Ufanyeje unapompenda aliyependwa?
KWANZA
nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu ambaye ameniwezesha kuandika haya
tena wiki hii tukiwa wazima. Lakini pia tumshukuru kwa kutuletea kitu
kinachoitwa mapenzi.
Mpenzi msomaji wangu, kupenda hakuna
macho! Moyo ukishapenda hausikii la kuambiwa. Katika hili ndiyo maana
unaweza kumuona mwanaume kazimika kwa demu ambaye hawaendani kabisa
lakini moyo wake ndiyo umeshapenda.
Ilishawahi kutokea msichana akampenda
kijana mmoja ambaye ni fukara kupita maelezo. Yeye akawa ndiyo
anamhudumia kwa kila kitu. Akamfanyia mpango wa ajira na mwisho wake
wakafunga ndoa.
Sasa hivi wanaishi maisha ya furaha na
amani. Wamegeuka mfano wa kuigwa kwa jinsi wanavyo-pendana lakini huko
nyuma msichana huyo alikuwa akichekwa kwa kutoa penzi kwa mwanaume asiye
na mbele wala nyuma.
Hayo ndiyo mapenzi jamani!
Lakini pia katika kufurukuta kumtafuta
mpenzi wa kuwa naye maishani, mwanaume unaweza kujikuta unaangukia kwa
demu ambaye tayari ana mpenzi wake yaani ameshapendwa. Moyo wako
unakuambia yeye ndiye mtu sahihi katika maisha yako lakini tayari ana
mtu wake, unafanyaje?
Utapambana kuhakikisha unapata kile
ambacho moyo wako umekipenda au utakubaliana na ukweli kwamba huwezi
kuwa naye kwa kuwa ana mtu wake? Inapofikia hatua hiyo unaweza kujikuta
upo njia panda hasa pale ambapo huyo mwenye mtu wake naye anaonesha kuwa
na chembechembe za mapenzi kwako.
Kuna mambo kadhaa ya kukusaidia kukabiliana na hali hii.
Chunguza
Tumia muda wako mwingi kuchunguza juu ya
uhusiano wake. Uhusiano wao umesimama na wanaonekana ni watu wenye
‘future’? Nasema hivyo kwa sababu, yawezekana uhusiano wa huyo
uliyetokea kumpenda ni wa kuzuga tu na huenda wewe ndiye mwenye future
naye.
Usitafute uadui
Baada ya kuchunguza, ukibaini kwamba
uhusiano wao hauko ‘siriasi’, vuta subira, lolote linaweza kutokea na
likaufurahisha moyo wako. Lakini kama utaona ni watu walio siriasi na
wanaelekea kuoana, usitafute uadui bure, kaa pembeni.
Una nafasi kwake?
Sawa umetokea kumpenda msichana aliye na
mtu wake, umeshawahi kujiuliza kama una nafasi ndani ya moyo wake?
Anaonesha dalili fulani za kukupenda kama unavyompenda na ni mtu
anayeonesha kukumisi anapokuwa mbali na wewe? Utakapobaini una nafasi
kwake, uamuzi wa kumpotezea hautakuwa na nafasi.
Ni rahisi kubadili uamuzi wake?
Unadhani huyo uliyetokea kumpenda
anaweza kubadili maamuzi ya kumuacha huyo aliyenaye kama kweli hawana
future? Utagundua hilo kwa kuongea naye na kumsikia kama anaweza kufanya
maamuzi hayo ili awe na wewe.
Pingana na moyo wako
Ifike wakati upingane na moyo wako.
Unajua moyo wako kukuambia kuwa unataka kuwa na uhusiano na demu ambaye
tayari ana mpenzi wake wakati mwingine utakuwa unakupotosha.
Kwa hiyo ukiona vipi, pingana nao. Acha
kumng’ang’ania msichana mwenye mpenzi wake licha ya ukweli kwamba,
huenda wewe ndiye mwenye nafasi ya kuwa mume wake na siyo huyo aliye
naye.
Urafiki ni poa?
Umempenda sana na hauko tayari kumkosa
katika maisha yako lakini imetokea kwamba tayari yuko na mtu na umebaini
huna nafasi kwake kabisa? Usiumie, omba angalau urafiki. Siyo urafiki
wa kivile sana ila angalau pale unapotaka kusikia sauti yake kwa
kumsalimia tu, upate nafasi hiyo.
Usiumie, yupo mwingine
Haina haja ya kujitafutia vidonda vya
tumbo bure kwa kuwa tu umebaini uliyetokea kumpenda tayari ana mtu.
Chukulia ni hali ya kawaida, mademu wazuri ambao wanaishi singo wapo
kibao huko mtaani ni suala la wewe kutulia tu. Amini yupo mwingine
ambaye atayafanya maisha yako yawe ya furaha.
Naomba nihitimishe kwa kusema kwamba,
unapotokea kumpenda mtu fulani, pambana kuhakikisha unampata kwa sababu
ukimkosa maisha yako yanaweza kuwa gizani. Ila pale utakapoona uwezekano
wa kuwa naye haupo, usilazimishe ndugu yangu. Kumbuka haya ni maisha
tu!
Comments
Post a Comment