RAIS DKT MAGUFULI ASHUHUDIA RAIS KABILA WA DRC AKIWEKA JIWE LA MSINGI KWENYE JENGO LA MAMLAKA YA BANDARI (TPA) JIJINI DAR ES SALAAM LEO


Rais wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) Mhe. Joseph Kabila akihutubia katika sherehe za uwekaji wa jiwe la msingi la Jengo la ONE STOP CENTRE la Mamlaka ya bandari (TPA) jijini Dar es salaam leo Oktoba 4, 2016.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkr John Pombe Magufuli akimkaribisha mgeni wake Rais wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) Mhe. Joseph Kabila katika sherehe za uwekaji wa jiwe la msingi la Jengo la ONE STOP CENTRE la Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari (TPA) jijini Dar es salaam leo Oktoba 4, 2016





Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli na Rais wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo Mhe. Joseph Kabila Kabange leo tarehe 04 Oktoba, 2016 wamefanya mazungumzo rasmi Ikulu Jijini Dar es Salaam na kisha kuzungumza na wananchi kupitia vyombo vya habari ambapo viongozi hao wawili wamekubaliana kuendeleza na kuimarisha uhusiano na ushirikiano wa kidugu na kihistoria katika nchi hizi mbili marafiki na majirani.
Katika Mazungumzo hayo Rais John Pombe Magufuli amemuhakikishia Rais Joseph Kabila Kabange kuwa Serikali ya Tanzania imechukua hatua kadhaa za kuimarisha huduma katika bandari ya Dar es Salaam na kupunguza vizuizi vya barabarani hadi kubaki vitatu ili nchi ya Kongo na nchi nyingine za kusini na magharibi mwa Tanzania ziitumie bandari hiyo bila vikwazo.
Dkt. Magufuli amesema Tanzania imejiwekea malengo ya kuhakikisha uchumi wake unakua kwa asilimia 7.2 na kwamba kutokana na hali hiyo anawakaribisha wafanyabiashara wa Kongo kuja kuwekeza nchini Tanzania na wafanyabiashara wa Tanzania kwenda kuwekeza nchini Kongo.
"Mhe. Rais Joseph Kabila Kabange takwimu zinaonesha nchi zetu zinafanya biashara kubwa kwani katika mwaka 2009 tulifanya biashara iliyofikia Shilingi Bilioni 23.1 na imekuwa ikikua mwaka hadi mwaka na hivi sasa tunafanya biashara yenye thamani ya shilingi Bilioni 393.6 kwa mwaka.
"Mimi ningependa kuona sisi ndugu na majirani tunafanya biashara zaidi, wafanyabiashara wa Kongo waje Tanzania kuwekeza na Serikali yangu itawaunga mkono" amesema Rais Magufuli.
Aidha, Rais Magufuli amezungumzia mikakati ya kuimarisha mawasiliano ya barabara na ujenzi wa reli ya kati kwa kiwango cha kisasa (Standard Gauge) ambapo Tanzania imetenga Shilingi Trilioni 1 kwa ajili ya kuanza ujenzi huo na kwamba hatua hiyo itarahisisha zaidi usafirishaji wa mizigo ya kwenda na kutoka Kongo kupitia bandari ya Dar es Salaam.
Kuhusu mradi wa ujenzi wa Bomba la mafuta ghafi kutoka Hoima nchini Uganda hadi bandari ya Tanga nchini Tanzania, Rais Magufuli amesema ni matarajio kuwa Kongo ambayo pia imegundua mafuta katika ziwa Albert itatumia bomba hilo kama ambavyo Tanzania pia inatarajia kulitumia kufuatia tafiti kuonesha uwepo wa mafuta katika maeneo ya ziwa Eyasi na Ziwa Tanganyika.
Kwa Upande wake Rais Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo Mhe. Jospeh Kabila Kabange amemshukuru Rais Magufuli kwa mwaliko huu wa ziara ya kiserikali na amemhakikishia kuwa Kongo itaendeleza na kuimarisha zaidi uhusiano wake na Tanzania kwa kuwa nchi hizi ni majirani na ndugu tangu enzi ya Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere.
Mhe. Kabila amesema Kongo inatambua umuhimu wa kushirikiana na Tanzania katika biashara na uwekezaji na kwamba amefurahishwa na hatua ambazo Serikali ya Tanzania imezichukua kuboresha huduma katika bandari ya Dar es Salaam ambayo ni tegemeo kwa usafirishaji wa mizigo ya Kongo Mashariki na sehemu nyingine za nchi hiyo.
Ameahidi kuwa pamoja na kuwahasisha wafanyabishara wa Kongo kuitumia bandari ya Dar es Salaam, Serikali yake itachukua hatua za kurekebisha kasoro zinazolalamikiwa na wafanyabiashara dhidi ya maafisa wa forodha wa Kongo waliopo hapa nchini.
Rais Kabila amezungumzia mradi wa ujenzi wa bomba la mafuta ghafi kutoka Hoima nchini Uganda hadi bandari ya Tanga nchini Tanzania akisema nchi yake pia imeamua kutumia bomba hilo kusafirisha mafuta yake iliyoyagundua katika ziwa Albert upande wa Kongo na pia juhudi zinazoendelea kupata mafuta katika ziwa Tanganyika na amesisitiza kuwa ili kufanikisha hilo ushirikiano ni muhimu.
Kuhusu hali ya usalama nchini Kongo, Rais Kabila amesema kwa asilimia 97 nchi hiyo ina usalama na kwamba ni maeneo machache tu ya mashariki mwa Kongo ndiko kuna vikundi vinavyoendesha vurugu.
"Mhe. Rais Magufuli hivi karibuni tutaanza mazungumzo ya kutafuta amani ya kudumu nchini Kongo, na lengo letu ni kuhakikisha nchi inakuwa na amani kabla, wakati na baada ya uchaguzi mkuu utakaofanyika mwezi Desemba ama baada ya mwezi Desemba" amesema Rais Kabila.
Mhe. Rais Kabila amekubali kuupokea ujumbe wa Mawaziri wa Mambo ya Nje wa nchi za Tanzania, Angola na Msumbiji ambao Mwenyekiti wa asasi ya Siasa, Ulinzi na Usalama ya Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika (SADC - Organ Trioka) Rais John Pombe Magufuli ataituma hivi karibuni kwa ajili kufuatilia hali ilivyo nchini Kongo.
Baada ya mazungumzo rasmi na kuzungumza na wananchi kupitia vyombo vya habari, Rais Kabila anatarajiwa kuweka jiwe la msingi la jengo la Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari (TPA) lililopo kando ya Bandari ya Dar es Salaam na jioni atashiriki dhifa ya kitaifa iliyoandaliwa na mwenyeji wake Rais John Pombe Magufuli.
Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Dar es Salaam
04 Oktoba, 2016
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkr John Pombe Magufuli akihutubia katika sherehe za uwekaji wa jiwe la msingi la Jengo la ONE STOP CENTRE la Mamlaka ya bandari (TPA) jijini Dar es salaam leo Oktoba 4, 2016.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkr John Pombe Magufuli akimkaribisha mgeni wake Rais wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) Mhe. Joseph Kabila kuhutubia katika sherehe za uwekaji wa jiwe la msingi la Jengo la ONE STOP CENTRE la Mamlaka ya bandari (TPA) jijini Dar es salaam leo Oktoba 4, 2016
Rais wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) Mhe. Joseph Kabila akipokea zawadi ya picha ya Bandari ya Dar es salaam kutoka kwa mwenyekiti wa Bodi ya TPA Bw. Ignas Aloys Rubaratuka katika sherehe za uwekaji wa jiwe la msingi la Jengo la ONE STOP CENTRE la Mamlaka ya bandari (TPA) jijini Dar es salaam leo Oktoba 4, 2016.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkr John Pombe Magufuli na mgeni wake Rais wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) Mhe. Joseph Kabila katika sherehe za uwekaji wa jiwe la msingi la wakipata maelezo toka kwa Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA), Mhandisi Deusdedit Kakoko.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkr John Pombe Magufuli akimkaribisha mgeni wake Rais wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) Mhe. Joseph Kabila katika sherehe za uwekaji wa jiwe la msingi la Jengo la ONE STOP CENTRE la Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari (TPA) jijini Dar es salaam leo Oktoba 4, 2016.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkr John Pombe Magufuli akimshuhudia mgeni wake Rais wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) Mhe. Joseph Kabila akifunua pazia kuashiria kuwekwa kwa jiwe la msingi la Jengo la ONE STOP CENTRE la Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari (TPA) jijini Dar es salaam leo Oktoba 4, 2016


PICHA NA IKULU.

Comments

Popular posts from this blog