Salum Mwalimu na Wafuasi 18 wa Chadema Waachiliwa kwa Dhamana
Mahakama
ya Hakimu Mkazi Simiyu imewaachia kwa dhamana Naibu Katibu Mkuu wa
Chadema (Zanzibar), Salum Mwalimu na wafuasi wengine 18 wa chama hicho
baada ya kukaa mahabusu kwa zaidi ya siku 12.
Kiongozi huyo wa Chadema na wafuasi
hao 18 walikuwa wakishikiliwa katika mahabusu za jeshi la polisi kwa
tuhuma za kuandaa na kuhamasisha maandamano na mikutano ya Oparesheni ya
chama hicho iliyopewa jina la UKUTA, ambayo ilipigwa marufuku na jeshi
hilo.
Walifanikiwa kupata dhamana baada ya
Hakimu wa Mahakama hiyo kueleza kuwa ameridhia hoja za upande wa utetezi
baada ya kusikiliza pande zote mbili na kubaini mapungufu kwenye maombi
ya upande wa mashtaka.
Awali, Mwendesha mashtaka aliitaka
Mahakama hiyo kuwanyima dhamana washtakiwa hao kwa madai kuwa endapo
wataachiwa wataendelea kufanya kosa hilo.
Hata hivyo, Hakimu alitupilia mbali
maombi hayo akieleza kuwa wameshindwa kuthibitisha pasipo shaka kuwa
endapo washtakiwa hao wataachiwa watafanya tena kosa hilo.
Pia, Hakimu alieleza kukubaliana na
hoja ya washtakiwa hao kuwa hati ya kiapo iliyowasilishwa mahakamani
hapo na mwendesha mashtaka ilikuwa na mapungufu ya kisheria.
“Ninakubaliana na upande wa utetezi kuwa hati ya kiapo iliyowasilishwa ina mapungufu ya kisheria,” alisema Hakimu baada kupitia na kugundua kuwa aliyesaini hati hiyo sio anayeonekana kuitoa.
Washtakiwa wote walitimiza masharti ya
dhamana kwa kuwasilisha wadhamini wawili kila mmoja ambaye ataweka
dhamana ya shilingi milioni 3.
Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe
alikuwa miongoni mwa watu waliohudhuria mahakamani hapo na kuondoka na
Salum na wafuasi hao ambao walifikishwa mahakamani hapo awali chini ya
ulinzi mkali. Kesi imeahirishwa hadi Oktoba 4 mwaka huu.
Comments
Post a Comment