
Kisanyage amesema rufaa hiyo itasikilizwa leo saa tatu asubuhi baada ya
kukamilisha mambo yanayotakiwa.
Lema alirudishwa mahabusu kutokana na
Mahakama Kuu Kanda ya Arusha kukataa kupokea ombi lake la kufanya
marejeo ya uamuzi wa kunyimwa dhamana.
Kaimu Jaji Mfawidhi wa Mahakama hiyo,
Mosha alisema uamuzi uliofanywa na Mahakama ya Hakimu Mkazi umeegemea
kifungu cha Sheria cha Makosa ya Jinai CPA 148, hivyo kilimtaka
mshtakiwa kukata rufaa siyo kuomba Mahakama hiyo kufanye rejea,
Rufaa hiyo itasikilizwa na Jaji Fatuma Massengi, huku Lema akitimiza siku ya 26 tangu apelekwe Gereza la Kisongo.
Comments
Post a Comment